Na Rosena Suka - Lushoto
Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ameahidi kushirikiana na Chuo
cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ili kiweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu,
ikiwemo kutoa wahitimu bora watakaolisaidia taifa katika maeneo mbalimbali ya
maendeleo.
Prof. Ole Gabriel,
ambaye ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama alitoa ahadi hiyo katika ziara
ya Tume iliyofanya katika Chuo hicho hivi karibuni kutembelea maeneo
mbalimbali, likiwemo Jengo la Hostel ya Wavulana ambalo linajengwa kwa kugharamiwa
na Mahakama ya Tanzania katika mpango wa uboreshaji wa majengo chuoni hapo.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa Baraza la Uongozi la Chuo, Mhe. Dkt. Gerald Ndika, ambaye ni Jaji wa
Mahakama ya Rufani aliupongeza uongozi wa Chuo kwa jitihada zake inazozifanya
katika kutoa mafunzo yanayolenga kuwajengea uwezo watumishi mbalimbali wa
Mahakama ya Tanzania.
Katika ziara hiyo,
ambayo ni mwendelezo wa shughuli mbalimbali zinazofanyika kuelekea siku ya
mahafali ya ishirini na moja ambayo inafanyika tarehe 12 Novemba, 2021, Prof.
Ole Gabriel ameambatana na Makamishna mbalimbali wa Tume ya Utumishi wa
Mahakama.
Wajumbe wa Tume hiyo pia
walipata nafasi ya kukutana na
menejimenti ya Chuo ambapo walifanya majadiliano yaliyolenga kuboresha
huduma zinazotolewa na chuo hicho.
Katika kikao hicho, Katibu wa Tume hiyo ambaye ni Mtendaji Mkuu wa
Mahakama alitoa salamu kwa niaba ya wajumbe wa Tume hiyo.
Prof. Elisante
aliiambia Menejimenti kwamba Chuo kina
wajibu mkubwa kwa Mahakama ya Tanzania na Taifa kwa ujumla katika kutoa elimu
ambayo italeta matokeo chanya kwa taifa sio tu kwa kufaulu katika mitihani
mbalimbali bali kutoa wanafunzi waliobora ambao wanaweza kufanya kazi popote na
katika mazingira yoyote.
1. Jaji
wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt.
Paul Faustine Kihwelo akifungua majadiliano ya wajumbe wa Tume ya Utumishi ya
Mahakama na Menejimenti ya Chuo yaliyofanyika Chuoni Lushoto hivi karibuni.
Baadhi ya wajumbe wa Tume ya Utumishi ya Mahakama wakipatiwa maelezo ya kitabu cha mwongozo wa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kutoka kwa msimamizi wa kitengo cha Maktaba cha Chuo, Bw. Faridi Sechonge (aliyesimama katikati).
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa maelekezo kwa mafundi wanaojenga jengo la hostel ya wavulana wakati wa ziara ya Makamishina wa Tume ya Utumishi ya Mahakama katika Chuo cha Mahakama Lushoto hivi karibuni.
Wajumbe
wa Tume ya Utumishi ya Mahakama wakiwa katika picha ya pamoja na wanachuo wa
Stashashada ya Sheria mwaka wa pili walipotembelea hivi karibuni katika Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni