Ijumaa, 12 Novemba 2021

UJUZI MLIOPATA UWE CHACHU KUJIENDELEZA: PROF. KABUDI

 Na Lydia Churi-Mahakama, Lushoto

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi ametoa wito kwa wahitimu wa chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kutumia ujuzi walioupata   kama chachu ya kujiendeleza katika ngazi za juu zaidi kitaaluma ili waweze kukabiliana na ulimwengu wa sasa unaohitaji ujuzi na maarifa ya kutosha.

Akizungumza katika sherehe za Mahafali ya 21 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto leo tarehe 12 Novemba 2021 ambapo alikuwa mgeni rasmi, Prof. Kabudi aliwapongeza wahitimu wote kwa kumaliza masomo yao kwa mafanikio na kuwaasa kujiendeleza zaidi kitaaluma kwa kuwa taifa linawategemea kulijenga.

“Ongezeni maarifa zaidi na muwe na moyo wa kizalendo ili mlifikishe taifa hili sehemu ambayo sote tunaitamani”, alisema Waziri Kabudi.

Prof. Kabudi aliwataka wahitimu wa chuo hicho ambao ni watumishi wa Umma kwenda kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, bidii, haki, uadilifu, kutanguliza mbele maslahi ya Taifa na kuendelea kuwa taswira nzuri ya Serikali na nchi kwa ujumla. Aidha, aliwataka watumishi wa Mahakama ya Tanzania kutumia vema maarifa na ujuzi waliopata kwa manufaa ya Umma

Aliwasihi wazazi wa wahitimu hao kuendelea kuwajengea uwezo wa kielimu vijana  wao ili wakawe watoa haki wanaotekeleza majukumu yao kwa kufuata misingi ya taaluma zao, taratibu, tamaduni, desturi na maadili mema.

Waziri huyo wa Katiba na Sheria alisema Serikali kupitia wizara yake itaendelea kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama katika kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwa lengo la kuhakikisha chuo hicho kinatimiza malengo yaliyokusudiwa.

Alisema Chuo hicho kimeiwezesha Serikali kupata watumishi wenye misingi bora ya utoaji haki. Aliongeza kuwa Mahakama ya Tanzania imekuwa ndiyo mnufaika mkubwa wa chuo cha uongozi wa Mahakama kwa kuwezesha uwepo wa watumishi wenye misingi imara ya taaluma na uongozi wa kimahakama.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo hicho, Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Gerald Ndika amewashauri wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kujiendeleza zaidi ili kukabiliana na changamoto za utandawazi katika soko la ajira zinazohitaji mbinu mpya ili kukabiliana nazo.

Naye Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Paul Kihwelo amewaasa wahitimu wa chuo hicho kutumia ngazi waliyofikia kitaaluma kama chachu ya kujiendeleza zaidi.

Dkt. Kihwelo alizitaja baadhi ya changamoto zinazokikabili chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kuwa ni upungufu wa watumishi wakiwemo Waalimu, hostel na vyumba vichache vya mihadhara pamoja na vitendea kazi. Alisema licha ya changamoto hizo, chuo kinatumia mbinu mbalimbali katika kukabiliana nazo.

Jumla ya wanafunzi 575 wamehitimu masomo yao katika chuo hicho katika fani ya Sheria ambapo kati yao, wahitimu 216 ni wa Stashahada na wengine 359 ni wa Astashahada.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akisisitiza jambo wakati alipokuwa akitoa hutuba kwenye Mahafali ya 21 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto leo wilayani Lushoto, Tanga. Waziri Kabudi alikuwa Mgeni rasmi kwenye Mahafali hayo.
Wahitimu wakitunukiwa Astashahada ya Sheria katika Mahafali ya 21 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto leo wilayani Lushoto, Tanga. Waziri Kabudi alikuwa Mgeni rasmi kwenye Mahafali hayo.
Wahitimu wakitunukiwa Stashahada ya Sheria katika Mahafali ya 21 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto leo wilayani Lushoto, Tanga. Waziri Kabudi alikuwa Mgeni rasmi kwenye Mahafali hayo.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Gerald Ndika akizungumza wakati wa sherehe hizo.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akizungumza wakati wa sherehe hizo.
Mmoja wa Wahitimu wa Stashahada ya Sheria ambaye ni mshindi wa masomo kadhaa akipokea zawadi ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliyotoa kwa washindi wote katika masomo.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akiongoza Maandamano kabla ya kuanza kwa sherehe za Mahafali ya 21 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto leo wilayani Lushoto, Tanga. Waziri Kabudi alikuwa Mgeni rasmi kwenye Mahafali hayo. Kulia ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho, Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Gerald Ndika. Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho. 
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wanachama wa chama cha wanafunzi waliowahi kusoma katika chuo hicho. 
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya wahitimu wa Astashahada ya Sheria. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni