Na Innocent Kansha – Mahakama.
Chuo cha Uongozi wa Mahakama - Lushoto kimeandaa mafunzo mengine kwa Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kuboresha utoaji huduma kwa jamii, kuongeza weledi na kuhakikisha kuwa Mahakama ya Tanzania inakuwa na maafisa wa kada hizo wenye maadili, mbinu bora na nyenzo za kufanyia kazi.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 6 Desemba 2021 na Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Bw. Goodluck Chuwa alipokuwa akifungua mafunzo hayo ya siku 14, ambayo ni ya awamu ya nane toka kuanzishwa kwake mwaka 2018 katika Ukumbi wa Shule ya Sheria kwa Vitendo jijini Dar es salaam
"Lengo kuu la mafunzo haya ni kuboresha utoaji huduma kwa jamii, kuongeza weledi na kuhakikisha kuwa Mahakama inakuwa na Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wenye maadili, mbinu bora na nyenzo za kufanyia kazi. Ili kuweza kufikia huko ni muhimu kuwa na utulivu wa kutosha na kuzingatia yale yote yaliyopangwa katika ratiba ya mafunzo, ushiriki kamilifu ndiyo utakaowafikisha kwenye utoaji wa huduma bora.
"Kuanzishwa kwa mafunzo haya ni mojawapo ya sehemu ya uboreshaji mkubwa unaoendelea katika Mhimili wa Mahakama ili kuondoa malalamiko mengi yaliyokuwepo kutoka kwa wananchi kwani moja ya eneo lenye kulalamikiwa ni ukosefu wa uadilifu wakati wa utekelezaji wa majukumu na kwa kufanya hivyo kutawawezesha Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kufanya kazi kwa uadilifu na kufuata kanuni zilizopo," alisema Bw. Chuwa alipokuwa akiongelea ubora wa mafunzo hayo.
Alisisitiza kuwa Madalali wa Mahakama ni wadau muhimu sana katika utekelezaji wa jukumu la utoaji haki kwa wananchi, hivyo endapo watafanikiwa kuhitimu mafunzo yao na kusajiliwa watakuwa maafisa wa Mahakama na kupewa jukumu la kutekeleza amri halali za Mahakama.
"Jukumu hilo msipolitekeleza vyema mtalalamikiwa kwa kutokuwatendea haki wananchi na kwa hiyo ni dhahiri kuwa Mahakama pia itakuwa imelalamikiwa. Niwasihi kuwa baada ya kupata mafunzo haya mkazingatie kanuni na maadili mtakayofundishwa katika kutelekeleza majukumu yenu. Nafahamu kuwa mtajifunza mambo mengi katika kipindi hiki cha wiki mbili, yakiwemo masuala ya maadili katika fani ya udalali na usambazaji nyaraka. Kila fani ina maadili yake na wale watakaopata nafasi ya kufanya kazi ya udalali au usambazaji nyaraka za Mahakama ni muhimu kuzingatia maadili ya kazi hiyo”, alitilia mkazo Kaimu Mkuu huyo wa chuo.
Aidha, Bw. Chuwa amewakumbusha washiriki kuwa mafunzo hayo yameanzishwa mahususi kwa lengo la kuweka utaratibu rasmi wa kurasimisha namna ya kuwapata Madalali pamoja na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kitu ambacho hakikuwepo hapo awali. Mafunzo hayo yanafanyika kwa mujibu wa Kanuni zilitolewa na Jaji Mkuu wa Tanzania ambapo kupitia kanuni hizo mtu yeyote mwenye nia ya kufanya kazi ya udalali na Usambazaji Nyaraka za Mahakama anapaswa kupata mafunzo hayo.
Ili kutatua
changamoto ya upatikanaji wa Madalali na Wasambaza nyaraka za Mahakama wenye
sifa, Mhimili wa Mahakama kupitia Mpango Mkakati wake wa kwanza wa mwaka 2015/2016 -
2019/2020 na Mradi wa Uboreshaji wa Mahakama kupitia mradi wa huduma
zinazomlenga mwananchi, iliandaa kanuni ziitwazo Kanuni za Uteuzi, Gharama,
Malipo na Nidhamu za Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama, Tangazo la
Serikali Namba 363 la 2017 (The Court Brokers and Process Servers
(Appointment, Remuneration and Disciplinary) Rules, GN. 363 of 2017).
“Kwa kuanzishwa mafunzo haya na kufuatiwa kwa kutungwa kwa kanuni hizo, hivi sasa Madalali wa Mahakama na Wasambaza Nyaraka za Mahakama zimekuwa ni kada mbili tofauti na hivyo mtu ana uwezo wa kuchagua moja kati ya kada hizo na ndiyo maana baadhi ya washiriki wa mafunzo haya wanasomea kada zote wakati kuna baadhi wanasomea kada moja tu”, alifafanua Kaimu Mkuu huyo.
Kwa kuzingatia jina la Kanuni linavyosomeka kanuni hizo zinahusu uteuzi, gharama, malipo na nidhamu za Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama ambapo mchakato huo ulikamilika mwaka 2017 baada ya kupata kanuni hizo ambazo zilitolewa na Jaji Mkuu wa Tanzania, aliongeza Bw. Chuwa.
Alitoa rai kwa washiriki kuwa wakati wanaendelea na mafunzo hayo waweke ndani yake mijadala huru itakayowasaidia kuboresha utendaji kazi wao ili kupunguza malalamiko yanayotokana na wananchi kutokupata huduma bora. "Msisite kuchangia uzoefu wenu kwa lengo la kuboresha na kuwaeleza wengine kipi kinachotakiwa kufanyika au kueleweka. Kwenu washiriki kosa hata liwe dogo sana katika utekelezaji wa majukumu yenu linaweza kuleta madhara makubwa kwa mtu binafsi, familia, Mahakama na Taifa kwa ujumla", alisema.
Picha
ya pamoja ya washiriki wa Mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama
wakiwa na meza Kuu mara baada ya Mgeni rasmi kufungua mafunzo hayo
yanayofanyika katika Chuo cha Sheria kwa Vitendo Jijini Dar es salaam, (katikati) ni mgeni rasmi
(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni