Jumanne, 23 Novemba 2021

TUMIENI FEDHA VIZURI ZIWATUNZE: JAJI MLACHA

 Na Festo Sanga, Mahakama-Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Jaji Lameck Mlacha amefungua mafunzo ya watumishi 15 wa kada mbalimbali wa Mahakama Kanda ya Kigoma wanaokaribia kustaafu katika kipindi cha kuanzia mwaka 2022 hadi mwaka 2024 huku akitoa rai kwa Watumishi hao kutumia vizuri fedha za mafao watakazopata ili ziweze kuwasaidia pia katika Maisha yao baada ya kustaafu.

Akifungua mafunzo hayo tarehe 19 Novemba, 2021, Mhe.  Jaji Mlacha alisema lengo ni kuwawezesha  wastaafu watarajiwa kujiandaa na Maisha baada ya kustaafu. 

“Baada ya kuona changamoto za wastaafu na kutambua kuwa kila mtumishi ni mstaafu mtarajiwa, tuliona ni vyema kuandaa mafunzo haya kwa lengo la kuwawezesha watumishi wenzetu kujua dhana nzima ya kustaafu, maandalizi muhimu kabla ya kustaafu na kujipanga kwa maisha baada ya kustaafu” Alisema Jaji Mlacha.

Aliongeza kuwa zipo simulizi za kweli kuhusu baadhi ya wastaafu kutokuwa na ufahamu mzuri wa matumizi sahihi ya fedha wanazozipata baada ya kustaafu kiasi cha kusababisha baadhi yao kujiingiza katika miradi isiyo na manufaa lakini pia kujiingiza katika kazi hatarishi au kazi zinazoondoa heshima ya utumishi wao wa muda mrefu.

Aidha aliwaasa watumishi ambao ni wastaafu watarajiwa kuhakikisha wanatumia vizuri fedha watakazozipata baada ya kustaafu kwa kutojiingiza katika miradi na mambo yasiyo sahihi ili fedha hizo ziweze kuwatunza na kuwafaa.

Naye Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Kigoma Bw. Moses Mashaka alisema kuwa kufanyika kwa mafunzo hayo ni utekelezaji wa sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 na Mpango wa mafunzo ya Ndani wa Kanda ya Kigoma ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya watumishi 87 watanufaiki na Mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo katika maeneo mbalimbali.

Aliongeza kuwa Mafunzo hayo ya wastaafu ni mafunzo ya awamu ya pili baada ya kufanya mafunzo awamu ya kwanza Oktoba 5-6, 2021 kwa kuwashirikisha washiriki 50 ambao walipata mafunzo kuhusu mifumo ya TEHAMA katika kazi za Mahakama huku mkazo ukiwekwa katika Mahakama za Mwanzo, Usimamizi wa mashauri ya Mirathi na Mpango Mkakati wa Mahakama.

Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki aliwaomba wastaafu watarajiwa kutumia hekima na kuwataka watumishi vijana katika meneo yao kuzingatia maadili na miiko ya kazi zao ili kujiepusha na vitendo vya utovu wa nidhamu.

Mafunzo hayo ya siku mbili yaliwezeshwa na Wakufunzi kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF), Benki ya NMB na Mahakama ambapo washiriki walipewa mafunzo kuhusu hitimisho la kazi (maana, haki, wajibu na changamoto), Taratibu za malipo ya mafao na viambata vyake, Matumizi sahihi ya fedha baada ya kustaafu (Ujasiriamali), namna ya Kujitunza na kuzikabili changamoto za kisaikolojia, kijamii na kiuchumi baada ya kustaafu na Mpango mkakati na Maadili.

Akitoa neno la Shukrani kwa niaba ya washiriki, Bi Rhoda Kigwambaye Kijumbe alipongeza Uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kwa kutoa mafunzo ya wastaafu watarajiwa na kusema kuwa mafunzo hayo watayatumia kama fursa muhimu na kumuomba Mungu awawezeshe kuyaishi yote waliyojifunza katika safari ya kuelekea kustaafu.

“Mafunzo haya ni fursa kwetu na zaidi tumefahamiana na miongoni mwetu wapo watumishi ambao hawakuwahi kufika Kigoma tangu wanaajiriwa hivyo tumefurahi sana na tunakwenda kuanza mabadiliko ya kifikra na Matendo katika safari ya kuelekea kustaafu” alisema Bi Kijumbe.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Kigoma, Mhe. Jaji Lameck Mlacha akitoa nasaha kwa wastaafu watarajiwa (hawapo katika picha) katika mafunzo yaliyofanyika mnamo Novemba 19, 2021 katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma.

Washiriki wa Mafunzo ambao ni wastaafu watarajiwa wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kigoma, Mhe Jaji Lameck Mlacha (aliyeketi katikati) pamoja na Wawezeshaji wa Mafunzo. Walioketi, wa pili kushoto ni Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki, wa kwanza kushoto ni Mwezeshaji kutoka Benki ya NMB, Bi. Pilly Gordon Mvunyi, wa kwanza kulia ni Afisa Utumishi wa Mahakama Kuu Kigoma Bw. Festor Sanga na wapili kulia ni Meneja wa Mkoa wa Mfuko wa hifadhi  ya Jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF), Bw. Thomas Labi.

Muwezeshaji Kutoka Benki ya NMB bi Pilly Gordon Mvunyi akiwasilisha mada kuhusu matumizi sahihi ya fedha baada ya kustaafu na elimu ya ujasiriamali kwa washiriki wa Mafunzo(Hawapo Pichani) katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma Novemba 19, 2021.

Afisa Mkaguzi wa Ndani Bw. Christsian Constatine Mrema akiwasilisha mada kwa wastaafu  watarajiwa waliohudhuria mafunzo Novemba 20, 2021 katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma.

Washiriki wa Mafunzo wakifuatilia moja ya mada zilizowasilishwa katika mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma Novemba 20,2021.

 Bi Rhoda Kigwambaye Kijumbe-Katibu Mahsusi daraja la pili akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wa Mafunzo kwa uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni