Jumanne, 14 Desemba 2021

JAJI SIYANI AAPISHWA KUWA MJUMBE WA TUME

 Na Lydia Churi-Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo amemuapisha Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani kuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama

Kufuatia Uapisho huo, Jaji Siyani anakuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama kwa mujibu wa kifungu cha 46 (2)(a) cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika leo katika ukumbi wa Ofisi ndogo ya Bunge jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume hiyo amesema baadhi ya kazi muhimu za Tume hiyo ni pamoja na kushughulikia ajira, maslahi na nidhamu ya Watumishi Mahakama ya Tanzania.

Alisema wananchi wanayo nafasi ya kuwasilisha malalamiko yao yanayotokana na huduma za Mahakama kupitia Kamati za Maadili ambazo zimesambaa mpaka ngazi ya wilaya.

“Mahakama haitafunga mlango wa kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kwa kuwa kuletwa kwa malalamiko hayo kunaipa nafasi Mahakama ya kujua kinachoendelea”, alisema Jaji Mkuu.

Akizungumza baada ya kuapishwa, Jaji Kiongozi alisema katika kutekeleza majukumu yake kama mjumbe wa Tume hiyo atakiishi kiapo chake kinachomtaka kujiweka kanda na mambo yatakayozuia kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Aliyataja mambo mengine atakayoyasimamia ili Tume ya Utumishi wa Mahakama ifikie malengo yake kuwa ni pamoja na kutunza siri, kutofikia uamuzi unaotokana na shinikizo litakalotokana na uoga, huba au upendeleo, na kutokusumwa na nia mbaya katika kutoa maamuzi yoyote.  

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amesema Watumishi wa Mahakama wanapokuwa na maadili mazuri husaidia kuufanya Mhimili wa Mahakama kuwa na taswira chanya kwa jamii.

“Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama wanaolalamikiwa kwa vitendo vya rushwa wakipungua itasaidia maamuzi na kazi za Mahakama kuaminika zaidi na hivyo Mhimili huo kuwa kimbilio la wengi”, alisema.

Alisema hivi sasa maadili ya kwa Maafisa wa Mahakama yameimarika na yanaendelea kuimarika kwa kuwa wapo vijana wengi watumishi ambao wanafanya kazi zao vizuri na kwa uadilifu mkubwa.

Aidha, Jaji Feleshi alimpongeza Mhe. Siyani kwa kuteuliwa kuwa Jaji Kiongozi na kuapishwa kuwa Mjumbe wa Tume ambapo pia alimshauri kuendelea kuangalia maslahi mapana ya Tume hiyo, Mahakama ya Tanzania na Serikali kwa ujumla.

Tume ya Utumishi wa Mahakama imeundwa kwa mujibu wa Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011. Tume hii iliundwa kwa lengo la kusimamia mambo muhimu yanayohusu Mhimili wa Mahakama.

Baadhi ya kazi za Tume hiyo ni pamoja na kumshauri Mhe. Rais katika uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu, kumshauri Rais kuhusu masuala ya nidhamu, mishahara na maslahi ya Majaji, kushauri kuhusu ajira za Mahakimu na kusimamia nidhamu yao.

Wajumbe wa Tume hiyo ni pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania (Mwenyekiti), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji moja wa Mahakama ya Rufani anayeteuliwa na Rais, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, na wajumbe wengine wawili wanaoteuliwa na Rais.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani akiapa mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 14 Desemba, 2021 kuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama. 

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani akisaini hati ya kiapo mara baada ya kuapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 14 Desemba, 2021 kuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama. Anayeshuhudia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel ambaye pia ni Katibu wa Tume hiyo.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis akimkabidhi hati ya kiapoJaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani mara baada ya kumuapisha kuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama. 

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis akisaini hati ya kiapo.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis akizungumza wakati wa hafla hiyo. 

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani akizungumza wakati wa hafla hiyo. 


Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye pia ni mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akizungumza wakati wa hafla hiyo. 

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama. 

(PICHA NA INNOCENT KANSHA-MAHAKAMA)


















 

     

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni