Jumatatu, 15 Novemba 2021

MAHAKIMU MKOANI MOROGORO WAKUTANA KUJINOA

 Na Evelina Odemba - Morogoro

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro imeanza kutoa mafunzo maalum kwa Mahakimu wote Mkoani hapa ikiwa ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa kuboresha huduma za kimahakama na kuweka mifumo bora ya kuwahudumia wananchi.

Mafunzo hayo yaliyofunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu wa Kanda hiyo, Mhe. Paul Ngwembe yamehudhuliwa na Mahakimu zaidi ya 60 wa Mkoa huo ambapo wawezeshaji waliwapitisha katika mada mbalimbali zikiwemo makosa yanayojirudia kwenye uendeshaji wa mashauri pamoja na maadili kwa maafisa wote wa Mahakama.

Makosa ya kimtandao na ushahidi wa kielektroniki ni miongoni mwa maada zingine zilizojadiliwa. Wakati wa mafunzo hayo,  Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, Mhe. Said Kalunde alitoa ufafanuzi wa kina kuhusu mada hizo pamoja na mada inayohusu ukaguzi wa Mahakama na usimamizi wa Masijala, hatua ambayo itawaongezea Mahakimu ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.

Pamoja na mafunzo hayo, washiriki pia walijadili mikakati mbalimbali itakayowaongoza katika kufanikisha kutoa haki kwa wananchi ambapo moja ya mikakati hiyo ikiwa ni suala la elimu kwa wananchi kwani kumekuwepo na makosa ya kujirudia rudia yanayochangiwa na wananchi kutokuwa na elimu sahihi ya sheria.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mhe. Ngwembe alibainisha kuwa Mahakama ya Tanzania, hususani katika Kanda yake imejipanga kutekeleza majukumu ya utoaji haki kwa kasi na kimkakati, ikiwemo kumaliza mashauri yote ya mrundikano ifikapo March 2022.

Sanjari na hayo, Mhe. Ngwembe alitilia mkazo suala la Matumizi ya TEHAMA na kusema kuwa matumizi ya Mkutano Mtandao (Video Conference) yataendelea kutumika kwa nguvu nyingi na ili kuthibitisha hilo tayari wameshafanya mazungumzo na wakuu wa Magereza mkoani Morogoro ili kufunga runinga kwenye Magereza yao zitakazounganishwa kuwezesha hukumu kutolewa kupitia njia hiyo.

Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mvomelo, Mhe. Asha Waziri aliwawakilisha Mahakimu kutoa neno la shukurani kwa uongozi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro kwa kuona umuhimu wa kuwepo kwa mafunzo hayo kwani yatawasaidia katika suala zima la kutoa huduma kwa jamii.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe (waliokaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Mahakimu wanaoshiriki katika mafunzo maalum mkoani hapo. Waliokaa kutoka kwa Jaji Ngwembe ni Mhe. Jaji Said Kalunde (kushoto) na Mhe. Jaji John Chaba (kulia). Mwanzo kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, Bw. Selemani Ng'eni na kulia mwisho ni Msajili wa Mahakama Kuu wa Kanda hiyo, Mhe. Arnold Kinekiano. 


Chini ni makundi mengine ya Mahakamu wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe (waliokaa katikati) na wajumbe wengine wa meza kuu.




 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni