Jumatano, 1 Desemba 2021

NAIBU WASAJILI NA WATENDAJI WA MAHAKAMA WAENDELEA KUPIGWA MSASA LUSHOTO

Na Faustine Kapama na Lydia Churi, Mahakama

Mafunzo elekezi yanayotolewa kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) leo tarehe 1 Decemba, 2021 yameingia siku ya tatu ambapo Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Cyprian Mkeha na Mhe. Katarina Revocati walikuwa miongoni mwa wawezeshaji waliowapiga msasa viongozi hao. 

Viongozi wengine waliowawezesha washiriki wa mafunzo hayo ni Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kelvin Mhina, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt na Mtendaji wa Mahakama Kuu, Bw. Leonard Magacha. Hata hivyo, washiriki hao waligawanywa katika makundi mawili tofauti kutokana na aina ya mada zilizowasilishwa. 

Mhe. Revocati alikuwa wa kwanza kuwapiga msasa viongozi hao kwa kuwapitisha juu ya mada inayohusu muundo wa Mahakama ya Tanzania na historia yake kwa ujumla ambapo alielezea kwa kina faida mbalimbali zilizopatikana baada ya kuanzishwa kwa muundo mpya ambao ulijumlisha, pamoja na mambo mengine, kutenganisha majukumu ya utendaji kuhusu masuala ya kiutawala na usimamizi wa mashauri kwa ujumla. 

Muundo huo mpya ambao ulichagizwa na Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama (the Judiciary Administration Act) ya mwaka 2011 ndio ulioanzisha ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Msajili Mkuu wa Mahakama, ofisi ya Msajili na Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, ofisi ya Msajili na Mtendaji wa Mahakama Kuu, pamoja na kurugenzi na idara mbalimbali za Mahakama. Kabla ya muundo mpya wa Mahakama, Msajili wa Mahakama ya Rufani ndiye aliyekuwa mtendaji mkuu wa shughuli zote za Mahakama akisaidiwa na Msajili wa Mahakama Kuu na Wasajili wengine katika masjala mbalimbali. 

Jaji huyo amezitaja baadhi ya faida zilizopatikana ikiwemo kuongezeka kwa ufanisi mahakamani, kupunguza mlundikano wa mashauri katika ngazi ya Mahakama Kuu kutoka 6,104 kwa 2012 hadi 1,779 kwa mwaka 2020, kuongezeka kwa idadi ya mashauri yanayomalizika kwa mwaka kutoka 5,600 mashauri kwa mwaka 2012 had 14,719 kwa mwaka 2020 na kupungua kwa muda wa wastani wa kumaliza mashauri kutoka siku 515 kwa mwaka 2012 hadi siku 390 kwa mwaka 2020. 

Mhe. Revocati alibainisha pia kuwa kumekuwepo na uondoshaji wa zaidi ya mashauri 856 yenye umri wa zaidi ya miaka 10, kupunguza mashauri 1,534 yenye umri wa kati ya miaka mitano na kumi hadi kufikia chini ya mashauri kumi tu, ongozeko la uondoshaji wa mashauri kwa kila Jaji kutoka 118 kwa mwaka 2012 hadi 227 kwa mwaka 2020 na kumarika kwa utendaji wa shughulizingine za kiutawala mahakamani kwa ujumla wake. 

Hata hivyo, Jaji huyo wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliwashauri viongozi hao kuendelea kufanya kazi kwa pamoja kwa vile bila kuwepo kwa uratibu, mashauriano na ushirikiano hawawezi kufanikiwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu katika kutoa haki kwa wananchi.

Kwa upande wao, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kelvin Mhina na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt aliwapitisha Naibu Wasajili kwenye eneo la kazi, mamlaka na wajibu wa Naibu Msajili, huku Mtendaji wa Mahakama Kuu, Bw. Leonard Magacha akiwajuza watendaji wa Mahakama kuhusu majukumu, mamlaka na wajibu wa Mtendaji wa Mahakama.

Naye Mhe. Mkeha, aliyewasislisha mada yake kipindi cha jioni aliwapitisha Naibu Wasajili hao kwenye suala zima la utekelezaji wa majukumu ya kimahakama, hususani usimamizi wa mashauri kuanzia hatua ya kwanza shauri linapowasilshwa mahakamani na baadaye kupangwa kusikilizwa na kutolea uamuzi na Jaji au Hakimu anayehusika.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati akionyesha kitu alipokuwa akiwasilisha leo tarehe 1 Desemba, 2021 mada juu ya muundo wa Mahakama ya Tanzania wakati wa mafunzo elekezi yanayotolewa kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kelvin Mhina akifafanua jambo wakati anawasilisha mada juu ya mamlaka na wajibu wa Naibu Msajili katika mafunzo hayo.


Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt akisisitiza jambo mbele ya Naibu Wasajili wanaoshiriki kwenye mafunzo hayo.

Naibu Wasajili wanaoshiriki kwenye mafunzo hayo wakimsikiliza kwa makini Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt wakati anawasilisha mada yake juu ya mamlaka na wajibu wa Naibu Msajili ndani ya Mahakama ya Tanzania.

Naibu Wasajili wanaoshiriki kwenye mafunzo hayo (juu na chini) wakifuatilia uwasilishaji wa mada uliokuwa unafanywa na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt (hayupo kwenye picha).



Naibu Wasajili (juu na chini) wakifurahia jambo wakati wa mafunzo.


Mtendaji wa Mahakama Kuu, Bw. Leonard Magacha akisisitiza jambo alipokuwa anawasilisha mada kuhusu majukumu, mamlaka na wajibu wa Mtendaji wa Mahakama kwa Watendaji wa Mahakama wanaoshiriki mafunzo hayo.

Watendaji wa Mahakama wanaoshiriki mafunzo wakifurahia jambo.

Watendaji wa Mahakama wanaoshiriki mafunzo (juu na chini) wakisoma moja ya nyaraka waliyopewa na Mtendaji wa Mahakama Kuu, Bw. Leonard Magacha (hayupo kwenye picha) wakati anawasilisha mada yake. 



Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara, Mhe, Cyprian Mkeha aliwasilisha mada juu ya Usimamizi wa Masjala mbele ya Naibu Wasajili wanaoshiriki mafunzo hayo.


Naibu Wasajili (picha ya juu na chini) wakimpashia kwa furaha (ishara ya kumpongeza) Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara, Mhe, Cyprian Mkeha mara baada ya kuwasilisha mada yake. 


Mhe. Kinabo Minja, ambaye ni miongoni mwa Naibu Wasajili wanaoshiriki mafunzo akisisitiza jambo alipokuwa akiwasilisha mada juu ya Ukaguzi wa Mahakama na Magereza.

Naibu Wasajili wakifuatilia uwasilishaji wa mada uliokuwa unafamnywa na Mhe. Minja


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni