Ijumaa, 10 Desemba 2021

TAWJA YAKABIDHI KANDA YA MOROGORO KITABU CHA MWONGOZO WA MASHAURI

 Na Evelina Odemba - Morogoro

Uongozi wa Chama cha Wanawake Mahakimu na Majaji Tanzania (TAWJA) tarehe 8 Desemba 2021 umekabidhi kitabu katika kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro ili kuwasaidia Majaji na Mahakimu kupata nukuu tofauti tofauti za kusimamia wakati wa kutekeleza majukumu yao ya utoaji haki.

Kitabu hicho kilichozinduliwa Ikulu hivi karibuni na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ikimepewa jina la “Gender Bench Book on Women’s Rights” ambacho kinazungumzia masuala mbalimbali yanayomuhusu mwanamke upande wa sheria pamoja na hukumu zilizotolewa kwenye mashauri yanayohusu mwanamke.

Akizungumza wakati wa kupokea kitabu hicho, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe alitoa pongezi za dhati kwa TAWJA kwa kufanikisha kuandaa kitabu hicho muhimu ambavyo kimesheheni ukweli unaopatikana katika jamii, huku akiongelea kuwa ukimpa haki mwanamke ni sawa na kuipa haki jamii nzima.

Mhe. Ngwembe ambaye aliambata na Jaji mwingine anayehudumu katika Kanda hiyo, Mhe. John Chaba aliongeza kwa kusema kuwa “haki ya mwanamke ni haki ya jamii nzima” hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha mwanamke anapatiwa haki stahiki.

Naye Kaimu Msajili Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, Mhe. Maua Hamduni aliongezea kwa kusema kuwa kitabu hicho ni muhimu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku na kitawarahisishia katika uwajibikaji kwani kimezingatia nukuu mbalimbali za mashauri yaliyosikizwa na Majaji waliootoa uamuzi ambao ni mwongozo ulio bora.

Akifafanua yaliyomo katika kitabu hicho, Mratibu wa TAWJA ambaye pia ni Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Morogoro Mjini, Mhe. Adela Nyambele alisema kuwa kitabu kimechambua sheria ambayo inamlinda mwanamke katika kila nyanja mbalimbali ikiwemo ajira, ndoa na hata katika biashara na pia kiana uamuzi unaohusu mashauri juu ya unyanyasaji wa wanawake.

Kitabu cha Women’s Access to Justice in Tanzania kinategemewa kugawaiwa kwa Majaji na Mahakimu wote waliopo katika Kanda hiyo pia baadhi ya nakala zitawekwa kwenye Maktaba ya Mahakama iliyopo ndani ya Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki mkoani hapo ili mtu yeyote mwenye uhitaji aweze kukisoma.

Jaji Mawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, Mhe Paul Ngwembe (katikati) pamoja na Mhe.  John Chaba, Jaji mwingine anayehudumu katika Kanfda hiyo (wa pili kulia) wakiwa na viongozi wa TAWJA baada ya kupokea kitabu cha mwongozo wa mashauri.


Baadhi Mahakimu kutoka Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, wakiwa na kitabu hicho.


Kaimu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, Mhe. Maua Hamduni (wa tatu kutoka kushoto) akipokea kitabu toka kwa mratibu wa TAWJA, Mhe. Adella Nyambele (kulia). Waliosimama kushoto ni Mhe. Beatha Richard na Mhe Shida Nganga, ambao ni viongozi wa TAWJA Kanda ya Morogoro walipotembelea Ofisi za Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki na kugawa  vitabu hivyo.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni