Alhamisi, 11 Novemba 2021

JAJI MUGETA AHIMIZA WELEDI NA HUDUMA BORA KWA WAKATI KWENYE VITUO JUMUISHI

 Na Faustine Kapama – Mahakama

Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke, Mhe. Ilvin Mugeta amewataka watumishi wa Mahakama ya Tanzania waliopangiwa kuhudumu katika Kituo hicho kufanya kazi kwa weledi na kutoa huduma bora kwa wakati kwa wananchi ili kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha huduma za kimahakama zinazotolewa kote nchini.

Mhe. Mugeta alitoa wito huo hivi karibuni alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tano ya watumishi wa Mahakama na wadau mbalimbali yanayofanyika katika Kituo hicho Jumuishi ili kupata maarifa yatakayowasaidia kutoa huduma bora kwa kiwango cha juu na kumfanya mwananchi kufurahia huduma hizo.

“Haitakuwa na maana yoyote kufanya kazi  katika majengo mazuri namna hii ya kisasa halafu huduma zetu zikawa zinalalamikiwa na wateja wetu na wananchi kwa ujumla. Sote tunapaswa kuiunga mkono serikali yetu na Mahakama kwa ujumla kwa uboreshaji unaoendelea kote chini kwa kufanya kazi kwa weledi na ufanisi mkubwa kuhakikisha lengo la kutoa huduma kwa wakati linatimia kwa ubora wa hali ya juu,” alisema.

Mhe. Mugeta aliwakumbusha washiriki hao wa mafunzo kuwa wao ni miongoni mwa watumishi wachache ambao wamepitia katika mchakato mrefu wa kuwapata kwa kuangalia vigezo maalumu ambavyo Mahakama imeonesha matumaini kwao kuwa watatoa huduma bora katika Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki.

“Tambueni kwamba Vituo hivi Jumuishi vinapaswa kufanya kazi kwa weledi, huduma bora na kwa wakati. Hivyo, ili kutimiza malengo haya, tunategemea watumishi wote mliopangiwa kwenye Kituo Jumuishi Temeke kuwa waadilifu na wawajibikaji katika kazi, kujituma na kutoa huduma iliyotukuka kwa wateja kwa upendo na tabasamu kila wakati,” aliwaambia washiriki hao wa mafunzo.

Mahakama ya Tanzania imekamilisha awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2014/2015-2020/2021) chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia, mpango ambao matunda yake ni uboreshaji mkubwa wa miundombinu ya Mahakama, masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), mafunzo mbalimbali ya muda mfupi na mrefu, na mangineyo.

Katika Mpango huo wa Mahakama, moja ya malengo makuu ni kupeleka huduma karibu na wananchi. Kwa msingi huo, vimejengwa Vituo Jumuishi sita vya Utoaji Haki vya Dodoma, Arusha, Mwanza, Morogoro na Dar es Salaam (Temeke na Kinondoni) kwa lengo la kutoa huduma za kimahakama katika ngazi zote katika jengo moja.

Mhe, Mugeta alibainisha kuwa Kituo Jumuishi cha Temeke ni maalumu kwa ajili ya kusikiliza mashauri ya mirathi na ndoa pekee kwa mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama Ustawi wa Jamii, Polisi, Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Baraza la Maaskofu, Baraza la Ndoa, Wanasheria wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea na Dawti la Jinsia.

Hivyo, Jaji Mfawidhi huyo alielezea matumaini ya Jaji Mkuu na Mahakama ya Tanzania kwa ujumla kuwa Kituo hicho kitasaidia mashauri yanayofunguliwa kusikilizwa kwa haraka, kwa wakati na weledi mkubwa kwa vile uwepo wa wadau wengine wanaotarajiwa kufanya kazi kwa pamoja na watumishi wa Mahakama utasaidia kupunguza gharama kwa wateja.

Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke,  Mhe. Ilvin Mugeta akifafanua jambo mara baada ya kufungua mafunzo kwa watumishi wa Mahakama na wadau mbalimbali yaliyoanza hivi karibuni katika kituo hicho kuwajengea ujuzi katika maeneo mbalimbali ya utoaji haki kwa wananchi.

Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi Temeke, Mhe Ilvin Mugeta (wa mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu mbalimbali wanaoshiriki katika mafunzo hayo. Kushoto kwake ni Bw. Allan Mwela na kulia kwake ni Bi. Mary Moyo.

Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi Temeke, Mhe Ilvin Mugeta (wa mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na maafisa mbalimbali wanaohudumu katika Kituo hicho.

Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi Temeke, Mhe Ilvin Mugeta (wa mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wanaohudumu katika Kituo hicho.

Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi Temeke, Mhe Ilvin Mugeta (wa mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi kutoka Kituo Jumuishi Kinondoni wanaoshiriki mafunzo hayo.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni