Na Faustine Kapama na Lydia Churi, Mahakama
Mafunzo elekezi yanayotolewa
kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto (IJA) yameendelea leo tarehe 30 Novemba, 2021 ambapo Jaji Mkuu mstaafu,
Mhe. Mohamed Chande Othman na Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. January
Msoffe wamewakumbusha viongozi hao mambo muhimu ambayo wanapaswa kuzingatia
wanapotekeleza majukumu yao ya kimahakama.
Aliyekuwa
wa kwanza kuwanoa viongozi hao alikuwa Mhe. Chande, ambaye aliwapitisha katika
Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama (the Judiciary Administration Act) ya mwaka
2011, ambayo imekuwa nguzo muhimu katika kuwawezesha viongozi na watendaji mbalimbali
wa Mahakama katika kutimiza wajibu wao bila kutegemea Mhimili mwingine wa dola.
Jaji Mkuu
huyo mstaafu alifafanua madhumuni makubwa ya kuanzishwa kwa sheria hiyo ikiwemo
kuimarisha uhuru wa Mahakama, kuongeza uhuru wa kitaasisi na watumishi wa Mahakama
katika kutekeleza majukumu yao, kuimarisha utawala wa haki na kurahisisha
utawala wa Mahakama.
Kwa
mujibu wa Mhe. Chande, kutungwa kwa sheria hiyo pia kuliondoa ubishi wa
madaraka ya Jaji Mkuu ambapo katika kutekeleza majukumu yake, sheria hiyo
inampa mamlaka ya kudai matokeo ya utendaji kazi kwa kila kiongozi, wakiwemo Majaji
na Mahakimu, mfano kujua ni mashauri mangapi yaliyosikilizwa katika kipindi
kilichowekwa na kupima utekelezaji wa shughuli za kimahakama.
Alibaisha
pia kuwa kutokana na sheria hiyo, shughuli zote za kiutendaji, ikiwemo kuajiri watendaji na kuchukua hatua za kinidhamu hufanywa na Mahakama yenyewe badala ya shughuli
hizo kufanywa na taasisi nyingine ndani ya Serikali. Pia sheria hiyo iliwezesha
kuanzishwa kwa mfuko maalum wa Mahakama, hatua ambayo imesaidia kuongeza
ufanisi katika kutekeleza shughuli mbalimbali katika mfumo mzima wa utoaji
haki.
Hata
hivyo, baadhi ya wachangiaji wa mada hiyo, Bw. Sostenese Mayoka na Bw. Geofrey
Mashafi, ambao ni Watendaji wa Mahakama na Mhe. Judith Kamala, Naibu Msajili,
walielezea namna ambavyo viongozi wa Mahakama wana kazi ya kufanya katika
kuuelimisha Umma juu na mawazo hasi waliyonayo juu ya Mahakama kwa ujumla.
Kwa mujibu
wa wachangiaji hao, kumekuwepo na mawazo potofu kwamba mwananchi wa kawaida
hawezi kupata haki kirahisi kama akipeleka shauri lake mahakamani, jambo
linalopelekea wananchi kukimbilia kwa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wakiamini
haki inaweza kupatikana kwa viongozi hao.
Mhe
Kamala alieleza kuwa mawazo kama hayo hayapaswi kupewa nafasi kwa kuzingatia
maendeleo makubwa ambayo yamefanywa na Mahakama katika kuweka mazingira mazuri
ya utoaji haki kwa wananchi, hivyo akashauri utoaji wa elimu ya kutosha utakuwa
ndiyo njia muafaka ili watanzania waelewe mambo mazuri yanayoendelea kufanyika mahakamani.
Halikadhalika,
washiriki katika mafunzo hayo waliona sheria inayowapa Wakuu wa Wilaya na Wakuu
wa Mikoa mamlaka ya kuendelea kuwa wenyeviti wa kamati za maadili kwa Mahakimu kuwa ina mapungufu
kwa vile inaweza kuathiri uhuru wa Mahakama.
Kwa
upande wake, Mhe. Msoffe, ambaye aliwasilisha mada juu ya Maadili ya Watumishi
wa Umma na Maadili ya Kimahakama alichukua muda mrefu kuwaeleza washiriki wa
mafunzo hayo namna ambavyo wanapaswa kuwa na tabia njema na kuwa mfano kwa
watumishi wengine walio chini yao na wananchi kwa ujumla.
Aliwakumbusha
kuwa wakati wanatekeleza majukumu yao hawana budi kufanya kazi kwa bidii,
kujizuia kuwa na tamaa, kujiheshimu, kufanya kazi bila upendeleo, kuepuka
kupokea vijizawadi, kutoa na kupokea rushwa, kuepuka kutumia madaraka
waliyonayo vibaya na kutotumia mali ya umma kwa maslahi binafsi.
Jaji huyo
mstaafu pia aliwakumbusha Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama kuhusu
matumizi sahihi ya taarifa za umma, kuongoza kwa kuzingatia Katiba, Sheria,
Kanuni, taratibu na mazoea na kujiepusha kufanya mambo ya upendeleo na ubaguzi
na kutotoa siri za serikali au taarifa muhimu kwa watu ambao hawahusiki.
Baadaye jioni, mwezeshaji mwingine, Bw. Malimo Manyambula, ambaye ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Kumbukumbu wa Mahakama ya Tanzania aliwashirikisha Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama hao kwenye suala zima la utunzaji wa kumbukumbu mbalimbali mahakamani.
Jaji Mkuu mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman akifafanua jambo wakati anatoa mada juu ya Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama (the Judiciary Administration Act) ya mwaka 2011 wakati wa mafunzo elekezi yanayotolewa kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambayo yameendelea leo tarehe 30 Novemba, 2021.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni