Jumatatu, 22 Novemba 2021

JAJI MKUU ANZINDUA VITABU VYA MKUSANYIKO WA MASHAURI YA KAZI

 Na Faustine Kapama, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 22 Novemba, 2021 amezindua Vitabu vya Mkusanyiko wa Maamuzi ya Mashauri ya Kazi (Labour Court Case Digest) ambapo amehimiza kasi ya usikilizaji wa mashauri na utatuzi wa migogoro ya kazi inayoletwa mahakamani ili kusaidia kuchochea ukuaji wa uchumi hapa nchini.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Vitabu hivyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Jaji Mkuu alisema kuwa hakuna ubishi kwamba maendeleo ya mtu mmoja mmoja na kukua kwa uchumi wa nchi kwa ujumla kunategemea upatikanaji wa haki ambayo huchagizwa na umalizaji wa haraka wa migogoro inayowasilishwa Mahakamani.

Alibainisha kuwa sekta ya kazi ni moja ya sekta muhimu katika ukuaji wa uchumu, hivyo kwa upekee, umalizaji wa haraka wa mashauri ya kazi yaliyopo katika ngazi mbali mbali za vyombo vya utatuzi wa migogoro ya kazi na utoaji haki ni moja ya nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi.

“Ndio maana mnamo mwaka 2018, tulifanya Ugatuzi wa Mamlaka na kuwapa mamlaka Majaji waliopo katika Kanda za Mahakama Kuu kuweza pia kusikiliza mashauri ya kazi. Hii imesaidia umalizikaji wa haraka wa mashauri ya kazi sehemu zote ambazo kuna Kanda ya Mahakama Kuu,” Jaji Mkuu alisema.

Mhe. Prof. Juma amesema pia kuwa ili migogoro ya kazi iweze kutatuliwa kwa haraka na kwa wakati, ni sharti Mahakama itoe tafsiri ya sheria za kazi kupitia maamuzi mbalimbali ili kumuwezesha mtatuzi wa migogoro kufanya maamuzi ya haki na kwa wakati.

 “Vitabu hivi vitawezesha Mahakama na vyombo vingine vya kutoa haki katika sekta ya kazi pamoja na wadau wake kufanya urahisi wa rejea wakati wa usikilizaji na utoaji maamuzi wa mashauri ya kazi. Si hivyo tu lakini pia vitabu hivi vitasaidia Waajiri na Wafanyakazi kujua zaidi mambo muhimu yaliyomo kwenye sheria za kazi kwa kuwa sheria hizo zimetafsiriwa katika vitabu hivi,” alisema.

Jaji Mkuu amesema kuwa Mkusanyiko wa vitabu hivyo utatasaidia kupunguza migogoro katika sehemu za kaz na kuchochea kuongeza ufanisi katika utendaji kazi kwa kila mmoja kujua haki na wajibu alionao itakayopelekea kukua kwa uchumi.

“Kwetu sisi Mahakama na vyombo vya Usuluhishi na Uamuzi, vitabu hivi vitasaidia kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri na hivyo itawezesha wananchi kupunguza muda watakaotumia katika kudai haki kwenye vyombo hivi na badala yake kutumia muda mwingi katika uzalishaji mali,” alisema.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi alisema kuwa kwa mujibu wa kanuni ya 3(1)(a) ya Kanuni za Mahakama  ya kazi, Mahakama hiyo inajukumu la kuweka kumbukumbu za maamuzi inayokuwa imeyatoa katika kutekeleza mamlaka yake, hivyo utekelezaji wa jukumu hilo ndilo chimbuko la kuwa na vitabu hivyo vya ripoti ya maamuzi ya Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi. 

Akifafanua zaidi, Mhe. Maghimbi alisema kuwa “Labour Court Case Digest” ni vitabu vinanyokusanya maamuzi mbalimbali yanayohusiana na ajira na mahusiano kazini, yaliyoamuliwa na Majaji wa Divisheni ya kazi na mashauri hayo hukusanywa kwa umahiri ili kujumuisha maamuzi yanayogusa masuala tofauti na yenye kutoa tafasiri na misimamo ya Sheria za kazi, Kanuni zilizopo pamoja na Mikataba ya Kimataifa inayohusiana na masuala ya kazi.

“Ukusanyaji huu hufanywa na watalaamu waliobobea katika Sheria na uwezo wa kufanya uchambuzi wa mashauri, kuyakusanya na kuyaripoti kwa namna ambayo itamnufaisha mlengwa,” alisema. Aidha, alibainisha hhumuni la uzinduzi wa vitabu hivyo ni kuongeza wigo wa ufahamu kwa wadau wote wa sekta ya kazi pamoja  na jamii kwa ujumla, juu ya uwepo wa vitabu hivyo ambayo ni miongozo ya sheria katika kushughulikia na kutatua masuala mbalimbali katika sekta ya kazi ikiwemo migogoro inayotokana na mahusiano kazini.

Hafla ya uzinduzi wa Mkusanyiko wa Vitabu hivyo inayojumuisha maamuzi ya Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi kwa mwaka 2016, 2017 na 2018 imehudhuriwa na maafisa mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania, akiwemo Kaimu Jaji Kiongozi, Mhe. John Mgetta na Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke, maalumu kwa mashauri yanayohudu ndoa na talaka, Mhe. Ilvin Mugeta.

Wageni wengine walikuwa Mkuu wa Shule ya Sheria, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Benhajj Masoud, Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Kazi (ILO-Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi), Bw. Wellington Chibebe, Majaji mbalimbali wa Mahakama Kuu ya Tanzania na wadau mbalimbali wa Mahakama.

Uzinduzi wa Vitabu hivyo unaweka historia nyingine ya kutoa toleo la tatu la ‘Labour Court Case Digest’ ikijumuisha maamuzi muhimu ya Divisheni ya kazi kwa miaka ya 2016, 2017 na 2018 kwa kukusanya na kuyaweka pamoja katika vitabu vya sheria vyenye maamuzi mbalimbali yenye kutafasiri na kuweka misimamo ya kisheria kwenye sekta nzima ya kazi.

Hii ni mara ya tatu machapisho kama hayo yameweza kutolewa na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO). Chapisho la kwanza lilihusisha “Labour Court Case Digest” za mwaka 2011 na 2012. Chapisho la pili lilikuwa la mwaka 2013, 2014 na 2015.

Kutokana na hatua hiyo, Jaji Mkuu aliishukuru ILO kwa kuendelea kutoa ufadhili kwa Mahakama ya Tanzania kuwezesha na kufanikisha matoleo yote hayo matatu ya Labour Court Case Digest. Amesema kuwa ILO wamekuwa wadau wakubwa wa utoaji haki katika mashauri ya kazi na wamekuwa wanasaidia Divisheni ya Kazi katika mambo mbalimbali ikiwemo mafunzo kwa Majaji.

Kabla ya uzinduzi huo, Jaji Mkuu alipokea neno fupi kutoka kwa wawakilishi mbalimbali, akiwemo Bw. Willington Chibebe (ILO), Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende, Bw. Frank Mwalongo kutoka Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Bi Suzzane Ndomba kutoka Chama cha Waajili (ATE), Bw.  Noel Nchimbi kutoka Chama cha Wafanyakazi (TUCTA) na Bw. Sammy Katerega ambaye anatoka Wawakilishi binafsi.

Kwa ujumla wao, wawakilishi hao waliiipongeza Mahakama ya Tanzania, kupitia Divisheni ya Kazi kwa kazi nzuri inayofanya ya kutatua migogoro mbambali ya wananchi, lakini wakaomba utafutwe utaratibu utakaowezesha majaji wanaohudumu katika mahakama hiyo kukaa muda mrefu ili kuwa na uelewa mpana wa sheria za kazi na pia maamuzi yanayotolewa yawe kwa lugha ya Kiswahili.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akizindua Vitabu vya Mkusanyiko wa Maamuzi ya Mashauri ya Kazi leo tarehe 22 Novemba, 2021 jijini Dar es Salaam. Kushoto kwa Jaji Mkuu ni Kaimu Jaji Kiongozi, Mhe. John Mgetta na Mkuu wa Shule ya Sheria, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Benhajj Masoud na kulia kwake ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Kazi (ILO-Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi), Bw. Wellington Chibebe.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akionesha moja ya Vitabu vya Mkusanyiko wa Maamuzi ya Mashauri ya Kazi alivyovizindua leo tarehe 22 Novemba, 2021 jijini Dar es Salaam.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Vitabu vya Mkusanyiko wa Maamuzi ya Mashauri ya Kazi leo tarehe 22 Novemba, 2021 jijini Dar es Salaam. 


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi akitoa hotuba katika hafla ya uzinduzi wa vitabu hivyo.




Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akifuatilia jambo katika hafla ya uzinduzi wa Vitabu vya Mkusanyiko wa Maamuzi ya Mashauri ya Kazi leo tarehe 22 Novemba, 2021 jijini Dar es Salaam. Kushoto kwa Jaji Mkuu ni Kaimu Jaji Kiongozi, Mhe. John Mgetta na Mkuu wa Shule ya Sheria, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Benhajj Masoud na kulia kwake ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Kazi (ILO-Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi), Bw. Wellington Chibebe.

Baadhi ya Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakifuatilia hafla ya uzinduzi wa vitabu hivyo. kutoka kulia ni Jaji Biswalo Mganga, Jaji Augustine Rwizile na Jaji Isaya Arufani na wa mwisho kushoto ni Jaji Mstaafu, Mhe, Sophia Wambura.


Baadhi ya wawakilishi wa sekta mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa vitabu hivyo wakifuatilia mambo kadhaa yaliyokuwa yanajili kwenye hafla hiyo.

Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Kazi (ILO-Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi), Bw. Wellington Chibebe akitoa neno fupi katika hafla ya uzinduzi wa vitabu hivyo.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi mara baada ya kuzindua Vitabu vya Mkusanyiko wa Maamuzi ya Mashauri ya Kazi leo tarehe 22 Novemba, 2021 jijini Dar es Salaam. Waliokaa kushoto kwa Jaji Mkuu ni Kaimu Jaji Kiongozi, Mhe. John Mgetta na Mkuu wa Shule ya Sheria, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Benhajj Masoud na kulia kwake ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Kazi (ILO-Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi), Bw. Wellington Chibebe.

Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe Prof. Ibrahim Hamis Juma (waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na watendaji mbalimbali (waliosimama).

Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe Prof. Ibrahim Hamis Juma (waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu (waliosimama).

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akimkabidhi 
Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Kazi (ILO-Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi), Bw. Wellington Chibebe zawadi kwa ushirikiano ambao shirika hilo limetoa ili kufanikisha upatikanaji wa vitabu hivyo. Wanaoshuhudia tukio hilo kutoka kushoto kwa Jaji Mkuu ni Kaimu Jaji Kiongozi, Mhe. John Mgetta na Mkuu wa Shule ya Sheria, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Benhajj Masoud.

Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende (kulia) akipokea sehemu ya vitabu hivyo kutoka kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma. 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni