Na Rosena Suka - Lushoto
Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto (IJA) kinaendesha mafunzo kwa wawezeshaji 36 kutoka sehemu
mbalimbali nchini Tanzania ili kuwajengea uelewa na ujuzi wa pamoja juu ya
uendeshaji bora wa mashauri ya mtoto.
Mafunzo hayo yanayofanyika kwa siku tano katika ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma yameanza leo tarehe 15 Novemba, 2021 ambapo washiriki ni Majaji kutoka Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Mahakama Kuu ya Tanzania, Mahakimu Wakazi wa ngazi mbalimbali, Waendesha Mashtaka na Maafisa Ustawi wa Jamii.
Mahakama ya Tanzania imeandaa mafunzo kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto chini ya ufadhili wa Shirika linalohudumia Watoto
Duniani (UNICEF). Wakati wa mafunzo, washiriki watapitishwa katika mada
mbalimbali zitakazowasilishwa na wawezeshaji mahiri na wabobezi ili kuwawezesha
kuwa na uelewa na ujuzi mpana juu ya haki za watoto na namna bora ya
kushughulikia mashauri yao.
Miongoni mwa
wawezeshaji hao mahiri na wabobezi ni Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Mhe. Sophia Wambura na Wakili wa Kujitegemea Mstaafu, Mhe. Matilda Philip.
Akitoa neno la ukaribisho, Mkuu wa Chuo hicho, Mhe. Dkt Paul Kihwelo, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania alisema kuwa wameamua kuandaa
mafunzo hayo kwa kundi hilo ili kuwaandaa waweze kupata ujuzi wa kutosha kuhusu
masuala ya watoto, jambo litakalowawezesha nma wao kuwafundisha wengine ambao
hawakupata nafasi hiyo.
Kwa upande wake,
Mwakilishi kutoka UNICEF, Bi. Victoria Mgonela ameushukuru uongozi wa Mahakama
na Chuo kwa kulipa uzito wa kipekee suala la uendeshaji wa mashauri ya watoto
na kuahidi kuwa shirika lake litaendeleza ushirikiano uliopo.
Mafunzo kama hayo
yalishawahi kuendeshwa mwaka 2014 ambayo yalijumuisha majaji sita (6), Mahakimu
Wakazi sita (6), maafisa ustawi wa jamii wawili (2) na watumishi watatu (3)
kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
1 Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto,
Mhe. Dkt Paul Kihwelo, ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania akitoa neno la ukaribisho kwenye mafunzo yanayojumuisha Majaji, Mahakimu na wawezeshaji wengine leo tarehe 15
Novemba, 2021 jijini Dodoma.
1.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo wakimsikiliza
mwezeshaji katika mafunzo hayo, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Sophia Wambura (hayupo katika picha).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni