Jumatatu, 29 Novemba 2021

HAKUNA SABABU YA KUGOMBEA FITO: JAJI KIONGOZI

 Na Faustine Kapama, Mahakama-Lushoto

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amewataka Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama nchini kushirikiana kwa karibu na kuacha kugombea fito na madaraka wakati wa kutekeleza majukumu ya utoaji haki kwa wananchi.

Mhe. Siyani ametoa wito huo leo tarehe 29 Novemba, 2021 wakati anafungua mafunzo elekezi ya siku tano kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

“Usimamizi wa utekelezaji wa majukumu yote yanayosaidia katika utoaji wa haki umo mabegani mwenu. Mkiwa wamoja, imara na madhubuti katika kazi zenu, tutaifikia dira yetu kwa haraka zaidi, vinginevyo safari yetu itakuwa ndefu. Nitumie fursa hii kusisitiza ushirikiano, upendo, kuheshimiana na kusaidiana baina yenu ili kazi iendelee. Msiende kugombea madaraka,” alisema.

Kwa mujibu wa Jaji Kiongozi, makoti ya uongozi waliyovikwa na Watanzania wanapaswa kuyatumia vizuri ili kuwaletea maendeleo, hivyo umoja miongoni mwa viongozi ni muhimu katika mafanikio ya aina yoyote. Alibainisha kuwa kwa kuwa viongozi hao wanajenga nyumba moja, hakuna sababu ya kugombea fito, hivyo ni budi kuwa kitu kimoja.

Mhe. Siyani aliwakumbusha viongozi hao jambo jingine muhimu linalohusu uhuru wa Mahakama, huku akibainisha kuwa uhuru unaokusudiwa sio ule wa kuifanya Mahakama ya Tanzania kuwa kisiwa. “Sisi tumekasimiwa jukumu la kusimamia haki nchini na uhuru wetu ni kwenye kuamua juu ya haki za watu. Uhuru huo unapaswa kulindwa kwa kusudi la kujenga na sio kubomoa. Ni vema kila mmoja wetu akaheshimu na akaulinda uhuru huo lakini pia kuheshimu mipaka ya mihimili mingine,” alisema.

Jaji Kiongozi alibainisha pia kuwa Mahakama inatekeleza Mpango Mkakati wake wa Miaka Mitano wenye nguzo kuu tatu ambazo ni Utawala, Uwajibikaji na Matumizi ya Bora ya Rasilimali; Upatikanaji wa haki sawa kwa wote na kwa wakati; na Kujenga taswira chanya na Kurejesha imani ya wananchi kwa Mahakama. Hivyo, aliwasihi katika utendaji wao kuzingatia nguzo hizo zote kwa uaminifu, bidii na uadilifu, kila mmoja kwa nafasi yake na kuonya kuwa matokeo ya kazi za kila mmoja wao yatapimwa kwa kutumia nguzo hizo tatu.

Mhe. Siyani alisema kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mahakama ina wajibu wa kutoa haki kwa wote na kwa wakati kama inavyoelezwa katika Ibara ya 107A na ili kuweza kutekeleza majukumu ya utoaji haki vema viongozi wote hawana budi kuwa na uelewa wa kutosha juu ya masuala ya sheria na haki kwa ujumla. Alikumbushia kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Hamis Juma mara kwa mara amekuwa akisisitiza kuwa watumishi wote wa Mahakama wanatakiwa kuwa na ujuzi na uelewa wa kutosha wa majukumu yao na nafasi zao.

“Hivyo, ni kwa muktadha huo mafunzo haya yameandaliwa ili kuweza kutimiza hitaji la kikatiba Pamoja. Binafsi nimepata nafasi ya kupitia ratiba yenu ya mafunzo kwa siku tano zijazo. Nimefurahi kuona kuwa mada zilizopo katika ratiba hiyo zinalenga kutukumbusha yatupasayo kufanya ili kutimiza nguzo hizo tatu za Mpango Mkakati,” Jaji Kiongozi alisema.

Akitoa neno la shukrani, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma alishukuru uongozi wa Mahakama na Chuo kwa ujumla kwa kuwezesha mafunzo hayo, huku akiahidi kwa niaba ya Naibu Wasajili na Watendaji kutekeleza maelekezo yote aliyoyatoa Jaji Kiongozi katika kuwatumikia Watanzania wakati wakitekeleza majukumu yao ya utoaji haki kwa umma.

“Tutafanya yote tutakayoweza kwa kadri tutakavyojaliwa kuweza kutimiza malengo ya kitaasisi. Migongano( baina ya viongozi) inaweza kuwepo, kama ambavyo hata kwenye vitabu vya dini wanasema majaribu hayanabudi kuja, ila ole wake ayaletaye,” alionya Mhe. Chuma.

Akitoa neno la salamu kabla ya Jaji Kiongozi kufungua mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel alibainisha kuwa Mahakama ya Tanzania ni Mhimili mkubwa, hivyo kuwa na watu sahihi, wenye taaluma sahihi na wabobezi sahihi ni jambo la msingi sana, hivyo hawatapoteza chochote katika kuwekeza katika uelewa wa watu. Alimhakikishia Jaji kiongozi kuwa sio kwa Naibu Wasajili tu na Wakurugenzi Wasaidizi waliojiunga hivi karibuni, bali pia Mahakama itaendelea kutoa mafunzo kwa kada zote.

“Nimeshaongea na Mkuu wa chuo watengeneze program fupi ya mafunzo kwa ajili ya makatibu muhtasi, watunza kumbukumbu na pia madereva wetu ambao wakati sisi tumelala kwenye magari wao wanatuendesha masaa yote, angalau nao waje Lushoto ili waweze kufurahia kazi zao wanazofanya. Nina amini hilo litafanyika,” alisema.

Katika mafunzo hayo, mada mbalimbali zitawasilishwa na waezeshaji waliobobea katika maeneo mbalimbali, akiwemo Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, Jaji Mkuu Mstaafu ,Mohamed Chande Othman, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. January Msoffe, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati na watendaji wengine waandamizi wa Mahakama.

Miongoni mwa mada zitakazowasilishwa kwenye mafunzo hayo zinajumuisha Uongozi wa Kimkakati, Stadi za Uongozi na Uwezo wa Kukabili Mabadiliko, Wajibu wa Mahakama, Utamaduni wake na Uhusiano wake na Mihimili Mingine ya Dola, Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama na Uboreshaji unaofanywa na Mahakama, Maadili ya Watumishi wa Umma na Maadili ya Kimahakama, Usimamizi wa fedha na Manunuzi ya Umma pamoja na Usimamizi wa Nyaraka.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akizungumza wakati wa ufunguzi mafunzo elekezi ya siku tano kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA). Ufunguzi wa mafunzo hayo umefanyika leo tarehe 29 Novemba, 2021.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel akisisitiza jambo wakati akitoa salamu zake kabla ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani kufungua mafunzo elekezi ya siku tano kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

Msajili Mkuu wa Mahakama, Mhe Wilbert Chuma akitoa neno la shukrani mara baada ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani kufungua mafunzo elekezi ya siku tano kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (katikati) akifuatilia jambo wakati wa mafunzo elekezi kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama. Kutoka kulia kwa Jaji Kiongozi ni Naibu Mkuu wa Chuo cha IJA anayejihusisha na Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Fatihiya Masawe na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, wakati kushoto kwake ni Msajili Mkuu wa Mahakama, Mhe Wilbert Chuma na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kelvin Mhina.
Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kelvin Mhina akitoa utambulisho wa washiriki wa mafunzo hayo.

Wajumbe wa Sekretarieti wakiongozwa na Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Mafunzo Mahakama ya Tanzania, Bi Patricia Ngungulu (wa pili kushoto), wakifuatilia mambo mbalimbali wakati wa mafunzo yanayotolewa kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama.
Sehemu ya Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama wanaoshiriki mafunzo hayo.


Kundi jingine la Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama wanaoshiriki mafunzo hayo.

Wajumbe wa meza kuu wakiongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (waliokaa katikati) wakiwa katika picha ya pamoja (juu na chini) na baadhi ya washiriki wa mafunzo. Wengine waliokaa kutoka kulia kwa Jaji Kiongozi ni Naibu Mkuu wa Chuo cha IJA anayejihusisha na Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Fatihiya Masawe na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, wakati kushoto kwake ni Msajili Mkuu wa Mahakama, Mhe Wilbert Chuma na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kelvin Mhina.



Wajumbe wa meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama wanaoshiriki katika mafunzo.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (waliokaa katikati) na wajumbe wengine wa meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Wasajili waliowahi kusoma katika chuo cha IJA wanaoshiriki katika mafunzo.

Wajumbe wa meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mahakimu kutoka Mahakama ya Lushoto.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (waliokaa katikati) na wajumbe wengine wa meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti ya mafunzo.

Wajumbe wa meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti ya IJA na Makatibu.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni