Jumanne, 23 Novemba 2021

JAJI MKUU AWAAPISHA MAHAKIMU WAKAZI WAPYA SITA

 Na Faustine Kapama, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 23 Novemba, 2021 amewaapisha Mahakimu Wakazi wapya sita  na kuwataka kutoa picha halisi ya ubora wa Mahakama kwa kuishi viapo vyao katika kutekeleza kikamilifu jukumu la utoaji haki kwa wananchi.

Akizungumza katika hafla fupi ya uapisho huo iliyofanyika ofisini kwake Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam, Mhe. Prof. Juma aliwakumbusha Mahakimu hao kuwa wameapa kwa kutumia Katiba na Kitabu Kitakatifu na kuahidi kwamba watalinda Katiba, kutetea sheria na kutoa haki bila upendeleo wa aina yoyote.

“Hivyo ahadi hii inatakiwa iwe sehemu ya maisha yenu mtakayoishi kama Mahakimu na katika shughuli nyingine yoyote mtakayoifanya. Napenda kuwakumbusha kuwa kiapo chenu kisiishie hapa. Ikiwezekana siku zote jitengenezeeni nakala iwaongoze siku zote kwa sababu inatoa muhtasari wa kile ambacho kinategemewa kutoka kwenu,” Jaji Mkuu aliwaasa Mahakimu hao.

Alibainisha pia kuwa hapa Tanzania, asilimia 70 ya wanaotafuta haki wanaipata katika Mahakama za Mwanzo, hivyo Mahakimu hao wanabeba mzigo mkubwa wa utoaji haki kwa sababu wananchi wengi kituo chao cha kwanza cha kutafuta haki ni Mahakama za Mwanzo na wengi huwa hawapati nafasi ya kuonana na Majaji.

“Kwa hiyo, picha yao ya Mahakama ni Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo. Nawaomba mtoe picha halisi ya ubora wa Mahakama. Sisi sote tutachafuka kama mkitoa picha ambayo sio halisi ya Mahakama. Nyie ndiyo picha kwa mwananchi wa kawaida na sehemu yoyote mtakayokwenda mtaishi pamoja na jamii,” alisema.

Jaji Mkuu alikumbushia jambo jingine kuhusu ukubwa wa mamlaka waliyonayo Mahakimu kwa kuangalia sheria ambazo huwa wanazitekeleza na kwamba amri yoyote wanayoweza kutoa hugusa haki za wananchi, ikiwemo haki za binadamu za kila siku, haki za mali au haki za uhuru wao binafsi, hivyo, aliwataka kutokuchelewesha maamuzi yao yanayogusa haki hizo.

“Kwa mfano, endapo utafuata sheria kwa umakini na ukatoa haki kwa umakini na wahusika wakaridhika na kutokukata rufaa, ina maana shauri husika litaisha na haki itapatikana ndani ya muda mfupi sana. Lakini kama utatoa uamuzi ambao sio makini na ikapatikana rufaa, maana yake upatikanaji wa haki utachelewa. Kwa hiyo ukiwa makini haki itapatikana kwa haraka zaidi na usipokuwa makini yule mwananchi anayetafuta haki hiyo atasubiri mpaka Mahakama ya Rufani itakapotoa uamuzi wake,” Mhe. Prof. Juma alisema.

Aidha, Jaji Mkuu aliwataka Mahakimu hao kuendelea kujisomea na kufuatilia mabadiliko ya sheria kadri yanavyotokea kwa sababu kila siku sheria inabadilika. Alitoa mfano wa Bunge lijalo ambapo kutakuwa na mabadiliko ya sheria kadhaa na baadhi ya mabadiliko hayo yatagusa utoaji haki mahakamani. “Tunatarajia mtafuatilia hayo mabadiliko na yakipishwa na Bunge lazima muende na hayo mabadiliko,” aliwaambia Mahakimu hao.

Naye Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani aliwasihi Mahakimu hao wapya kuzingatia uadilifu, juhudi na kuzingatia sheria, miongozo, taratibu na kanuni mbalimbali zinazotawala nchi yetu.  “Bahati nzuri ninyi wote mmekuwa watumishi wa Mahakama na mnafahamu yanayoendelea katika Mahakama ya Tazania hivi sasa. Hivyo ni matumaini yetu mtaenda kufanya kazi inayotakiwa. Hivyo, nendeni mkafanye kazi,” alisema.

Mahakimu hao wapya walioapishwa leo ni Mhe. Raymond Kweka aliyekuwa Msaidizi wa Kumbukumbu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mhe. John Musiime ambaye alikuwa Msaidizi wa Kumbukumbu Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, Mhe. Clifford Masinde, Msaidizi wa Kumbukumbu Mwandamizi Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Haudeface Mpanju, Msaidizi wa Kumbukumbu katika Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo, Martha Mabagala, aliyekuwa Msaidizi wa Ofisi Mahakama ya Mwanzo Kimara na Mhe. Protas Honono, aliyekuwa Msaidizi wa Hesabu  Mahakama ya Wilaya Singida.

Viongozi wengine wa Mahakama waliohudhuria hafla hiyo ya uapisho ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kelvin Mhina, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania anayeshughulikia Mahakama za Mwanzo, Bw. Humphfrey Paya na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Bahati Chitepo.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimwapisha Mhe. Martha Mabagala, aliyekuwa Msaidizi wa Kumbukumbu katika Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo kuwa Hakimu Mkazi katika hafla ya uapisho iliyofanyika leo tarehe 23 Novemba, 2021 ofisini kwake Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam. Katika hafla hiyo, jumla ya Mahakimu Wakazi sita waliapishwa.


Mhe. Raymond Kweka, aliyekuwa Msaidizi wa Kumbukumbu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu naye alipata nafasi ya kula kiapo kama Hakimu Mkazi mbele ya Jaji Mkuu (hayupo kwenye picha).


Mmoja wa Mahakimu Wakuu wapya (juu na chini) wakila kiapo cha uaminifu.


Mmoja wa Mahakimu Wakazi sita wapya akikabidhi mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kiapo cha uaminifu mara baada ya kuapishwa.


Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kevin Mhina akielezajambo katika hafla ya uapisho wa Mahakimu Wakazi sita wapya mbele ya Jaji Mkuu (hayupo kwenye picha).

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akitoa nasaha fupi kwa Mahakimu Wakazi wapya mara baada ya kuapishwa.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifafanua jambo alipokuwa akiongea na Mahakimu Wakazi sita wapya mara baada ya kuwaapisha.


Viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania wakifuatilia matukio mbalimbali katika hafla ya kuwaapisha Mahakimu Wakazi sita wapya. Kutoka kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel. Picha ya chini kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania anayeshughulikia Mahakama za Mwanzo, Bw. Humphfrey Paya na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Bahati Chitepo.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Wahe. Mahakimu Wakazi mara baada ya kuwaapisha. Picha za chini ni meza kuu ambayo inajumuisha Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kelvin Mhina ikiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu Wakazi wapya katika makundi tofauti tofauti.



(Picha na Mary Gwera, Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni