Alhamisi, 2 Desemba 2021

MHASIBU MKUU WA MAHAKAMA YA TANZANIA AFAFANUA CHANGAMOTO YA MALIPO YA FAINI KWA WASHITAKIWA

 Na Faustine Kapama, Mahakama-Lushoto 

Mhasibu Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw Fanuael Tiibuza amefafanua kwa kina changamoto ambayo huwa inajitokeza kwa washitakiwa wanaoshinda rufaa kuchelewa kurudishiwa faini wanazotozwa na Mahakama katika ngazi mbalimbali baada ya kutiwa hatiani kwenye makosa ya jinai. 

Bw. Tiibuza ametoa ufafanuzi huo leo tarehe 2 Desemba, 2021 alipokuwa akijibu baadhi ya hoja zilizowasilishwa na Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama wanaoshiriki kwenye mafunzo elekezi yanayotolewa kwa viongozi hao katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) baada ya kuwasilisha mada juu ya usimamizi wa fedha za umma na manunuzi katika siku ya nne ya mafunzo hayo.

Amebainisha kuwa kiasi kinachotolewa mara baada ya mtuhumiwa anapotiwa hatiani na kuhukumiwa kulipa faini hupelekwa Hazina na hivyo kuwa kama pato la serikali lisilotokana na kodi. 

“Wewe umepelekwa mahakamani, umetozwa faini. Si umeshindwa? Kwa hiyo, ukishatozwa faini hayo yanakuwa mapato ya serikali. Sisi tunapotoa taarifa ya mwisho wa mwaka, maduhuri yanayopatikana tunajumlisha na hizo faini na fedha hizi tunapokusanya kila mwezi tuzipeleka Hazina,” alisema. 

Hata hivyo, Bw. Tiibuza alisema kuwa changamoto hujitokeza pale mwananchi ambaye hakuridhika na hukumu iliyotolewa dhidi yake ambapo huaenda kukata rufaa na baadaye kushinda kwenye rufaa yake, wakati huo huo watendaji wengine wanakuwa hawajui kama kuna rufaa ilikatwa. 

“Sasa wewe kama uneshinda una haki ya kuidai serikali na serikali ina utaratibu wake wa kulipa ambapo lazima kuwepo na bajeti. Mfano, wewe umeleta madai yako leo, lakini sisi kwenye bajeti yetu hatukujua kama kuna mtu anatudai, kwa mazingira hayo huwezi kulipwa. Deni lako litachukuliwa na litawekwa kwenye bajeti ya mwaka ujao, halafu utalipwa,” alisema.

Kutokana na mazingira hayo, Bw. Tiibuza aliwaomba watendaji kuwafafanulia wananchi hatua ambazo wanapaswa kuzifuata kwani Hazina huwa wanalipa, lakini sio kitu ambacho mtu anaweza akakiomba na kupata siku hiyo hiyo.” Sisi huwa tunakusanya maombi ya aina hiyo kutoka kwenye mikoa na tunapeleka hazina ambao hulipa madeni hayo wakishaweka kwenye bajeti,” alieleza Mhasibu Mkuu huyo. 

Wakati akiwasilisha mada yake, Bw. Tiibuza aliwapitisha washiriki kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo mfumo wa MUSE ambao ndio unaotumika kufanya malipo yote ya taasisi na kwamba mfumo huo ulianza kutumika Julai, 2019. Alieleza pia kuwa mfumo wa manunuzi ya umma kwa njia ya mtandao (TANePS) ulianza kutumika Januari  2020 kupitia Waraka Na.4 wa mwaka 2019.

Hata hivyo, alibainisha baadhi ya maeneo yenye hoja za mara kwa mara kama manunuzi yanayofanyika kutoka kwa Wazabuni wasioidhinishwa, kinyume na Kanuni ya Mannuzi ya Umma Na. 131 (5) na 164(1), malipo yasiyoambatana na risiti za kielektoniki (EFD), kinyume na Kanuni Na. 24 ya EFD ya mwaka 2021 na malipo yasiyo na viambatanisho vya kutosha, kinyume na Kanuni Na. 95 (4) ya Kanuni ya Fedha za Umma ya mwaka 2001. 

Eneo lingine alilozungumzia lenye changamoto ni manunuzi kufanyika nje ya mpango wa manunuzi ya mwaka, jambo ambalo ni kinyume cha Kanuni Na. 49 (2)(3) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwala 2011, kufanya mapokezi ya vifaa bila kufanya ukaguzi, kinyume cha Kanuni Na 244 (1) ya Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2013. 

Bw. Tiibuza alimalizia kwa kushauri kuwa kila afisa aliyekasimiwa madaraka ya kuidhinisha matumizi ya fedha za umma ni muhimu kukumbuka kuwa fedha zinazotolewa ni za serikali, hivyo haziwezi kuwa fedha za ubani unaotolewa kwenye  msiba bila kuuliza zimetumikaje na kwamba watendaji wamekasimiwa madaraka yenye masharti ambayo wanawajibika kuyazingatia. 

Katika siku hiyo ya nne ya mafunzo, wawezeshaji wengine waliotoa mada ni Mkurugenzi Msaidizi  katika Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri, Mhe. Moses Ndelwa, ambaye pia ni mshiriki katika mafunzo hayo, aliyewashirikisha Naibu Wasajili mada juu ya nafasi ya Wasajili katika kusimamia mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa mashauri. 

Mwezeshaji mwingine alikuwa Bw. Allan Machella, ambaye, kwa upande wake, aliwapitisha Watendaji wa Mahakama wanaoshiriki katika mafunzo hayo kwenye mada inayohusu barabara kuelekea haki mtandao na mahakama mtandao na hali ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Mahakama ya Tanzania.

Mhasibu Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw Fanuael Tiibuza akifafanua jambo wakati alipokuwa akiwasilisha mada leo tarehe 2 Desemba, 2021 juu ya usimamizi wa fedha za umma na manunuzi kwenye mafunzo elekezi yanayotolewa kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).



Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama(picha mbili juu na mbili chini) wakifuatilia mada iliyokuwa inawasilishwa na Mhasibu Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw Fanuael Tiibuza (hayupo kwenye picha).



Mkurugenzi Msaidizi  katika Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri, Mhe. Moses Ndelwa, akiwasilisha mada juu ya nafasi ya Wasajili katika kusimamia mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa mashauri katika mafunzo hayo. 



Sehemu ya washiriki katika mafunzo (picha mbili juu na tatu chini) wakifuatilia mada inayowasilishwa na Mhe. Ndelwa. 









Mwezeshaji Allan Machella akiwapitisha Watendaji wa Mahakama (waliopo kwenye picha chini) wanaoshiriki katika mafunzo hayo kwenye mada inayohusu barabara kuelekea haki mtandao na mahakama mtandao na hali ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Mahakama ya Tanzania.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni