Jumatatu, 8 Novemba 2021

TWENDE KISASA: JAJI MRUMA AWAASA WATUMISHI IJC KINONDONI

 Na Faustine Kapama – Mahakama

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma amewataka watumishi wa Mahakama na wadau wengine katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kinondoni kuwa na mtazamo wa kisasa na kutoa huduma za haki kwa wananchi bila upendeleo.

 Mhe. Mruma ametoa wito huo leo tarehe 8 Novemba, 2021 alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tano ya watumishi wa Mahakama na wadau mbalimbali watakaohudumu katika Kituo hicho ili kuwajengea uwezo katika maeneo mbalimbali, ikiwemo huduma bora kwa wateja.

“Wajibu wa msingi kwa watumishi kufanya kazi katika jengo hili ni kuwa na mtazamo wa kisasa wenye thamani sawa na jengo, utendaji kazi wenye ufanisi mkubwa na uliotukuka na utoaji wa huduma bora na muonekano nadhifu kwa watoa huduma wote, ambao ni ninyi,” aliwaambia washiriki hao wa mafunzo.

Kwa mujibu wa Mhe. Mruma, uboreshaji mkubwa wa huduma za utoaji haki unaoendelea ndani ya Mahakama una malengo makuu matano hadi kufikia mwaka 2025, lengo kuu likiwa ni uwepo wa mazingira ya utulivu, amani, usalama na umoja sambamba na kujenga utawala bora.

“Hivyo, mafunzo mtakayoyapata yakawe chachu katika uboreshaji wa utendaji kazi wenu na mkawe mabalozi kwa watumishi wengine wa Mahakama ambao hawakubahatika kupata mafunzo haya,” amesema Jaji Mfawidhi huyo aliyekuwa ameongozana na Mtendaji wa Mahakama, Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Edward Mbara na Mtendaji katika Kituo hicho cha Kinondoni, Bw. Beatus Mlando.

Mhe. Mruma amesema pia kuwa ili huduma za utoaji haki ziweze kutolewa vizuri lazima kuwepo na ushirikishwaji wa wadau wote wa Mahakama, wakiwemo Polisi, Magereza, Takukuru, Ustawi wa Jamii, Mawakili wa Serikali na Mawakili wa Kujitegemea ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo na uboreshaji wa huduma za Mahakama ya Tanzania.

Aidha, Jaji Mfawidhi huyo alibainisha pia kuwa katika matumizi ya mifumo ya TEHAMA inayoendelea kuboreshwa itasaidia kupunguza gharama kubwa ya utumiaji wa vifaa vya ofisi ‘Stationaries’ ambavyo vimekuwa na bajeti kubwa ya uendeshaji wa ofisi, hivyo aliwasisitiza kuendelea kutumia mifumo hiyo iliyoandaliwa ili kuendana na uboreshaji wa huduma hizo.

Alisema kuwa katika uboreshaji wa huduma za kimahakama kila mtumishi awajibike kwa kila kitu ikiwemo usalama wa jengo, usimamizi wa mali za Umma zikiwemo Samani za ofisi, Umeme, Maji na mali nyinginezo.

Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuboresho miundombinu na huduma mbalimbali za utoaji haki, ikiwemo kukamilisha ujenzi wa Vituo Jumuishi sita vya Utoaji Haki vya Dodoma, Arusha, Mwanza, Morogoro na Dar es Salaam (Temeke na Kinondoni), ikiwa ni mwendelezo wa uboreshaji wa huduma za utoaji haki za Mahakama kwa jamii.

Katika kipindi chote cha mafunzo, wawezeshaji mbalimbali watawapitisha washiriki katika maeneo kadhaa kama mfumo wa masijala za kiutawala, maadili ya kimahakama, matumizi ya TEHAMA, mfumo wa kusajili mashauri kwa njia ya mtandao na mwongozo wa uendeshaji wa Kituo Jumuishi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma (aliyesimama)  akifungua mafunzo kwa watumishi wa Mahakama na wadau mbalimbali (hawapo katika picha) watakaohudumu katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kinondoni . Mafunzo hayo ya siku tano yanalenga  kuwajengea uwezo watumishi hao katika maeneo mbalimbali, ikiwemo huduma bora kwa wateja. Katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma, kushoto ni  Mtendaji wa Mahakama, Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Edward Mbara na kulia ni Mtendaji katika Kituo hicho cha Kinondoni, Bw. Beatus Mlando.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kinondoni, Mhe. Franco Kiswaga (aliyesimama) akitoa utambulisho wa meza kuu leo  tarehe 8 Novemba, 2021 katika siku ya kwanza ya mafunzo kwa watumishi wa Mahakama na wadau mbalimbali watakaohudumu katika Kituo hicho (hawapo pichani). Mafunzo hayo ya siku tano yanalenga  kuwajengea uwezo watumishi hao katika maeneo mbalimbali, ikiwemo huduma bora kwa wateja. Katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma, kushoto ni  Mtendaji wa Mahakama, Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Edward Mbara na kulia ni Mtendaji katika Kituo hicho cha Kinondoni, Bw. Beatus Mlando.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakiwemo Mahakimu na Watumishi wa Kituo na watumishi wa Mahakama kutoka Zanzibar pamoja na wawakilishi wa wadau wengine wa Mahakama kutoka wakiwemo Polisi, Magereza, Takukuru na Ustawi wa Jamii.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma (aliyevaa tai nyekundu) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mahakimu wa kituo hicho.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma (aliyevaa tai nyekundu) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wadau wa Mahakama.

  Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma (aliyevaa tai nyekundu) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Mahakama.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma (aliyevaa tai nyekundu) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Mahakama ya Zanzibar.


Muonekano wa nje wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kinondoni.

 

 

 


 

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni