Na Faustine Kapama, Mahakama-Lushoto
Mafunzo elekezi yaliyokuwa yanayotolewa kwa
Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto (IJA) yamekamilika leo tarehe 2 Decemba, 2021 huku viongozi hao
wakihimizwa kuzingatia yote waliyoshirikishwa, ikiwemo kudumisha ushirikiano,
umoja, upendo na kuboresha huduma za utoaji haki kwa wananchi.
Akizungungumza wakati anafunga mafunzo hayo,
ambayo ni ya kwanza kuwashirikisha Naibu Wasajili na Watendaji wa
Mahakama, Mkuu wa Chuo hicho, Mhe, Dkt Paul Kihwelo, ambaye pia ni Jaji wa
Mahakama ya Rufani alibainisha kuwa heshima, upendo pamoja na ushirikiano
sehemu za kazi ikawe ndio dira yao katika kutekeleza majukumu mbalimbali za
kimahakama.
“Waha wanamsemo kuwa samaki anaoza kuanzia
kichwani. Ninyi ni kichwa cha Mahakama, hivyo msikubali kuoza kwani mtawaharibu
walio chini yenu. Ni tegemeo la kila mmoja wetu kuwa nyinyi ndio mtakuwa kioo
cha tabia njema na sio kinyume chake. Nawaasa kwa mara nyingine mkawe
wasimamizi wazuri wa maadili na nidhamu katika maeneo yenu ya kazi,” alisema.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa chuo, moja ya sifa
kubwa iliyopo mahakamani ni upendo, udugu na mshikamano, hivyo hakuna shaka
kuwa viongozi hao watapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa watangulizi wao
pamoja na wale watakaowakuta vituoni. “Naamini ninyi pia mtatoa ushirikiano na
niwaase pia kuwa msisite kuwafundisha mambo mapya ambayo hawayajui lakini pia
muendelee kuwa wanafunzi wazuri kwani Wahaya wanamsemo usemao Experience
is a Good Teacher,” alisesma.
Aliwakumbusha washiriki wa mafunzo hayo kuwa wakati
wa ufunguzi walihusiwa mengi na viongozi mbalimbali, akiwemo Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, aliwaeleza kuwa Mahakama na
umma wa watanzania kwa ujumla una matarajio na imani kubwa kwao na kwamba watapimwa
kupitia nguzo tatu za Mpango Mkakati wa Mahakama. Hivyo anaamini kuwa baada ya
mafunzo hayo imani waliyonayo wananchi, wadau na Mahakama kwao itazidi kuongezeka
kutokana na kuimarika kwa utendaji wao wa kazi.
Mhe. Dkt Kihwelo aliwaambia kuwa Mtendaji Mkuu
wa Mahakama ya Tanzania, Prof Elisante Ole Gabriel pia wakati wa ufunguzi
aliwakumbusha kuwa hawakupata nafasi hizo kama zawadi bali kupitia tanuru. “Nirudie
kwa kusema hamkupata nafasi hizi kwa bahati bali mnastahiri kutokana na sifa zanu,
ikiwemo utendaji kazi uliotukuka na sina shana kuwa mtatumikia nafasi hizi kwa
bidii na uadilifu huku mkiheshimu mamlaka,
madaraka na majukumu mliyonayo na yale ya wale mnaofanya nao kazi,” alisema.
Aidha, Mkuu huyo wa Chuo aliwakumbusha pia
viongozi hao kuwa kwa upande wake wakati akiwawezesha mada Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe.
Mohamed Chande Othman aliwaeleza juu ya umuhimu wa kufanya kazi kwa
kushirikiana ili kuifanya Mahakama iweze kustawi zaidi.
“Katika hilo aliwasisitiza juu ya C tatu ambazo
ni consultation,
coordination na cooperation. Ni matumaini yangu kuwa baada ya kuwasikiliza
nyote mtazingatia ushirikiano kwa kuwa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.
Kwa vile sote tunajenga nyumba moja basi hatuna sababu ya kugombea fito,”
alisema.
Wakitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki
kwa nyakati tofauti, Naibu Msajili Mwandamizi, Mahakama ya Rufani, Mhe.
Happiness Ndesambiro na Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Tanga, Bw. Tutubi
Mangazeni waliushukuru uongozi wa Mahakama ya Tanzania pamoja na IJA kwa ujumla
kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo ni ya kwanza kuwashirikisha Naibu Wasajili na
Watendaji. Waliahidi kutekeleza yote waliyojifunza kwa siku zote tano ili
kuboresha huduma za utoaji haki kwa wananchi kwa kuwa mada zilizowasilishwa
zimekuwa na manufaa makubwa sana kwao.
Mapema kabla ya kufika kileleni cha mafunzo
hayo, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. John Kahyoza, ambaye ni Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma na Mhe. Cyprian Mkeha, ambaye ni Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara, walikuwa miongoni mwa
wawezeshaji waliowasilisha mada mbalimbali kwa washiriki.
Mhe. Kahyoza alijikita katika kutoa maelezo ya
kina kuhusu mamlaka ya ziada ya kwa Mahakimu katika kusikiliza mashauri ya
Mahakama Kuu, ambapo Mhe. Mkeha aliwapitisha Naibu Wasajili hao kwenye eneo
linalohusu namna ya kushughulikia maombi ya gharama za malipo baada ya
kuendesha mashauri ya madai.
Wawezeshaji wengine waliotoa mada zao ni Bi.
Sadaka Gandi, ambaye ni Mwanasaikolojia Mshauri Nasaha na Namna ya Kuishi,
alitoa mada juu ya ustawi wetu, maisha yetu katika usawa mbele ya washiriki
wote, huku mwezeshaji mwingine, Bw. Bwai Biseko kutoka Wakala wa Maji Vijijini,
akiwasilisha mada juu ya kuendesha mashauri ya kinidhamu mbele ya Watendaji wa
Mahakama.
Kabla ya kuhitimisha mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo,
Mhe, Dkt Kihwelo aliwakabidhi vyeti na zawadi mbalimbali Naibu Wasajili na
Watendaji wa Mahakama wote kama ishara ya kushiriki na kuonesha nidhamu ya hali
ya juu wakati wote wa mafunzo hayo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. John Kahyoza akiwasilisha mada juu ya mamlaka ya ziada kwa Mahakimu kusikiliza mashauri ya Mahakama Kuu leo tarehe 3 Desemba, 2021 katika siku ya tano na ya mwisho ya mafunzo yaliyokuwa yanayotolewa kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni