Alhamisi, 25 Novemba 2021

BENKI YA DUNIA YAIPONGEZA MAHAKAMA YA TANZANIA UWEKEZAJI KWENYE TEHAMA

Na Faustine Kapama na Lydia Churi, Mahakama

Mahakama ya Tanzania imepongezwa na Benki ya Dunia kwa uwekezaji mkubwa iliyofanya katika kutoa huduma mbalimbali za kimahakama kwa kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Hayo yamebainshwa leo tarehe 25 Novemba, 2021 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwenye hafla ya kuwaapisha Naibu Wasajili 27 wapya, uapisho ambao uliyofanywa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani.

“Sisi tumefanya uwekezaji mkubwa sana katika teknolojia. Mkurugenzi wa Benki ya Dunia alipotutembelea juzi alishangazwa na hatua kubwa ambayo tumepiga. Yeye anatoka nchi ya Indonesia lakini anasema atatuma watu waje wajifunze kutoka kwetu,” Mhe. Prof. Juma aliwaeleza viongozi mbalimbali waliohudhuria uapisho huo.

Hata hivyo, alielezea wasiwasi wake kama mtu huyo akija siku hiyo akakutana na kiongozi ambaye mapinduzi hayo ya teknolojia yamempita. “Ni kiongozi, ni Naibu Msajili, lakini haelewi Mahakama tunakwenda wapi, yule atatoka na hisia kwamba sisi sio wakweli.  Kwa hiyo uwekezaji mkubwa tulioufanya katika maeneo ya TEHAMA lazima tuuedeleze,” alisisitiza.

Hivyo, Jaji Mkuu aliwataka Naibu Wasajili hao kuwa injini na moyo kwenye maendeleo ya TEHMA kwa kuwa wote wanafahamu dunia inakokwenda  na kwa kuzingatia kasi ya madadiliko na kwa kiasi gani teknolojia inavyoweza kuwabadilisha.

Mhe. Prof. Juma pia alielezea kufurahishwa na maendeleo makubwa ambayo yamefikiwa na Mahakama ya Tanzania katika usajili wa mashauri kwa njia ya mtandao (e-filing), hatua ambayo ni chanya na imepokelewa vizuri na wananchi kwa ujumla. “Hivi sasa e-filing ni kama asilimia 100. Hata wananchi wanakubali kwamba mashauri yasajiliwe kwa njia ya mtandao, Sasa kuna nafasi ya kuendeleza kwa vile wananchi wanataka zaidi,” alisema.

Aliyataja maeneo mengine ambayo yamekonga nyoyo za viongozi wa Benki ya Dunia ni usikilizaji wa mashauri kwa Mkutano Mtandao (Video Conference) hatua ambayo imesaidia sana hasa wakati wa janga la ugonjwa wa Uvico-19 na pia uwekezaji ambao umefanywa kwenye mfumo wa kupandisha hukumu za Mahakama (Tanzill).

“Wote mnafahamu Uamuzi hasa wa Mahakama ya Rufani kila siku unapotoka hupandishwa kwenye mtandao. Kwa upande wa Mahakama Kuu, tumefanya utafiti kuna Majaji wengine wamemaliza kutoa hukumu zao, lakini hazipandishwi, Hapa huwezi kumlaumu Jaji, yeye akishamaliza inabaki kazi ya Msajili. Kama hakuna upandishwaji,  Msajili  Mkuu atawafuata ninyi,”aliwaambia Naibu Wasajili hao.

Jaji Mkuu pia alitumia nafasi hiyo kuwapa ushauri kwa upole kabisa viongozi hao  juu ya mambo mbalimbali ambayo wanatakiwa kuzingatia wanapotekeza majukumu yao mapya katika muktadha mzima wa utoaji haki kwa wananchi.

Aliwaona Naibu Wasajili hao kama madaraja unganishi, ambalo linaunganisha watumishi wa Mahakama na viongozi, wadau wa shughuli za kimahakama na pia huunganisha viongozi wa Mahakama na maelekezo na sheria mbalimbali zinazotungwa na kuhakikisha zinafika kwa wahusika.

“Shughuli zenu ni muhimu sana katika uboreshaji wa shughuli za Mahakama. Nyinyi kama viongozi katika masjala ndiyo taswila ya Mahakama, kwa sababu mtu anapofika kwa mara ya kwanza, kituo cha kwanza mara nyingi ni masjala. Ingawa katika Vituo Jumuishi tutakuwa na wale watakaopokea na kuelekeza wapi pa kwenda, lakini hadi kufikia sasa ni masjala ndiyo kituo cha kwanza,”alisema.

Jaji Mkuu alisema kuwa kwa sababu wao ndio wasimamizi wa hizo masjala chochote kinachotokea pale huwa kinaashiria uongozi wao. Alitoa mfano wa lugha ambayo inaweza kutumika katika kumhudumia mwananchi kama ikiwa ni ya kistaarabu ni Msajili ndiye atakuwa anajenga ustarabu katika hiyo masjala. Hivyo, alibainisha kiuwa yote yanayofanyika katika masjala yanamchango mkubwa katika upatikanaji wa haki na yanaumuhimu katika kujenga imani ya wananchi.

“Wakati mwingine mwananchi anajenga imani siku ya kwanza anayofika mahakamani. Akipokelewa vizuri anakuwa na imani kuwa anaenda kupata haki. Lakini akifika siku ya kwanza anakutana na sura au dalili za rushwa, anapokutana na lugha kali ya kutisha  hiyo ndiyo picha atakayoondoka nayo mahakamani,” alisema.

Jambo lengine ambalo Mhe. Prof. Juma alisisitiza ni uwepo wa mahusiano mazuri kati ya Naibu Msajili na watumishi wengine waliopo chini yake ambapo kuna maelekezo ambayo hutolewa na vingozi wa ngazi za juu lakini huishia kwa wasajili pekee bila wengine kujua.

“Utakuta kuna barua, maelekezo na nyaraka mbalimbali ambazo zinatoka kwa viongozi kama Majaji Wafawidhi, Jaji Kiongozi na zingine zinatoka kwa Msajili Mkuu na tunadhani ni barua zetu wenyewe. Hakikisha waliochini yako wanelewa hayo maelekezo mara barua na nyaraka zinapofika kwako,” aliwaambia Naibu Wasajili hao.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifafanua jambo alipokuwa anaongea na Naibu Wasajili 27 wapya mara baada ya kuapishwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani leo tarehe 25 Novemba, 2021 jijini Dar es Salaam.


Sehemu ya Naibu Wasajili 27 wapya wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma  mara baada ya kuapishwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani leo tarehe 25 Novemba, 2021.


Sehemu ya Naibu Wasajili 27 wapya wakichukua kumbukumbu muhimu wakati Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma  alipokuwa anaongea nao.


Sehemu nyingine ya Naibu Wasajili 27 wapya wakimsikilza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma. 

Naibu Wasajili wengine (juu na chini) wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma  na kuchukua kumbukumbu muhimu. 

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (waliokaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Wasajili 27 wapya (waliosimama) baada ya kuapishwa leo tarehe 25 Novemba, 2021 Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam. Wengine waliokaa, kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani na kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (waliokaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Wasajili wapya wanawake (waliosimama)ambao waliungana na Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe.Joaquine De Mello (aliyevaa suti nyeupe).Wengine waliokaa, kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani na kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni