Jumatatu, 22 Novemba 2021

SIKU TANO ZATUMIKA KUWAFUNDA WATUMISHI WA MAHAKAMA MOROGORO


Na Evelina Odemba - Morogoro

Mafunzo yaliyokuwa yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa watumishi wanaofanyakazi kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kilichopo Morogoro ili kuboresha ufanisi katika utoaji huduma za haki kwa wananchi yamehitimishwa tarehe 19 Novemba, 2021, huku wito wa mabadiliko ukitawala katika mafunzo hayo.

Mafunzo hayo yaliyotolewa kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 15 Novemba, 2021 ambayo yalihusisha pia wadau mbalimbali wa Mahakama yaliyofunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe ambaye aliwataka wadau na watumishi wa Mahakama kuwa tayari kwa mabadiliko na kutoa huduma kwa wananchi kwa weledi wa hali ya juu.

Mhe. Ngwembe pia alisisitiza watumishi wa Mahakama kuwa chachu ya mabadiliko na mabalozi wazuri katika utoaji haki na kuwasikiliza wateja wote wanaofika katika ofisi za Mahakama na kuwahudumia kwa usahihi. “Tunategemea kuona mabadiliko katika utumishi wenu baada ya mafunzo haya” aliongeza.

Miongoni mwa wawezeshaji katika kipindi cha mafunzo alikuwa Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Temeke kinachojihusisha na masuala ya ndoa na talaka na yale ya kifamilia, Mhe. Ilvin Mgeta ambaye alifundisha juu ya maadili kwa watumishi na kuweka wazi kuwa ni wakati sahihi kwa jamii kupata huduma wanayoitarajia toka Mahakamani, hivyo akatoa wito kwa kila mtumishi kufanye kazi kwa ufanisi ili kuifikia Dira ya Mahakama ya “Haki Sawa kwa Wote na kwa Wakati.”

Aliongeza kuwa kwa miaka 60 wananchi wa Morogoro wameitafuta haki na sasa haki imekuja nyumbani kwao, hivyo watumishi wa Mahakama wanapaswa kutoa huduma za haki zile wananchi wanazotarajia kupata. Alisema kuwa uwepo wa huduma za Mahakama Kuu umewarahisishia wananchi wa Mkoa wa Morogoro ambao hapo awali walikuwa wakisafiri kuifata huduma hiyo Mkoani Dar es Salaam kwa miaka mingi.

Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, Bw. Ahmed Selemani Ngeni alitoa shukurani za dhati kwa wawezeshaji na wote walioshiriki mafunzo hayo na akuongeza kuwa maelekezo yote yaliyotolewa yatawasaidia kuboresha utendaji kazi.


Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Temeke kinachojihusisha na masuala ya ndoa na talaka na yale ya kifamilia, Mhe. Ilvin Mgeta, akisistiza jambo wakati akitoa mada juu ya maadili kwenye mafunzo yaliyokuwa yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa watumishi wanaofanyakazi kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kilichopo Morogoro. 

Sehemu ya watumishi wanaofanyakazi kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kilichopo Morogoro (juu na chini) wakifuatilia mafunzo hayo.



Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, Mhe Paul Ngwembe akiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali wa Mahakama (waliosimama) walioshiriki katika mafunzo hayo. Waliokaa kulia kwa Mhe. Ngwembe ni Hakimu Mfawidhi Mwandamizi Mh. Lome Mwapemela na Hakimu Mkazi Mwandamizi Mh. Christopher Bwakila, kushoto kwake ni Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, Mhe Arnold Kilekiano na Naibu Mrajis Mhe. Valentina Katema kutoka Zanzibar.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, Mhe Paul Ngwembe akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro (waliosimama juu na chini) walioshiriki katika mafunzo hayo.



Sehemu nyingine ya watumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro walioshiriki katika mafunzo hayo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni