Na Faustine Kapama, Mahakama-Arusha
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani ametoa wito kwa viongozi mbalimbali nchini kuacha kuzuia utekelezaji wa amri za Mahakama na kujizuia kutoa matamko kwenye mashauri yanayosilizwa mahakamani.
Mhe. Siyani alitoa wito huo leo tarehe 18 Novemba, 2021 alipokutana na
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella kwenye ziara yake ya siku moja ya
Mahakama ambayo ameifanya kukagua shughuli mbalimbali za kiutendaji katika
Kanda ya Arusha.
"Mara nyingi Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya na viongozi, tena wengine
wapo kwenye kamati za ulinzi na usalama huzuia utekelezaji wa amri za Mahakama.
Matukio haya yametokea sehemu mbalimbali nchini kwetu, hivyo tunapopata nafasi
za kukutana na nyingi wenzetu tunakumbushana na ndiyo dhana ya utawala
bora," alisema.
Jaji Kiongozi alibainisha pia uwepo wa viongozi kutolea matamko ya mashauri
ambayo yapo mahakamani, vitendo ambavyo huletea changamoto sana, ambapo wakati
mwingine hupaswa kufika mahakamani kutoa ushahidi kwa kauli ambazo wamezitoa.
"Kwa hiyo unapopata nafasi ya kukutana na Wakuu wa Wilaya ni vizuri
kuwakumbusha wajibu wao kuhakikisha kwamba amri za mahakama zinatekelezwa na
wajizuie kutoa matamko kwenye mashauri yanayoendelea mahakamani. Kufanya
vinginevyo kunaharibu dhana ya utawala bora," alisisitiza.
Jambo jingine ambalo alizungumzia ni juu ya kamati za maadili ambazo
Wakuu wa Mikoa ni wenyeviti katika kamati za mikoa na vile vile Wakuu wa Wilaya
ambao ni wenyeviti wa kamati hizo kwenye wilaya zao. Mhe. Siyani alishangazwa
kukuta kwenye chombo cha habari Mkuu wa Wilaya analalamika kuhusu mwenendo wa
Hakimu fulani au anaandika barua wakati amepewa mamlaka ya kuchunguza mwenendo
wa Hakimu husika.
"Tukuombe uwakumbushe kuhakikisha
zile kamati zinakutana hata kama hakuna malalamiko na zikikutana
hakutakosekana neno la kusema kwa sababu ni vikao vya kisheria, hata kwa kupongezana
kwamba kwa kipindi hiki hapakuwepo na malalamiko," alisema.
Kuhusu ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki, Jaji Kiongozi
alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa ni dhana mpya, kwa maana kuwa majengo hayo
yanahusisha uwepo wa wadau wote wa mfumo wa kutoa haki kwenye jengo moja.
Alibainisha kuwa majengo hayo yametenga sehemu kwa ajili ya wadau hao, hivyo ni
matumaini ya Mahakama kuwa watakaa kwenye maeneo yao ili wananchi akienda wapate
huduma zote.
"Lakini baadhi ya maeneno tumekuta wadau hawa hawakai kwenye ofisi
walizotengewa. Majengo haya yapo kutoa huduma tofauti na zile tulizozizoea.
Mwananchi akihitaji msaada wa kisheria, watu wa sheria wawepo, hivyo ni muhimu
ukatusaidia kuwakumbusha wadau wetu ili kutimiza sababu ya kuanzishwa kwa vituo
hivi,” alimwambia Mkuu huyo wa mMkoa.
Eneo lingine alilogusia Jaji Kiongozi mbele ya Mhe. Mongella ni safari ya
Mahakama kwenda kwenye mtandao kamili kufikia 2025 kama dhamira iliyoelezwa na
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma. Mhe. Siyani alieleza kuwa
Mahakama ya Tanzania imedhamilia kupunguza na baadae kuondokana kabisa na
matumizi ya karatasi.
Alisema kuwa suala hilo siyo la Mahakama pekee bali linahusisha wadau
wote na wananchi kwa ujumla. Kwa mujibu
wa Jaji Kiongozi, ni safari ambayo wadau wote wanapaswa kwenda nayo kwa
vile Mahakama inaweza kuwa na vifaa
vyote lakini unaweza kukuta wananchi hawajisikii kuvitumia.
"Kwa mfano, kwa sasa tunasikiliza mashauri kwa njia ya mtandao na
tunawajulisha watu mashauri mbalimbali kupitia simu zao, na wakati mwingine kwa
sababu ya teknolojia hii hawalazimiki kufika mahakamani, lakini kwa sababu ya
historia mtu anaona asipofika mahakamani atakosa haki yake. Tunakusudia
kuhakikisha kwamba hakuna haki itakayopotea wakati tunaimarisha mifumo ya
matumizi ya teknolojia," alisema.
Mhe. Siyani pia alikumbushia Serikali kuijumuisha Mahakama katika
mipango yake ya maendeleo, mfano pale inapoanzisha wilaya lakini haitengi
maeneo kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama, matokeo yake inapotaka kujenga
hulazimika kulipa gharama kubwa kwa ajili ya kupata kiwanja, gharama ambayo
ingetumika kuboresha miundombinu mahakamani.
"Sisi kwa upande wetu tunafanya mengi kuhakikisha kwamba huduma za
Mahakama zinaboreshwa, lakini tunajua hatuwezi kwenda peke yetu. Mhimili wa
Serikali ndiyo mdau wetu namba moja, kwa
hiyo ushirikiano kati ya Serikali na Mahakama ni jambo ambalo
halikwepeki,"alisisitiza Jaji Kiongozi.
Hivyo aliomba upande wa Serikali kusaidia bila kuleta wasiwasi kwamba
inaingilia uhuru wa Mahakama, ambapo kuna maeneo mengi ambayo Serikali inaweza
kusaidia na watu wakawa na imani kwamba wakienda mahakamani watapata haki bila
kujali nani anayeshitàkiwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa alimshukuru Mhe. Siyani kwa ujio wake na pia kumpongeza
kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na kwamba kwa vile anauwezo mkubwa wa uongozi
ataweza kumudu dhamana hiyo mpya aliyoaminiwa, hivyo kukidhi matarajio ya
mamlaka.
Zaidi ya yote, Mhe. Mongella
alisisitiza uwepo wa mawasiliano kati ya viongozi wa pande zote mbili ili kuwa
na uelewa mpana wa masuala mbalimbali, hivyo kuchochea juhudi za utoaji wa haki
kwa wakati kwa wananchi.
Kuhusu swala la kamati za maadili, Mkuu wa Mkoa huyo alimhakikishia Jaji
Kiongozi kuwa zitakutana ili kushughulikia changamoto zinazojitokeza kwa lengo
la kuboresha utendaji wa mahakimu na watumishi wengine.
Mkuu wa Mkoa pia alisema kuwa suala la viongozi kutolea matamko mashauri
yaliyopo mahakamani ni kosa la mtu binafsi kwa sababu sheria zipo wazi, ila
alisema watajitahidi kuwaambia ili waiache Mahakama ifanye kazi yake.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (katikati) akisisitiza jambo alipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella (kulia) ofisini kwake leo tarehe 18 Novemba, 2021.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella akieleza jambo alipokutana ofisini kwake na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani na viongozi wengine wa Mahakama (hawapo kwenye picha) leo tarehe 18 Novemba, 2021.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni