Na Faustine Kapama na Rosena Suka, Mahakama-Lushoto
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani leo tarehe 29
Novemba, 2021 amefungua mafunzo elekezi ya siku tano kwa Naibu Wasajili na
Watendaji wa Mahakama ambapo amekisisifia Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
(IJA) kwa mchango mkubwa kinachofanya na kujenga taaluma
bora kwa watumishi wa Mahakama na wananchi wengine kwa ujumla.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku tano yanayowashirikisha viongozi hao, Mhe. Siyani amebainisha kuwa Chuo kwa
kushirikiana na Kitengo cha mafunzo cha Mahakama ya Tanzania wamekuwa wakifanya kazi
nzuri kwa kutoa mafunzo mbalimbali elekezi na endelevu kwa watumishi wa
Mahakama ya Tanzania.
“Kama ilivyo kwa wengine, mimi nina imani kuwa
chuo hiki kweli ni kitovu na kisima cha elimu bora. Kimsingi, chuo hili kina
uwezo wa kujenga taaluma na kufanya leo hii tuna Wasajili ambao kesho ni Majaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania. Kwa hiyo, mimi niwapongeze sana na nifikishie salamu zangu kwa Mkuu
wa Chuo,” Jaji Kiongozi alimweleza Kaimu Mkuu wa Chuo, Prof. Fatihiya Massawe,
ambaye pia ni Naibu Mkuu wa IJA, Mipango, Fedha na Utawala.
Amesema kuwa
mafanikio katika utoaji wa mafunzo elekezi ya awali na mafunzo endelevu ya
kimahakama ni mojawapo ya matunda ya kazi nzuri yanayofanywa na IJA kwa
kuzingatia Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya mwaka 2019 ambayo inakitambua Chuo hicho
kama kitovu au kisima cha utoaji mafunzo kwa watumishi wa Mahakama, lakini vile
vile utafiti wenye lengo la kuongeza tija na kuboresha utendaji wa Mahakama ya
Tanzania.
Jaji Kiongozi
aliwakumbusha washiriki kuwa mafunzo ambayo yameandaliwa kwa ajili yao yamelenga
kuwapa mbinu na nyenzo sahihi za kuweza kukabili changamoto mbalimbali za kiutendaji.
“Hivyo muwe wazi kuuliza maswali na kuchangia uzoefu kila mmoja kwa namna
ambayo mnaona italeta matokeo chanya katika utendaji kazi wenu. Shabaha ya kila
mmoja wetu iwe ni utoaji wa haki na kuliletea maendeleo taifa letu na
kutekeleza kwa vitendo Mkataba wa Huduma kwa Mteja,” amesema.
Mhe.
Siyani alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha washiriki wa mafunzo hayo kuwa wapo katika
kipindi cha mapinduzi ya nne ya viwanda na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma amekuwa akisisitiza watumishi wa Mahakama kujinoa zaidi
kwenye eneo la TEHAMA ili waweze kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidunia hivi
sasa.
Amebainisha
kuwa miongoni mwa mada zitakazotolewa katika mafunzo hayo inahusu TEHAMA, hivyo
ni imani yake kupitia mada hiyo washiriki wote watapata nafasi ya kujifunza juu
ya nafazi zao katika usimamizi wa mashauri kwa njia za kielektroniki. Aliwaomba
kutumia fursa hiyo kupata kitu cha nyongeza katika eneo hilo na kwamba kila
mmoja wao awe mfuasi wa karibu wa TEHAMA kama dunia inavyowataka hivi sasa.
“Tambueni
kwamba tunakoelekea hakutakuwa na nafasi kwa Msajili au Mtendaji
asiye na uelewa wa TEHAMA katika Mahakama yetu. Hiyo ni dhahiri kwa sababu
ninyi ni wasimamizi wa mifumo ikiwemo ya TEHEMA na bila shaka msimamizi bora ni
yule anayefahamu anachokisimamia,” aliwaambia viongozi hao wa Mahakama ya
Tanzania.
Awali akitoa
neno la ukaribisho, Kaimu Mkuu wa Chuo, Prof. Fatihiya Massawe alisema kuwa
mafunzo yanayotolewa kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama siyo ya kwanza
kutolewa hapo Chuoni, kwani IJA imekuwa ikitoa mafunzo elekezi (Induction) kwa
wahesimiwa Majaji wote wapya wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na mafunzo ya awali
na elekezi kwa Majaji wote wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Zanzibar
wanapoteuliwa kwenye wadhifa huo na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani
pamoja na Rais wa Zanzibar.
Kwa mujibu
wa Prof. Massawe, vilevile IJA imekuwa ikiendesha mafunzo elekezi kwa Mahakimu
wote mara wanapoajiriwa kujiunga kwa mara ya kwanza na utumishi wa Mahakama kwa
lengo la kuwajengea uwezo wa kutenda haki kwa wote na kwa wakati kwa kuzingatia
misingi ya sheria na uadilifu.
“Hii ni
mara ya kwanza mafunzo ya namna hii yametolewa kwa Naibu Wasajili na hata kwa
Watendaji. Tunapenda kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kulisimamia hili.
Tunaamini mafunzo haya elekezi ni mwanzo tu wa mafunzo endelevu ambayo
washiriki hawa wataendelea kupata kama watumishi wa Mahakama. Chuo kinaahidi
kitaendelea kutayarisha programu za mafunzo kulingana na uhitaji kadri
watakavyoendelea kutekeleza majukumu yao na kubaini changamoto katika maeneo ya
uhitaji wa mafunzo,” alisema.
Katika
mafunzo hayo, mada mbalimbali zitawasilishwa na waezeshaji waliobobea katika
maeneo mbalimbali, akiwemo Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole
Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, Jaji Mkuu
Mstaafu ,Mohamed Chande Othman, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe.
January Msoffe, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati na
watendaji wengine waandamizi wa Mahakama.
Miongoni
mwa mada zitakazowasilishwa kwenye mafunzo hayo zinajumuisha Uongozi wa
Kimkakati, Stadi za Uongozi na Uwezo wa Kukabili Mabadiliko, Wajibu wa
Mahakama, Utamaduni wake na Uhusiano wake na Mihimili Mingine ya Dola, Sheria
ya Uendeshaji wa Mahakama na Uboreshaji unaofanywa na Mahakama, Maadili ya
Watumishi wa Umma na Maadili ya Kimahakama, Usimamizi wa fedha na Manunuzi ya
Umma pamoja na Usimamizi wa Nyaraka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni