Na Faustine Kapama na Innocent Kansha - Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaonya Mawakili kote nchini
kuacha kutumia majina ya Majaji na Mahakimu ili kujipatia kipato kikubwa kutoka
kwa wateja wao wanapokuwa wanawawakilisha mahakamani.
Akizungumza
katika sherehe ya kuwapokea na kuwakubali Mawakili wapya 313 katika Viwanja vya
Karimjee Jijini Dar es Salaam leo tarehe 10 Desemba, 2021, Mhe. Prof. Juma
amebainisha kuwa wamekuwa wakipokea malalamiko kuwa Mawakili wanapotoza malipo
kutoka kwa wateja wao hujumuisha na mgao wa Majaji na Mahakimu wanaosikiliza
mashauri mbalimbali kutoka kwa wateja.
“Tumepokea
malalamiko kuwa baadhi ya Mawakili huwatoza wateja wao pesa zaidi kwa madai
kuwa sehemu yake hupelekwa kama mgao kwa Jaji au Hakimu. Sisi hatuchukui mgao
hata siku moja. Majaji na Mahakimu hawachukui mgao hata siku moja. Lakini wapo Mawakili ambao wanataka fedha zaidi ya sheria inavyotamka na kusema kiasi hiki
ni kwa ajili ya kamati yake ya ufundi ili kupelekwa kwa Jaji au Hakimu. Napenda
kuwaambia wananchi, ukikutana na Wakili wa aina hiyo tuletee, tutamfuta katika
orodha ya Mawakili dakika hiyo hiyo. Nawaomba sana Majaji tutumie mamlaka
tuliyonayo ili kurudisha nidhamu,” Jaji Mkuu ameonya.
Kwa
mujibu wa Jaji Mkuu, rushwa
na utovu wa maadili ni changamoto ambayo inachafua imani, hadhi na taswira ya
mfumo mzima wa utoaji wa huduma za uwakili ambazo zitawanyima fursa ya
ushindani sio tu katika eneo huru la biashara la Afrika, bali hata katika Kituo
cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro.
“Zama za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda haina nafasi kwa Mawakili wasio na maadili na pia wale wanaotoa huduma zilizo chini ya viwango.
Katika zama hizi za utandawazi na teknolojia ya habari, unahitaji Wakili mmoja
tu asiye na maadili au asiye na viwango, kuweza kuchafua sifa za Mawakili wote
wa Tanzania,” amesema.
Mhe. Prof. Juma ameeleza pia kuwa baadhi ya Mawakili
wanashindwa kutambua kuwa wao ni maafisa wa Mahakama na ni nguzo muhimu ya
utetezi wa uhuru wa Mahakama na kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama, lakini
kwa bahati mbaya, badala ya kukosoa uamuzi wa Mahakama kwa haki, wanajificha
nyuma ya majina ya bandia katika mitandao ya kijamiii na kupotosha uamuzi huo.
“Wengine wanatumia mitandao ya kijamii kuwashambulia
Majaji na Mahakimu kwa jina na kwa picha kwa lengo la kuwafedhehesha na
kuwadhalilisha. Hii haikubaliki. Huyo Wakili hastahili kabisa kuwa kwenye
orodha ya Mawakili. Najua Mawakili kama hao hukimbilia kusema ni haki za
binadamu, lakini haki za binadamu zinapande zote, zinaheshimu uhuru wa
Mahakama, zinaheshimu utawala wa sheria na kufuata taratibu. Unapochafua
taswira ya Mahakama, kumbuka unachafua taaluma yako ya uwakili, hivyo nawaomba
sana msiwe Mawakili kama hao. Bahati nzuri wote tunawafahamu, siku zao zimekwisha,” aliwaeleza Mawakili hao wapya.
Jaji Mkuu alieleza kuwa asilimia kubwa ya Mawakili
ambao hulalamikiwa mbele ya Kamati ya Maadili ya Mawakili wanakuwa hawana
mikataba ya kazi na wateja wao. Alieleza kuwa athari za kutoandikishiana mikataba
hujitokeza malalamiko yanapofikishwa mbele ya Kamati ya Mawakili na inakuwa
vigumu kwa mteja kuthibitisha madai yake.
“Ni muhimu kwa kila Wakili kuwa na mkataba na kila
mteja anayemwakilisha mahakamani. Mawakili wengi wanapokea fedha kutoka kwa wateja
wao lakini hawatoi risiti. Changamoto hii hujitokeza wakati wateja wakifikisha
malalamiko katika Kamati ya Mawakili. Hofu tuliyonayo sasa hivi ni kwa kiasi
gani Mawakili watakapoanza kutoa huduma Mahakama za Mwanzo watapeleka
changamoto ambazo hivi sasa Mawakili wanalalamikiwa,” alibainisha.
Akizungumza katika sherehe hizo, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi aliwakumbusha Mawakili hao wapya mambo
mbalimbali ambayo wanapaswa kuyazingatia wanapotekeleza majukumu yao kwa
Mahakama, kwa mteja, kwa umma, kwa Mawakili wengine na taaluma yenyewe ya
sheria ili kurahisisha utoaji wa haki kwa wananchi, ikiwemo kuzingatia maadili
ya kazi zao kwa kuwa uwakili ni taaluma adhimu.
Amesema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 66 cha sheria
ya Mawakili, Sura ya 341, Mawakili kama maafisa wa Mahakama wana wajibu wa
kuisaidia Mahakama kufikia uamuzi wa haki na kwa wakati ambapo Kanuni ya 92 (1)
ya Maadili ya Mawakili inawataka kuheshimu Mahakama pamoja na uamuzi unaotolewa
hata kama hawajaridhika nao, yapaswa kuchukua fursa ya nafuu zilizowekwa na
sheria katika kuhoji uamuzi huo.
“Aidha, Kanuni ya 92 (2) ya Maadili ya Mawakili
inakataza Mawakili kuhujumu wajibu wa Mahakama wa utoaji haki katika
utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za uongo au
kupotosha uamuzi wa Mahakama au taratibu za uendeshaji wa mashauri kwa njia
yoyote,” alisema Dkt. Feleshi.
Akizungumzia mabadiliko ya sheria yaliyowaruhusu
kuwakilisha wateja katika Mahakama za Mwanzo, Mhe. Dkt Feleshi aliwakumbusha
Mawakili hao kuwa Mahakama hizo zitaendelea kutumia taratibu kama
zinavyoainishwa katika Sheria na Kanuni zinazoongoza mienendo ya mashauri,
hivyo wanapaswa kuzifuata.
“Naomba kuwaasa Mawakili wote mtakaowawakilisha wateja
wenu katika Mahakama za Mwanzo kwamba, kuruhusiwa kwenu katika Mahakama hizo
iwe chachu ya kuongeza kasi na ufanisi katika upatikanaji wa haki kwa wakati.
Msiende kuibua masuala ya kiufundi yatakayosababisha ucheleweshaji wa mashauri
kwa makusudi au dhamira ovu katika Mahakama hizo isiyozingatia maslahi ya
haki,” alionya Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria
Tanganyika (TLS), Mhe. Prof. Edward Hosea, aliwaeleza Mawakili hao kuwa tasnia
ya uwakili ni tasnia ya kipekee inayohitaji uadilifu mkubwa, kusoma, kujituma,
kushirikiana na Mawakili wengine katika kuboresha tasnia hiyo na kufanya tafiti
ili kuweza kufikia malengo yao na kutoa huduma bora kwa jamii.
“Wakati mnasherehekea mafanikio yenu ya kufikia hatua
hii kubwa katika tasnia hii, ni muhimu kutambua kuwa, ukiwa Wakili, Sheria imekupa
wajibu mkubwa kwa mteja, Mahakama, jamii na Mawakili wenzako. Ni nyema kutambua
wajibu wako huu na kuutimiza,” alisema Rais huyo.
Prof. Hosea amesema kuwa katika kutekeleza wajibu wao Mawakili hao wanatakiwa kuzingatia viwango vya utendaji wa sheria na maadili
yake ipasavyo kama inavyoelezwa katika
Sheria ya Mawakili Sura. 341 na Kanuni ya Mawakili, 2018.
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa hotuba katika Mahafali
ya 65 ya kuwapokea na kuwakubali mawakili wapya 313 yaliyofanyika leo tarehe 10
Desemba 2021, kwenye viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam.
Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akitoa hotuba yake katika
hafla hiyo.
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Shamillah Sarwatt akiongoza kiapo cha uadilifu kwa Mawakili wapya waliopokelewa leo tarehe 10 Desemba, 2021 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Baadhi ya Mawakili wapya wakila kiapo cha uadilifu katika majukumu ya taaluma hiyo.
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwapokea na kuwakubali
mawakili hao.
Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (wa pili kushoto), (wa kwanza
kushoto) ni Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Boniface Luhende, (wa pili
kulia) ni Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP)Sylvester Mwakitalu,na (wa kwanza
kulia) ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS) Mhe. Prof. Edward Hosea
wakiwa wamesimama kwa ajili ya kuwapokea na kuwakubali mawakili hao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni