Na Lydia Churi-Mahakama
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan amemtumia salaam za rambirambi Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma kufuatia kifo cha Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania
Mhe. Njengafibili Mponjoli Mwaikugile kilichotokea mwishoni mwa wiki jijini Dar
es salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais, Ikulu Bw. Jaffar Haniu tarehe 20 Novemba, 2021 jijini Dar
es salaam, Rais Samia amesikitiswa na kifo cha Jaji Mstaafu Mwaikugile kwa kuwa
alikuwa na mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa.
Katika taarifa hiyo, Rais ametoa pole kwa Jaji Mkuu wa
Tanzania pamoja na wanafamilia wote wa Mahakama na kuw omba kuwa na moyo wa
uvumilivu katika kipindi hiki kigumu na cha majonzi na pia amemuombea marehemu
apumzike mahali pema peponi.
Kwa mujibu wa Msajili wa Mahakama Kuu
ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt, Jaji Mwaikugile alikutwa na umauti tarehe
20 Novemba, 2021 jijini Dar es Salaam.
Taratibu za mazishi zinaendelea,
ambapo; taarifa za awali zinasema kuwa marehemu Jaji Mwaikugile atazikwa siku ya Jumatano tarehe
24 Novemba, 2021 jijini Dar es Salaam. Msiba upo nyumbani kwake Salasala, Dar es Salaam.
Mahakama ya Tanzania inatoa pole kwa
familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia msiba huu.
Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe.
Njengafibili Mwaikugile enzi ya uhai wake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni