Na Magreth Kinabo – Mahakama
Jaji wa Mahakama Rufani ya
Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo jana tarehe
18 Novemba, 2021 amefungua kongamano namna ya utoaji adhabu, ambapo amewaomba
washiriki kubadilishana uzoefu ili kuweza kutatua changamoto wanazozikabili
wakati wa utoaji adhabu kwa wakosaji mahakamani.
Kongamano hilo ambalo limeandaliwa
Mahakama Tanzania kupitia Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa
ushirikiano wa Ubalozi wa Uingereza na Taasisi ya Majaji Wastaafu nchini
Uingereza (Slynn Fundation) limefanyika katika
Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
“Kama vile tunavyofahamu
kwamba katika uendeshaji na usikilizaji wa mashauri inapofikia hatua ya mwisho
wa utoaji adhabu ni kipindi kigumu na kinachangamoto,’’ Mhe. Dkt Kihwelo
aliwaambia washiriki wa kongamano hilo.
Aliongeza kuwa kutokana na
ugumu huo ni vizuri mafunzo juu ya suala hilo yakatolewa mara kwa mara au
wakati wa mafunzo elekezi ili kuweza kuwa na uelewa mpana na uwiano wa adhabu ambazo
zinaweza zikatolewa.
Hivyo, Jaji huyo wa
Mahakama ya Rufani alisema kuwa kupitia
kongamano hilo Jaji Mstaafu Nic Madge kutoka Taasisi ya Majaji Wastaafu
ya Uingereza atatoa uzoefu wa nchi ya Uingereza kwenye utoaji wa adhabu na uzoefu
wa Tanzania utatolewa na Jaji Mstaafu wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Robert
Makaramba, kupitia Mwongozo wa Utoaji adhabu Tanzania.
Dkt. Kihwelo aliongeza
kwamba mwongozo huo umetayarishwa kwa msaada kutoka Ubalozi wa Uingereza. Aliushukuru
Ubalozi wa Uingereza kwa msaada iliyoutoa kwa kuwezesha mafunzo hayo kufanyika,
ambapo jumla Majaji 14 na Mahakimu wanne wamehudhuria kongamano hilo.
Jaji Mahakama
ya Rufani Tanzania, Mhe. Paul Kihwelo (wa pili kulia) akiwa katika picha ya
Pamoja mara baada ya kufungua kongamano hilo. Wengine ni washiriki wa kongamano
hilo.
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania,
Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akifungua kongamano la namna ya Utoaji adhabu lililofanyika jana kwenye Hoteli ya Serena, jijini Dar es Saalam.
Jaji Mahakama
ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt.Paul Kihwelo (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji na Mahakimu walioshiriki Kongamano mara baada ya kufungua.
Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe.Robert Makaramba akitoa uzoefu wa namna ya kutoa adhabu katika nchi ya Tanzania wakati wa Kongamano hilo.
Jaji Mstaafu kutoka Taasisi ya Majaji Wastaafu ya
Uingereza (SYLNN FOUNDATION) Mhe. Nic Madge akitoa uzoefu wa namna ya utoaji adhabu katika
nchi yake.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza wakati alipotembelewa na ujumbe kutoka Sylnn Foundation leo ofisini kwake jijini Dar es salaam. Jaji Mkuu alisema, hivi sasa Sheria zinafanyiwa marekebisho ikiwemo Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai pamoja na Sheria ya Kanuni ya adhabu. Alisema pia ni vizuri Taasisi hiyo ikaendeleza ushirikiano na Mahakama ya Tanzania katika kutoa mafunzo kwa Majaji, Mahakimu na wadau wanaofanya kazi na Mahakama ya Tanzania.
Sehemu ya wajumbe kutoka Taasisi ya Sylnn Foundation ya Uingereza wakiwa ofisini kwa Jaji Mkuu walipomtembelea leo jijini Dar es salaam.Jaji Mstaafu kutoka Taasisi ya Majaji Wastaafu ya Uingereza (SYLNN FOUNDATION) Mhe. Nic Madge akiangalia kitabu cha Mpango Mkakati Mpya wa Mahakama ya Tanzania mara baada ya kukabidhiwa na Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Taasisi ya Sylnn Foundation walipomtembelea leo ofisini kwake jijini Dar es salaam. Kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Paul Kihwelo
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni