Jumanne, 23 Novemba 2021

TOENI HUDUMA BORA KWA WANANCHI: JAJI MZUNA

Na Faustine Kapama, Mahakama 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna amewataka watumishi wanaohudumu katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kuzingatia weledi na kutoa huduma bora kwa wananchi ili kutimiza dira ya Mahakama juu ya utoaji wa haki kwa wakati.

Mhe. Mzuna alitoa wito huo tarehe 22 Novemba, 2021 alipokuwa akifungua mafunzo kwa watumishi wa Mahakama na wadau wanaofanya kazi katika Kituo hicho, nafasi ambayo itawafanya washiriki wote kupata maarifa yakayowasaidia kutoa huduma zilizo bora kwa kiwango cha juu ili kumfanya mwananchi aweze kufurahia huduma za kimahakama.

“Haitakuwa na maana yoyote kufanyia kazi katika majengo mazuri namna hii na ya kisasa halafu huduma zetu zikawa zinalalamikiwa na wateja wetu na wananchi kwa ujumla. Sote tunapaswa kuiunga mkono Serikali na Mahakama kwa ujumla kwa uboreshaji unaofanyika kote nchini kwa kufanya kazi kwa weledi na ufanisi mkubwa kuhakikisha tunatimiza lengo la kutoa huduma kwa wakati linatimia kwa ubora wa hali ya juu,” alisema.

Jaji Mfawidhi huyo aliwakumbusha washiriki wa mafunzo kuwa wao ni miongoni mwa watumishi wachache ambao wamepitia katika mchakato mrefu wa kuwapata kwa kuangalia vigezo maalumu ambavyo Mahakama inatarajia na kuwa na matumaini ya kutoa huduma katika Vituo hivyo Jumuishi.

“Tambueni kwamba Vituo hivi Jumuishi zinapaswa kufanya kazi kwa weledi,  huduma bora na kwa wakati. Hivyo ili kutimiza malengo haya, tunategemea watumishi wote mliopangwa kwenye Kituo Jumuishi Arusha kuwa waadilifu na wawajibikaji katika kazi, kujituma na kutoa huduma iliyotukuka kwa wateja kwa upendo na tabasamu bashasha kila wakati,” alisema.

Mhe. Mzuna aliwaeleza washiriki kuwa safari ya Mahakama ya Tanzania ni kufikia Mahakama Mtandao  katika ngazi zake zote za utoaji haki na shughuli zote za kimahakama, hivyo mafunzo kama hayo ni muhimu katika kuwajengea watumishi na wadau uwezo na uelewa zaidi.

Alielezea matarajio ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Mahakama, wadau na wateja wengine kuwa Kituo Jumuishi hicho kitasaidia usikilizwaji wa mashauri yanayofunguliwa kukamilika kwa haraka, kwa wakati, lakini pia kwa weledi mkubwa na kwa gharama nafuu.

Jaji Mafawidhi huyo alibainisha kuwa uwepo wa wadau wengine wanaotarajiwa kufanya kazi katika Kituo wakiwemo Mawakili wa Kujitegemea, Wanasheria wa Serikali, Magereza, Ustawi wa Jamii, Polisi, Dawati la Jinsia na Watoa huduma za kisheria (Legal Aid Providers) utawasaidia wateja ambao wanapofika kufata huduma  kupunguza gharama.

Mafunzo hayo yatahitimishwa tarehe 26 Novemba, 2021 ambapo jumla ya washiriki ni 132 wakiwemo watumishi pamoja na wadau wa Mahakama.Wadau walinaohudhuria mafunzpo hayo ni Magereza, Ustawi wa Jamii, Mawakili wa Kujitegemea, Polisi jamii na wengineo.

Mahakama ya Tanzania imekamilisha awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2015/2016-2020/2021) chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia, mpango ambao matunda yake ni uboreshaji mkubwa ya miundombinu ya Mahakama, masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, mafunzo mbalimbali ya muda mfupi na mrefu na mengineyo mengi.

Katika mpango mkakati wa Mahakama ya Tanzania, moja ya malengo makuu ni kupeleka huduma karibu kwa wananchi. Kwa msingi huo vimejengwa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki sita Arusha, Dar es Salaam (Temeke na Kinondoni), Dodoma, Morogoro na Mwanza ambapo malengo yake ni kutoa huduma za Kimahakama katika ngazi zote katika jengo moja.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna akisisitiza jambo wakati akifungua mafunzo kwa watumishi wa Mahakama na wadau wanaofanya kazi katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Arusha tarehe 22 Novemba, 2021.


Baadhi ya wawezeshaji wanaotoa mafunzo kwa watumishi wa Mahakama na wadau wanaofanya kazi katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Arusha.

Sehemu ya watumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Arusha wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna (hayupo kwenye picha) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni