- Yawasilisha vikombe hivyo kwa shangwe
Na Mary Gwera, Mahakama
Timu ya Michezo ya Mahakama ya Tanzania ‘Mahakama Sports’ leo tarehe 08 Novemba, 2021 imekabidhi vikombe vitatu (3) kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel walivyonyakua katika Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yaliyomalizika hivi karibuni.
Akizungumza na Wanamichezo wa Timu hiyo ya Mahakama, Mtendaji Mkuu wa Mahakama alieleza kufurahishwa kwake na ushindi huo ambapo ameifikisha pia salaam za pongezi kwa wanamichezo hao kutoka kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma.
“Nikiri wazi kuwa nimefurahishwa na ushindi wenu katika mashindano ya SHIMIWI nimekuwa nikiwafuatilia kwa karibu kupitia mitandao na kuangalia ‘video clips’ mbalimbali ambazo amekuwa akinitumia mlezi wenu Bw. Uisso, vilevile Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma amenituma kuwafikishia salaam zake za pongezi kwenu,” alisema Prof. Ole Gabriel.
Aidha, Mtendaji Mkuu ameahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa timu hiyo huku akiwashauri kuanza maandalizi mapema kwa ajili ya ushiriki katika mashindano ya SHIMIWI ya mwakani 2022.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mahakama Sports, Bw. Wilson Dede alisema kuwa timu ya Mahakama imeshiriki kikamilifu mashindano ya SHIMIWI 2021 na kufanikiwa kuibuka kuwa washindi wa kwanza katika mchezo wa kuvuta kamba wanawake na wanaume na kuweka rekodi.
Akitoa neno la utangulizi, Mlezi wa Mahakama Sports, Bw. Erasmus Uisso ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji alisema kuwa miongoni mwa vitu vilivyochangia katika ushindi wa timu hiyo ni pamoja na kuwa na nidhamu na usikivu kipindi chote cha mashindayo hayo.
“Timu yetu imeshiriki kikamilifu na kwa nidhamu ya hali ya juu katika mashindano ya SHIMIWI 2021 na kufanikiwa kuweka rekodi,” alisema Bw. Uisso.
Timu ya Mahakama sports ilishiriki katika mashindano ya SHIMIWI yaliyofanyika kitaifa mkoani Morogoro kuanzia tarehe 20/10/2021 hadi tarehe 02/11/2021.
Katika mashindano hayo Mahakama Sports ilipata ushindi kupitia mchezo wa kuvuta kamba ambao wanawake walishinda michezo yote katika makundi na kuingia fainali ambapo iliivuta Ofisi ya ‘RAS’ Iringa ambayo ilikuwa bingwa mtetezi kwa muda wa miaka mitatu.
Mchezo mwingine ni Kamba kwa upande wa wanaume ambao waliingia fainali na Timu ya Uchukuzi, ambapo katika mvuto wa kwanza zilitoka sare na mvuto wa pili Mahakama iliwavuta na kuwa mabingwa kitaifa 2021.
Vilevile Mahakama Sports ilikuwa mshindi wa pili kwa mbio (riadha) wazee na kupata medali ambapo mahakama iliwakilishwa na Bw. Willson Dede ambaye ni Mwenyekiti wa Mahakama Sports.
Hali kadhalika Mahakama Sports ilipata kikombe cha nidhanu, iliyoambatana na medali ya nidhamu na cheti cha ushiriki.
Malengo ya jumla ya mashindano ya SHIMIWI ni kuboresha mahusiano baina ya watumishi wa umma kutoka wizara na idara mbalimbali, jamii inayotuzunguka kuboresha na kulinda afya za watumishi na kuimarisha nguvu kazi katika utumishi wa umma. Malengo hayo hayakinzani na malengo ya kitaasisi ya kushiriki michezo hii.
Wizara na Idara za Serikali zilizoshiriki mashindano haya zilikuwa Arobaini na Saba (4) ikiwemo Mahakama ya Tanzania. Timu ya Mahakama ilijumuisha washiriki Sabini na Tisa (79) kati yao wakiwemo makocha wawili (2) na viongozi wa michezo Taasisi yetu ilishiriki katika michezo nane (8) tu ya Mpira wa Miguu, Mpira wa Pete, Kuvuta Kamba kwa timu za wanaume na wanawake, riadha kwa wanaume na wanawake, Draft, Karata, Kurusha Tufe kwa wanaume na mchezo wa bao.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akipokea kombe la nidhamu kutoka kwa Mwenyekiti wa Mahakama Sports, Bw. Wilson Dede, pindi kiongozi huyo pamoja na wanamichezo wenzake kutoka timu ya Mahakama walipowasilisha jumla ya Vikombe vitatu (3) walivyoshinda katika mashindano wa SHIMIWI yaliyomalizika hivi karibuni.
Wakiwa katika nyuso za furaha na bashasha wakati wakipokea kombe lingine kutoka Mahakama Sports.
Wanamichezo wa Mahakama Sports wakiwa kwenye maandamano kuelekea Mahakama Kuu-Dar es Salaam kukabidhi kwa Viongozi wa Mahakama vikombe vitatu (3) walivyonyakua wakati wa Mashindano ya SHIMIWI yaliyomalizika hivi karibuni.
Sehemu ya Wanamichezo wakiwa katika ukumbi namba moja wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Dar es Salaam wakati wa kukabidhi vikombe kwa Viongozi wa Mahakama wakiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na Wanamichezo wa Timu ya Mahakama. Ameahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali kuwezesha timu hiyo kuendelea kufanya vizuri.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni