Jumamosi, 4 Desemba 2021

WATUMIENI WANACHAMA WA TAALUMA MBALIMBALI KUENDANA NA MABADILIKO YA KITAASISI – NYIMBI

Na Innocent Kansha – Mahakama.

Mtendaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Bw. Solanus Meinrad Nyimbi amewaasa viongozi wa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Mahakama ya Tanzania (Mahakama Saccos) kutumia ujuzi wa wataalam wa fani mbalimbali ambao ni wanachama wa Saccos waliopo ili kuboresha shughuli za chama ziendane na mabadiliko ya Kitaasisi, kwa kutambua Mahakama ya Tanzania inaendelea na mageuzi makubwa ya kimifumo kuendana na karne ya 21.

Akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa  Mahakama Saccos leo tarehe 4 Desemba, 2021, katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Jijini Dar es salaam kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Bw. Nyimbi alisema viongozi  wanapaswa kutumia fursa ya kila kunapotokea mafunzo ya waajiriwa wapya wa Mahakama kuwashawishi kujiunga na chama ili kuongeza idadi ya wanachama kwani ndio njia bora ya kuimarisha Saccos hiyo.

“Nafahamu kuwa Chama hiki kina umri wa miaka 51 tangu kupata usajili wake mwaka 1970, hivyo nawapongeza kwa kudumu muda wote licha ya changamoto zinazoendelea kujitokeza. Kudumu kwa chama kunatokana na aina ya viongozi wanaochaguliwa, kuaminiana kati ya wanachama wenyewe na misaada halikadhalika faida ya mikopo mbalimbali inayotolewa na Saccos kwa wanachama wake”, alifafanua Mtendaji Nyimbi.

Akiongelea suala la kushawishi wanachama wapya kujiunga na Mahakama Saccos, Mtendaji Nyimbi alisema, "niwahakikishie kumfikishia salamu Jaji Mkuu kuhusu kuwashawishi Majaji na Viongozi wengine waandamizi wa muhimili kujiunga katika umoja huo ili iwe chachu kwa watumishi wengine wa ngazi mbalimbali."

Aidha, Mtendaji huyo aliwaasa viongozi kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kuzingatia sheria za nchi kwa maana kama wakiaminiwa na wao wanatakiwa waaminike. Alisema kuwa utendaji wa shughuli za chama uendane na mabadiliko hasa mageuzi ya mfumo wa TEHAMA ili kutobaki nyuma na kuleta ufanisi kwenye huduma.

Aliongeza kuwa wanachama wanaoomba mikopo wahakikishe wanachukua kwa malengo mahususi hasa kuwekeza kwenye shughuli za kiuchumi, huku akikitaka Chama kuangalia uwezekano wa kuwekeza kwenye miradi ya uzalishaji mali ili kuongeza mtaji.

Kwa upande mwingine, Mtendaji Nyimbi aliwatia shime Viongozi na wanachama kuendelea kutoa hamasa kwa watumishi wasio wanachama ili wajiunge katika kujiimarisha kiuchumi kupitia utaratibu wa kujiwekea akiba.

Wakati huo huo, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mahakama Saccos, Bi. Stephania Bishobe, akisoma hotuba yake kwa Mgeni rasmi alisema lengo la umoja huo wa Saccos ni kuinuana watumishi kiuchumi, hivyo basi huduma mama inayotolewa kwa wanachama ni mikopo ya aina mbalimbali ikiwemo, mkopo wa maendeleo, wa dharula, sikukuu, mkopo wa viwanja na pia mkopo wa kuanzia maisha kwa mwanachama wa ajira mpya.

Makamu Mwenyekiti huyo alisema kuwa licha ya kupata mafanikio ndani ya mwaka 2021, pia Chama kinachangamato kadhaa ambazo ni pamoja na uchache wa wanachama ukilinganisha na idadi ya watumishi. Kwa sasa chama kina idadi ya asilimia sita kati ya watumishi wote wapatao 5,800. Ukosefu wa ofisi ya kutosha kutekeleza majukumu ya chama na Mahakama Saccos kuonekana kama sio sehemu ya Mahakama.

Aidha, Bi. Bishobe akataja marajio ya chama kwa mwaka 2022 kuwa ni kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa uendeshaji wa shughuli za za chama, kufanya utafiti na kuona uwezekanao wa kupunguza riba ya mkopo kuwa chini ya asilimia 10, kutoa gawio la faida kwa wanachama kwa mujibu wa sera na sheria na kuendelea kuongeza hisa za wanachama.

Ushirika huu wa akiba na mikopo Mahakama ulianzishwa miaka 51 iliyopita na kusajiliwa tarehe 1 Agosti, 1970 kwa jina la Chama cha Ushirika  wa Akiba na Mikopo Mahakama ya Tanzania (Mahakama Savings and Credit Cooperative Society Limited). Hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2021 Chama kina jumla ya wanachama 425, sawa na asilimia sita ya watumishi 5,800 wa Mahakama.

   

Mtendaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Bw. Solanus Meinrad Nyimbi akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha ushirika cha akiba na mikopo cha Mahakama ya Tanzania (Mahakama Saccos) leo tarehe 4 Desemba, 2021, kwa niamba ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Dar es salaam mbele ya wajumbe wa mkutano huo (hawapo pichani), Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mahakama Saccos Bi. Stephania Bishobe na  kushoto ni Afisa Ushirika Jiji la Dar es salaam Bw. Abdulihakimu Haidar.


Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mahakama Saccos Bi. Stephania Bishobe (katikati) akisoma hotuba yake kwa Mgeni rasmi na wanachama (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa kikao cha mkutano mkuu wa mwaka wa Mahakama Sccos, Kulia ni Mtendaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Bw. Solanus Meinrad Nyimbi na kushoto ni Afisa Ushirika Jiji la Dar es salaam Bw. Abdulihakimu Haidar.
 
Baadhi ya wanachama wa Chama cha ushirika cha akiba na mikopo cha Mahakama ya Tanzania (Mahakama Saccos) wakishiriki kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka 2021


Miongoni mwa Wajumbe wakilishi kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania bara na  wanachama wa Chama cha ushirika cha akiba na mikopo cha Mahakama ya Tanzania (Mahakama Saccos) wakishiriki kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka 2021.

Baadhi ya wanachama wa Chama cha ushirika cha akiba na mikopo cha Mahakama ya Tanzania (Mahakama Saccos) wakishiriki kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka 2021

(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni