Na Faustine Kapama, Mahakama-Arusha
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, leo tarehe 18 Novemba, 2021 amefanya ziara ya kikazi ya Mahakama, Kanda ya Arusha kukagua shughuli mbalimbali za kimahakama ambapo amewahimiza watumishi wote watakaohudumu kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kufanya kazi kwa nidhamu na ubora wa hali ya juu huku akionya wale watakaoenda kinyume hawatavumuliwa.
Hii ni mara yake ya kwanza kufanya ziara hiyo tangu ateuliwe na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo
tarehe 8 Oktoba, 2021, ambapo alichukua wadhifa huo kutoka kwa mtangulizi wake,
Jaji Eliezer Mbuki Feleshi ambaye ameteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Ziara ya Mhe. Siyani ilianza kwa kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha,
Mhe. John Mongella ambapo alifanya naye mazungumzo mafupi kabla ya kuelekea
kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Arusha ambapo mara baada ya kukutana na Waheshimiwa
Majaji wa Mahakama Kuu kutoka Kanda hiyo alifanya ukaguzi wa jengo la kituo hicho
kabla ya kuongea na watumishi.
Akiwa katika mkutano na watumishi wa Kituo hicho, Jaji Kiongozi aliwaeleza
bayana matarajio yake na ya Mahakama ya Tanzania kwa ujumla kuwa huduma
zitakazotolewa kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki zitakuwa tofauti na huduma
ambazo zimekuwa zikitolewa miaka yote.
“Tumekuwa na changamoto nyingi na tumezizungumza pamoja kwa miaka mingi.
Sasa ni wakati wa kuachana na changamoto ambazo sote tunazifahamu. Tumekuwa tukisemwa
na kunyoshewa vidole kwa vitendo vya rushwa, lugha mbaya kwa wateja, kwa
kupoteza mafaili na kutotoa huduma zinazoridhisha. Mambo haya hayatapewa nafasi
katika vituo jumuishi. Atakayeona yeye mwenyewe hana uwezo wa kufanya kazi
katika jengo hili alete taarifa kwa Mtendaji kwa sababu hatutavumiliana,”
alisisitiza.
Jaji Kiongozi alisema kuwa uwajibikaji, nidhamu na uadilifu wa hali ya
juu ni vitu ambavyo vinatarajiwa kwenye vituo jumuishi na watumishi wote watapimwa
baada ya mafunzo kuhusu namna gani watafanya kazi, ambapo Msajili wa Mahakama Kuu
aligusia mafunzo hayo yataanza kutolewa hivi karibuni, hivyo alimtaka kila
mtumishi wa Mahakama kuanzia ngazi ya chini mpaka ya mwisho kuwajibika kwa
kiwango tofauti kabisa akiwa kwenye kituo jumuishi.
“Tunataka wananchi watakaokuja kupata huduma katika kituo hiki waone
tofauti sio tu ya uzuri wa jengo bali pia ubora wa huduma tunazozitoa,” Mhe. Siyani
alisema. Alimpongeza Jaji Mfawidhi Kanda ya Arusha, Mhe Moses Nzuna kwa taarifa
nzuri ya utendaji aliyoiwasilisha kwenya mkutano huo ambayo imesheheni mambo
mengi mazuri, ikiwemo kasi ya uskilizaji wa mashauri.
Awali, akiwasilisha taarifa yake, Mhe. Mzuna alieleza kuwa Mahakama Kuu
ya Tanzania, Kanda ya Arusha inaundwa na Mikoa miwili ya kiutawala ya Arusha na
Manyara yenye jumla ya Wilaya 11 ambazo, kwa Mkoa wa Arusha ni Arusha, Arumeru,
Longido, Karatu, Monduli na Ngorongoro na kwa Mkoa wa Manyara ni Babati,
Hanang’, Kiteto, Mbulu na Simanjiro.
Mhe. Mzuna alibainisha kuwa hali ya majengo ya Mahakama imeendelea
kuboreshwa kwa baadhi ya Mahakama kujengewa majengo mapya pamoja na kufanyiwa
ukarabati mdogomdogo ili kuboresha mazingira ya kazi na kusogezwa huduma kwa
wananchi.
Aidha alisema mradi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki
(Integrated Justice Center) umekamilika na tayari shughuli za kimahakama
kuanzia Mahakama ya Mwanzo hadi Mahakama ya Rufani zinafanyika katika jengo hilo.
Hata hivyo alimweleza Jaji Kiongozi kuwa hali ya miundombinu ya Mahakama katika
maeneo mengine hasa Mahakama za Mwanzo bado ni duni.
Kwa upande wa mashauri, Jaji Mfawidhi huyo alisema kuwa kwa Mahakama Kuu
mwaka 2020/2021 takwimu za mashauri zimekuwa zikipokelewa na huwasilishwa Makao
Makuu kwa njia ya mtandao, ambapo hadi tarehe 16 Novemba 2020, jumla ya
mashauri 820 yalibaki na kwa kipindi cha Januari 2021 hadi Novemba 2021 jumla
ya mashauri 627 yalipokelewa, yaliyomalizika yalikua 842 na hivyo kubakia
mashauri 820.
Kwa upande wa Mahakama Kuu, Masjala ya Kazi, Mhe. Mzuna alibainisha kuwa
hadi kufikia mwezi Novemba 2021 kulikua na mashauri 290 yaliyopokelewa na 405
yalimalizika na jumla ya mashauri yaliyosalia yalikua 389. Kwa upande wa
Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya, Kanda ya Arusha, Jaji Mfawidhi alisema hadi
kufikia mwezi Novemba 2021 yalipokelewa mashauri 2,981 ambapo jumla ya mashauri
3,170 yalisikilizwa na yaliyosalia ni 2,174.
Kuhusu Mahakama za Mwanzo, Jaji Mfawidhi alimweleza Mhe. Siyani kuwa hadi
kufikia Octoba 2021, yalisalia jumla ya mashauri 981 katika Mkoa wa Arusha,
huku katika kipindi cha January 2021 hadi Octoba 2021 jumla ya mashauri 7,091
yalipokelewa. Aidha jumla ya mashauri 7,171 yalisikilizwa na hivyo mashauri 901
yalisalia.
Kwa mujibu wa Mhe. Mzuna, mashauri ya watoto nayo yalipewa kipaumbele
cha pekee ambapo alisema hadi kufikia Novemba 2021 yalipokelewa jumla ya
mashauri 126 na yaliyomalizika yalikuwa 99, hivyo kufanya mashauri yaliyobaki hadi
sasa kuwa 72 ambayo yanayoendelea kusikilizwa.
Katika ziara hiyo, Jaji Kiongozi aliambatana na viongozi wa Mahakama ya Tanzania
kutoka Makao Makuu, wakiwemo Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Shamillah Sarwatt, Katibu wa Jaji Kiongozi, Mhe. Obadia Bwegoge na Mtendaji wa
Mahakama Kuu, Masjala Kuu anayeshughulikia Mahakama za Hakimu Mkazi, Bi. Masalu
Kisasila.
Meza kuu ikiongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani ipo tayari kwa ajili ya mkutano wa watumishi. Kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna na kulia ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Shamillah Sarwatt.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni