Na Innocent Kansha – Mahakama.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewakumbusha Watendaji wote wa Mahakama nchini kutambua dhamana kubwa waliyonayo katika kujenga kwa weledi, uadilifu na kujiamini na kusimamia shughuli za kiutendaji kwenye maeneo yao ya kazi na kuhakikisha Taasisi inabaki kuwa imara na mfano wa kuigwa.
Akizungumza
katika kikao kazi cha Watendaji wa Mahakama wa ngazi mbalimbali wapatao 44,
pamoja na baadhi ya viongozi waandamizi kutoka Makao Makuu walioshiriki kwenye kikao hicho kilichoendeshwa kwa njia ya Mkutano
Mtandao “Video Conference” leo tarehe
20 Desemba 2021 ofisini kwake Jijini Dar es Salaam, Prof. Ole Gabriel alisema
kusimamia na kufuatilia kazi za Taasisi za kila siku ni jukumu lao la msingi kwa
ngazi ya mikoa na wilaya, kwani ndiko waliko wateja wengi wanaohudumiwa na
Mahakama.
“Tujitume
kwa asilimia 100, tufanye kazi kwa uwazi, uwajibikaji na tuoneshe ufanisi
mkubwa katika utendaji wetu. Tutoe uamuzi kwa wakati hasa kwenye mambo yote
yaliyo ndani ya uwezo wetu na tuepuke utamaduni wa kulalamika,” alisema Mtendaji Mkuu huyo wa Mahakama ya Tanzania.
Prof.
Ole Gabriel aliwasisitiza Watendaji kusimamia shughuli za Mahakama hasa upande
wa miradi ya ujenzi iliyopo kwenye maeneo yao ya kiutawala ambapo aliwaasa kujua
miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao, huku akibainisha kutokuridhishwa na kasi ndogo na
usimamizi dhaifu wa miradi ya ujenzi na hivyo kuwataka kutambua kila jambo linalofanywa na kujua ni sehemu yao ya utendaji kazi.
Aidha,
Mtendaji Mkuu huyo alisema kuwa Watendaji ni watu muhimu katika kusimamia uboreshaji mkubwa unaofanywa na Mahakama ya Tanzania, hivyo kuwataka kuchukua changamoto ndogo ndogo zilizopo
katika maeneo yao, kuzigatia fursa na kuzitatua kwa ubunifu uliotukuka huku wakiongozwa
na fikra chanya.
Kwa
upande wa matumizi ya Ofisi Mtandao “e –
Office Management System” Prof. Ole Gabriel amewataka Watendaji kujielekeza
zaidi katika matumizi hayo ili kuondokana na matumizi ya ripoti na barua
za watumishi kwa njia ya nakala ngumu, kwani Mahakama sasa hivi inaelekea
kwenye mapinduzi ya kuepuka matumizi ya karatasi katika shughuli mbalimbali za
kutendaji, hatua ambayo itasaidia usimamizi na ufuatiliaji wa haraka.
Akizungumzia
suala la manunuzi, Mtendaji Mkuu huyo alisema kuwa Mahakama ya Tanzania inashughulikia mchakato
wa kuanzisha bodi za manunuzi ili kugatua madaraka na taratibu za manunuzi ili zianze kufanyika kwenye ngazi za mikoa badala ya Makao Makuu na kusema kuwa hatua hiyo
itapunguza ucheleweshaji wa taratibu hizo na kuongeza ufanisi katika kazi.
Aliongeza
kuwa watendaji wanapaswa kuboresha taarifa kwenye mfumo wa ramani unaonesha
maeneo mbalimbali ya kijiografia ya Mahakama “Judiciary Mapping”, ili kutoa
mwanya wa kuonesha uboreshaji unaoendelea kufanyika ndani ya Mhimili huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni