Lydia Churi- Mahakama, Lushoto
Waziri wa Katiba
na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi ametaja mafanikio makubwa sita ambayo
Tanzania imeyapata katika kipindi cha miaka 60 tangu uhuru wake Desemba 9, 1961.
Akizungumza katika mahafali ya 21 ya chuo cha Uongozi
wa Mahakama Lushoto ambapo alikuwa mgeni rasmi, Prof. Kabudi amesema Tanzania
inaadhimisha miaka 60 ya uhuru ikiwa ni taifa imara na siyo mkusanyiko wa
makabila yasiyokuwa na umoja.
Alisema kuwa ndani ya miaka 60 ya uhuru Tanzania
imeingia katika uchumi wa kati. Alifafanua kuwa wakati wa uhuru, Tanganyika
ilikuwa nchi maskini kuliko zote Afrika ya Mashariki na Kati, lakini leo ni
nchi ya pili kwenye ukanda huo kuingia uchumi wa kati miaka mitano kabla ya
wakati uliokuwa umetarajiwa, tena pamoja na kuwepo kwa ugonjwa wa UVIKO 19
uliosababisha uchumi kuporomoka kwenye mataifa mengi duniani.
“Tunasherehekea miaka 60 ya uhuru tukiwa ni taifa lililojikita
katika kuenzi na kudumisha tunu za taifa ambazo ni amani, umoja, mshikamano,
utu, haki, heshima, uhuru na demokrasia”, alisema Prof. Kabudi.
Alisema mafanikio mengine makubwa ambayo nchi imeyapata
katika kipindi cha miaka 60 ni kuwa taifa lenye udhubutu na moyo wa kujitegemea
katika kufanya mambo makubwa kwa rasilimali zake yenyewe. Alisema, hivi sasa Tanzania inatekeleza
miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere
litakalozalisha umeme wa Megawatt 2,115 pamoja na kujenga reli ya kisasa ya
umeme ambayo kwa mujibu wa wataalamu itachukua miaka 150 kabla ya kufanyiwa ukarabati mkubwa. Miradi yote hii
na mingine inatekelezwa kwa fedha za ndani.
Waziri wa Katiba na Sheria alisema, Tanzania
inasherehekea miaka 60 ya uhuru ikiwa imetangaza kwamba mali asili zote na
rasilimali zote ni mali ya watanzania. Alisema hatua hii imewezesha kurejewa
upya kwa mikataba na kampuni kubwa zikiwemo za madini ili wananchi wafaidike na
mali zao. “Nathubutu kusema kuwa katika nchi za Afrika sisi ni wa kwanza
kufanya hivyo”, alisisitiza.
Prof. Kabudi alisema Tanzania imeidhihirishia Dunia
ukomavu wa kisiasa na umadhubuti wake katika ukatiba (Constitutionalism).
Alisema nchi ilionesha ukomavu mkubwa wa kiasiasa na utaratibu wake wa kisiasa
na kikatiba katika kipindi cha mpito kwa amani na utulivu baada ya kifo cha
Rais wa awamu ya tano Hayati John Pombe Magufuli, na kwa mujibu wa katiba,
Makamu wa Rais aliapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akiwaasa wahitimu 575 wa fani ya Sheria, Prof. Kabudi
amewataka kufanya kazi kwa bidii ili kuendeleza mazuri yaliyoanzishwa. “Mkiwa
ni vijana wa taifa hili, kazi yenu ni kuyaendeleza hayo yote”, alisisitiza.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akianzisha rasmi Mahafali ya 21 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto jana Lushoto, Tanga.
Sehemu ya Wahitimu wa Stashahada ya Sheria wakiwa wamesimama kutunukiwa Stashahada zao katika Mahafali ya 21 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto jana Lushoto, Tanga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni