Ijumaa, 10 Desemba 2021

MAWAKILI WA KUJITEGEMEA WALA KIAPO CHA UADILIFU

 Na Faustine Kapama na Magreth Kinabo, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 10 Desemba, 2021 amewapokea na kuwakubali Mawakili wapya 313, ambao wamekula kiapo cha uadilifu kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa tasnia hiyo hapa nchini.

Sherehe za kuwapokea Mawakili hao zimefanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam na kuhudhuliwa na wageni na waalikwa mbalimbali, wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Mashtaka, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Wajumbe wa Baraza la Elimu ya Sheria, Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) pamoja na watendaji wengine wa Mahakama wa ngazi mbalimbali.

Mawakili wapya na wageni mbalimbali walianza kuwasili katika viwanja hivyo majira ya asubuhi na shamrashamra za sherehe hiyo zilizokuwa zikirushwa mubashara na Kituo cha Televisheni cha Taifa-TBC 1, zilianza majira ya saa tatu asubuhi kwa Mhe. Prof. Juma ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi kufika katika eneo hilo na baadaye kuwakubali na kuwapokea Mawakili hao.

Baada ya zoezi hilo, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Shamillah Sarwatt aliwainua Mawakili hao wapya kwa ajili ya kula kiapo cha uadilifu, zoezi ambalo limekuwa la kwanza tangu tasnia hiyo ianzishwe hapa Tanzania. Baadaye, Jaji Mkuu wa Tanzania aliwakabidhi vyeti Mawakili hao kama ishara ya kuanzia sasa wanakuwa Mawakili wa Kujitegemea na watakuwa na wajibu sio tu wa kuwawakilisha wateja wao bali pia kuisaidia Mahakama ya Tanzania katika kufikia uamuzi wa haki kwa wananchi.

Akizungumza kwa ufupi kuhusu hatua hiyo, Mhe. Prof. Juma alibainisha kuwa hapo awali Mawakili wapya walikuwa hawali kiapo cha uadilifu kama walivyo watumishi wengine wa umma wanapoteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali, jambo ambalo lilipelekea uongozi mpya wa TLS kuja na pendekezo la kuwepo kwa utaratibu huo kwa  Mawakili wote watakaokubaliwa na kupokelewa kuwa Mawakili wa Kujitegemea, kuanza kula kiapo cha uandilifu, pendekezo ambalo lilikubaliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania.

“Nimefurahi kuona kuwa mmekula kiapo cha uadilifu, na hili wazo lilitoka kwa Rais wenu wa Chama cha Mawakili Tanganyika aliponitembelea ambapo alionesha nia ya kupambana na utovu wa maadili na akatuuliza kama kuna sehemu ambayo tunaweza kuwataka Mawakili kula kiapo cha uadilifu. Ninyi ni Mawakili wa kwanza kabisa kula kiapo cha uadilifu na tutapimana. Baada ya muda tutaangalia kama hicho kiapo kilikuwa ni cha siku ya leo kuturidhisha mpate vyeti au mtakuwa waadilifu wa kudumu,” alisema Jaji Mkuu.

Akizungumza katika sherehe hizo, Rais wa TLS Prof. Edward Hosea amebainisha kuwa Chama kinaendela na utekelezaji wa maono yake ya  kupambana na vitendo haramu na visivyo ya kimaadili vya utendaji wa kazi za uwakili vilivyoshamiri mijini. Amesema kuwa vitendo hivyo vimesababisha kushuka kwa hadhi ya taaluma hiyo adhimu, hivyo kusababisha kukosa kuaminiwa na Serikali, wadau mbalimbali na jamii kwa ujumla.

Amevitaja miongoni mwa vitendo hivyo kama uwepo wa Vishoka wa Uwakili, ambao ni baadhi ya watu wanaofanya kazi za uwakili wakati sio mawakili. Kwa mujibu wa Prof. Hosea, watu hao wamekuwa wakifanya kazi mbalimbali za kiuwakili kama  kuandaa na kuthibitisha nyaraka,  kushuhudia  viapo, kuwakilisha wateja mahakamani na kazi nyinginezo  za uwakili.

“Wahalifu wa vitendo hivi viovu ni watu wanaojifanya ni Mawakili lakini sio, pamoja na Mawakili wanaofanya kazi zao kinyume na maadili ya uwakili kama kutoa huduma ya kisheria bila kuwa na leseni halali, kufanya kazi za uwakili katika mazingira yasiyofaa kama  madukani, barabarani na vijiweni, kuruhusu mihuri yao kutumiwa na mtu asiye Wakili na kutoza ada za uwakili chini ya kiwango kilichowekwa kisheria,” amesema. 

Amebainisha pia kuwa Chama cha Wanasheria Tanganyika kimekua kikipokea malalamiko lukuki kutoka wa wateja wakilalamika dhidi ya vitendo viovu visivyo vya kiuwakili vifanywavyo na Mawakili kama kuwatekeleza wateja wao na kutohudhuria mahakamani, matumizi mabaya ya fedha za wateja, kutokuwepo na mawasiliano mazuri na kuvunjika kwa usiri kati ya Wakili na mteja wake.

“Ni wito wangu leo kwa Mawakili kuhudhuria mahakamani, kusimamia na kufanya kazi za wateja wenu  kwa uadilifu, ili kuhakikisha haki za wateja zinapatikana kwa wakati na kwa utimilifu. Ni wito wangu pia kwa Mawakili kufungua akaunti za wateja ili kuepuka kutumia fedha  bila idhini zao,” amesema.

Hivyo, amesisitiza Mawakili wanapaswa kuwa na mawasiliano mazuri na wateja wao kwa kuwapa mrejesho wa kesi au kazi zao, kupokea simu na kujibu ujumbe wa mteja, kutunza siri zao na kwa kufanya hivyo wataweza kulinda taaluma hiyo adhimu na kurudisha hadhi ya tasnia yao inayoonekana kushuka siku hadi siku.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa hotuba katika Mahafali ya 65 ya kuwapokea na kuwakubali mawakili wapya 313 yaliyofanyika leo tarehe 10 Desemba 2021, kwenye viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam. 

Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt akiongoza kiapo cha Mawakili wapya (picha ya chini) mara baada ya kupokelewa na kukubaliwa kuwa Mawakili wa kujitegemea.


Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS), Mhe. Prof. Edward Hosea akisisitiza jambo wakati wa sherehe hiyo.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma(kushoto) akikaribishwa na Kaimu Jaji Kiongozi Mhe. John Mugeta (katikati) leo kwenye viwanja vya Karimjee, Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwapokea na kuwakubali mawakili wapya 313, (kulia) ni Msajili wa Mahakama ya Rufani (T) na Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Kevin Mhina.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma(kushoto) akiwaongoza Majaji wa Mahakama ya Rufani na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuingia katika viwanja vya Karimjee leo kwa ajili ya hafla ya kuwapokea na kuwakubali mawakili wapya, (Kulia) ni Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Kevin Mhina.

Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiingia katika viwanja hivyo.

Baadhi ya wajumbe wa menejimenti ya Mahakama ya Tanzania wakifuatilia hafla hiyo.

(Picha na Magreth Kinabo na Innocent Kansha-Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni