Na Faustine Kapama - Mahakama
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania anayeshughulikia Mahakama za Mwanzo, Bw. Humfrey Paya amewaasa Madalali kote nchini kufanya kazi
zao kwa kuzingatia haki na sheria, hasa wanapotekeleza hukumu za Mahakama zinazohusu
makundi ya watu wenye mahitaji maalumu ambao ni watoto, walemavu, wanawake na
wazee.
Bw. Paya alitoa wito
huo Ijumaa tarehe 12 Novemba, 2021 alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Chama
cha Madalali kwa niaba ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Mustafa Siyani, kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Alibainisha kuwa kuna
utafiti ambao ulifanywa na ndugu marafiki wahisani hasa Benki ya Dunia kuhusu
vikwazo mbalimbali juu ya jukumu nyeti la Mahakama ya Tanzania kuhusu utoaji
haki sawa kwa wote na kwa wakati, hususani kwenye makundi ya watu wenye
mahitaji maalumu.
“Utafiti huo ulibaini
kuwa hili ni kundi linaloathirika sana na kutotimizwa kwa wakati au kutokutekelezwa
kabisa kwa amri halali za Mahakama kulikosababishwa na udhaifu katika usimamizi
wa Madalali wakati huo. Mapendekezo ya utafiti huo yalipekea afua mbalimbali
zilizochukuliwa na Mahakama ili kurekebisha hali hii na umuhimu mkubwa uliwekwa
kwenu Madalali katika mchakato mzima wa utoaji haki,” alisema.
Kwa mujibu wa Mtendaji
huyo, Madalali wa Mahakama ni wadau muhimu sana katika utekelezaji wa jukumu la
Mhimili huo ambao ni utoaji wa haki kwa wananchi. Alibainisha pia kuwa Madalali
waliosajiliwa ni maafisa wa Mahakama ambao wamepewa jukumu la kutekeleza amri
halali za Mahakama.
“Kuthibitisha umuhimu
huo, katika Mpango Mkakati wa Mahakama ulioanza 2015/206 hadi 20/21, Mahakama
ya Tanzania iliingiza mchakato wa uboreshaji
wa huduma za kundi hili muhimu katika katika mradi wa uboreshaji wa Mahakama
kupitia mradi wa huduma zinazomlenga mwananchi” alisema.
Bw. Paya alieleza kuwa
mchakato huo ulilenga, pamoja na mambo mengine, kuimarisha kitengo kinachosimamia
Mawakili na Madalali katika ofisi ya Msajili wa Mahakama Kuu ili kusimamia na
kuratibu shughuli za madalali, lakini pia kuandaa kanuni kuhusu uteuzi,
gharama, malipo na nidhamu za Madalali na Wasambaza nyaraka ambapo mchakato huo
ulikamilika 2017 baada ya kupata kanuni zilizotolewa na Jaji Mkuu wa Tanzania.
Alibainisha hatua
zingine zilizochukuliwa ni kusimamia mchakato wa uanzishaji wa Umoja wa Madalali
na Wasambaza nyaraka, kuendesha usaili na mafunzo kwa Madalali na kuhakikisha
idadi ya Madalali inaongezeka nchi nzima hadi kufikia 100. “Mpaka tunapomaliza
Mpango Mkakati wa Miaka Mitano tulikuwa na Madalali 81, hivyo nasikitika kusema
tumeshindwa kufikia lengo hilo,” Bw. Paya aliwaambia wajumbe wa Mkutano huo.
Hatua nyingine
iliyochukuliwa, kwa mujibu wa Mtendaji huyo wa Mahakama, ilikuwa kuanzisha
mfumo wa kielektroniki wa utambuzi na usimamizi wa Madalali, mpango ambao bado
haujawa rasmi, lakini unatarajiwa kukamilika baada ya Chama cha Madalali kupata
uongozi.
“Ni dhahili kuwa hadi
kufikia tukio la leo majukumu ya Mahakama ya Tanzania kupitia ofisi ya Msajili
wa Mahakama Kuu yametekelezwa zaidi ya asilimia 90 na kazi iliyobaki ni yenu
kupitia umoja wenu ambao utaanza kazi
rasmi baada ya kupatikana uongozi kupitia uchaguzi wa leo,” alisema.
Katika Mkutano Mkuu huo
kulifanyika uchaguzi wa uongozi wa Chama cha Madalali ambapo Bi. Mwamvua Kigulu
alichaguliwa kuwa Mwenyekiti, huku Bw. Boniface Buberwa akishika nafasi ya
Makamu Mwenyekiti. Viongozi wengine ni Bw. Hilary Ligate aliyechaguliwa kuwa
Katibu, Bi. Jesca Masawe kuwa Katibu Msaidizi na Bw. Benson Swai alishika
nafasi ya Mweka Hazina na Bw. Mark Msilu kuwa Mweka Hazina Msaidizi.
Mtendaji huyo wa
Mahakama alitumia nafasi hiyo kuwaasa viongozi hao wapya kulinda kwa nguvu zao
zote umoja wa chama hicho, waelewe katiba na kanuni zilizopo na kuwa mfano wa
kuigwa katika masuala mazima ya maadili ya kazi na kukemea vitendo vya utovu wa
nidhamu, rushwa na uzembe wa wanachama katika utekelezaji wa majukumu yao kwa
ujumla.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania anayeshughulikia Mahakama za Mwanzo, Bw. Humfrey Paya akisisitiza jambo alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Madalali uliofanyika jijini Dar es Salaam Ijumaa tarehe 12 Novemba, 2021.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Madalali wakifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka kwa Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania anayeshughulikia Mahakama za Mwanzo, Bw. Humfrey Paya (hayupo kwenye picha)
Mwenyekiti wa Chama cha Madalali, Bi. Mwamvua Kigalu akiwahutubia wajumbe wa Mkutano Mkuu (hawapo katika picha)
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania anayeshughulikia Mahakama za Mwanzo, Bw. Humfrey Paya akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Chama cha Madalali na wajumbe wa sekretarieti katika Kitengo cha Madalali Mahakama Kuu ya Tanzania baada ya kufungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Madalali Ijumaa tarehe 12 Novemba, 2021 jijini Dar es Salaam. Waliokaa kushoto ni Mwenyekiti wa Chama cha Madalali, Bi. Mwamvua Kigalu na kushoto ni Makamu Mwenyekiti Bw. Boniface Buberwa.
Kundi jingine la wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Madalali wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi (aliyekaa katikati) pamoja na viongozi wa Chama cha Madalali baada ya kufungua mkutano huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni