Na Mary Gwera, Mahakama
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Maendeleo ya Kisera na Ushirikiano, Bi. Mari Pangestu amesifu na kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa uboreshaji wa huduma zake kwa wananchi hususani huduma za Mahakama inayotembea ‘Mobile Court Services’ na huduma ya Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki nchini (Intergrated Justice Centres-IJCs).
Mkurugenzi huyo alifanya ziara fupi tarehe 16 Novemba, 2021 ambapo alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, kutembelea Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke (One stop centre for Probate and Family Matters), kupata maelezo ya huduma za Mahakama inayotembea ‘Mobile Court services’ na mwisho kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Maboresho wa huduma za Mahakama wa mwaka 2015/2016-2019/2020, iliyowasilishwa na Jaji wa Mahakama Kuu-Masjala Kuu, Mhe. Zahra Maruma.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa ‘twitter’, Bi. Pangestu ameeleza kufurahishwa kwake na huduma zinazotolewa na Mahakama inayotembea ambapo amesema, “Nilifurahi sana kuona jinsi Mahakama ya Tanzania inavyotoa huduma zake kwa wananchi wakiwemo wanawake na watoto kupitia Mahakama inayotembea ambayo ilipatikana kwa msaada wa fedha kutoka Benki ya Dunia.”
Alikiri kufurahishwa na huduma ya Mahakama hiyo ambayo tangu ianze kutoa huduma Julai mwaka 2019, imesikiliza na kumaliza zaidi ya mashauri 1,600, mbali na usikilizaji wa mashauri amevutiwa pia na huduma nyingine zinazotolewa na Mahakama hiyo ambazo ni pamoja na kutoa elimu ya sheria/ushauri bure wa sheria katika maeneo ambayo yapo mbali na Mahakama.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi huyo wa Benki ya Dunia, alipongeza kuanza kwa utoaji wa huduma kwenye Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJC’s) vilivyozinduliwa tarehe 06, Oktoba 2021 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
“Tumetembelea Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke (One stop centre for Probate and Family Matters), moja ya Vituo sita vilivyojengwa na Benki ya Dunia, Kituo hiki kinatoa huduma mbalimbali za haki chini ya paa moja, huduma hizo ni pamoja na masuala ya talaka, mirathi,” alieleza Bi. Pangestu.
Katika ukaguzi wa jengo la Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Bi. Pangestu alionyesha pia kufurahishwa na muonekano wa jengo na zaidi ni sehemu/chumba maalum cha kunyonyesha watoto kwa ajili ya wateja wanawake wenye watoto wadogo.
Aidha, Bi. Pangestu alitoa pongezi kwa Mahakama ya Tanzania kwa uboreshaji wa huduma zake kufuatia Mradi wa Uboreshaji wa huduma za Mahakama uliofadhiliwa na fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuendelea na uboreshaji wa huduma za Mahakama kuwafikia wananchi wengi.
Mahakama ya Tanzania imepata mafanikio kadhaa kupitia utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa huduma za Mahakama uliofadhiliwa kupitia fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia, hivi sasa Mahakama inaendelea na awamu ya pili ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa pili wa uboreshaji wa huduma za Mahakama wa mwaka 2020/2021-2024/2025.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Maendeleo ya Kisera na Ushirikiano, Bi. Mari Pangestu akifurahia Mahakama inayotembea mara baada ya kupata maelezo ya huduma zinazotolewa na Mahakama hiyo. Bi. Pangestu alipata maelezo ya Mahakama hiyo alipotembelea Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke (One stop centre for Probate and Family Matters) tarehe 16 Novemba 2021.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia, anayeshughulikia Maendeleo ya Kisera na Ushirikiano, Bi. Mari Pangestu (katikati) akifurahia Mahakama inayotembea wakati alipotembelea Mahakama hiyo tarehe 16 Novemba, 2021. Wakati wa ziara yake, Bi. Pangestu alikuta Mahakama hiyo ikitoa huduma katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke Dar es Salaam ambapo alionyesha kufurahishwa na huduma zinazotolewa na Mahakama hiyo ambayo ipo katika mfumo wa gari. Wa kwanza kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Masjala Kuu, Mhe. Zahra Maruma, wa pili kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, wa pili kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia-Tanzania, Bi. Mara Warwick pamoja na Afisa kutoka Benki ya Dunia (wa kwanza kulia) aliyeambatana na Bi. Pangestu.
Picha ya pamoja mbele ya jengo la Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke wakati Bi. Pangestu alipotembelea Mahakama hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni