Alhamisi, 2 Desemba 2021

UONGOZI NI MZIGO: MKUU WA CHUO IJA AWAAMBIA NAIBU WASAJILI

 Na Faustine Kapama, Mahakama-Lushoto

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt Paul Kihwelo, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani amewataka Naibu Wasajili kuwatumikia Watanzania kwa moyo wao wote na kujiona kuwa ni watumishi wa watu na sio viongozi wanaopenda kutumikiwa.

Mhe Dkt Kihwelo ametoa wito huo leo alipokuwa akiozungumza na viongozi hao katikati ya mafunzo elekezi yanayotolewa na IJA kuwajengea uwezo kwenye maeneno mbalimbali ya kiutendaji ndani ya Mahakama ya Tanzania.

“Kwanza nawapongeza, nafasi mlizoaminiwa ni kubwa na najua utaratibu mliopitia, mnastahili. Kikubwa ambacho napenda kuwaambia msiwaangushe. Bahati nzuri mmeingia kipindi kizuri sana na inawezekana kuna wenzenu mliowaacha ambao walibadilika au hawakubadilika. (Hata hivyo) nawashauri (muelewe kuwa) uongozi ni mzigo,” alisema.

Akifafanua zaidi, Mhe. Kihwelo alisema huwa anawaambia watu kuwa angependa awe jaji wa kawaida na jalada lake kwa sababu mtu akiwa kwenye uongozi anakuwa tofauti. “Ukiwa kiongozi unabeba mzigo mzito na mkilibeba hilo litawaongoza sana kuliko kuona uongozi kama ni nafasi,”aliwaambia viongozi hao.

Mkuu huyo wa chuo alibainisha kuwa viongozi wa sasa wanaona zaidi kama wawakilishi wa watu kuliko kuona watu wanawatumikia. “Mimi nawashauri mkienda na hilo litawasaidia sana, na bahati nzuri Mahakama ya sasa imebadilika sana. Furahia uteuzi asilimia 25 lakini beba ule mzigo kwa asilimia 75,” alisema.

Mhe. Dkt Kihwelo aliwakumbusha viongozi hao pia kuwa bado wana safari ndefu na kwamba wasipate kitu na kukifanya ndiyo mwisho wa maisha, labda iwe mwenyezi Mungu kapanga na sio wao kujiharibia.

“Nafasi mnazozipata ziwasaidie muwe watu wa maadili, kwani suala la uadilifu ni jambo la msingi. Wasajili na watendaji ndiyo moyo wa Mahakama. Mimi naamini mkifanyakazi mnaibeba Mahakama yote. Msikubali kutumiwa,” alisema.

Mhe. Dkt Kihwelo pia alitumia nafasi hiyo kuwaomba viongozi hao kuwapa ushirikiano wa kutosha Majaji wanapotekeleza majukumu mbalimbali ya utoaji haki kwa wananchi. Alibainisha kuwa Majaji wanafanya kazi kubwa,  wamebadilika na huwezi kuwasikia wanalalamika na ukiona wamebeba mabegi ndani yake asilimia kubwa ni majalada ya mashauri.

Aliwakumbusha pia kuwa maisha siyo fedha peke yake, hivyo aliwaomba watumishi wa Mahakama kulibeba suala hilo kwa sababu fedha inawapoteza watu wengi. “Ukipenda fedha sana mwisho wako huwa sio mzuri sana. Na watu huwa wanaharibikiwa kwa hilo. Acha hela ikufuate nyuma,” alisema.

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt Paul Kihwelo, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani akitoa ufafanuzi wa jambo fulani alipokuwa akiongea na Naibu Wasajili wanaoshiriki mafunzo elekezi katika chuo hicho leo tarehe 2 Desemba, 2021.

Sehemu ya Naibu Wasajili (juu na chini) wanaoshiriki mafunzo elekezi wakimsikiliza Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt Paul Kihwelo (hayupo kwenye picha) alipokuwa akiongea nao leo tarehe 2 Desemba, 2021.
Sehemu nyingine ya Naibu Wasajili (picha mbili chini) wanaoshiriki mafunzo elekezi wakimsikiliza Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt Paul Kihwelo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni