Na Innocent Kansha, Mahakama - Dodoma.
Serikali ya Mkoa wa Dodoma imewaalika wananchi wote kuhudhuria kwa wingi
kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria yatakayo kufanyika siku ya Jumatano tarehe
2 Februari, 2022, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Akihitimisha maadhimisho wa Wiki ya Sheria yaliyoambatana na maonyesho
ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania na wadau wake wote
katika mnyororo wa utoaji haki nchini katika viwanja vya Nyerere Square, Mkuu
wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabir Shekimweri amewaomba wananchi kujiandaa
kikamilifu kwa ajili ya siku hiyo muhimu ambayo huashiria kuanza rasmi kwa
shughuli za kimahakama kote nchini.
“Niwahimize wananchi wote tujitokeze kwa wingi siku ya uzinduzi wa
shughuli za Mahakama tarehe (2) Februari, 2022 siku ya (Jumatano). Tujiandae,
tutakuwa na kiongozi wetu, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, kama mgeni rasmi.
Tuhamasishane kila mmoja na kila mdau kwenye tasnia hii ya sheria kujitokeza
kwa wingi siku hiyo,” amesema Mhe. Shekimweri aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma, Mhe. Antony Mtaka kwenye hafla hiyo fupi.
Ameupongeza Mhimili wa Mahakama chini ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof.
Ibrahim Hamis Juma kwa kuandaa maadhimisho hayo kwa mafanikio makubwa ambayo
yalishirikisha madanda 46 yanayojumuisha saba ya Mahakama na mengine 39
yaliyobaki ya wadau wengine mbalimbali.
“Tumefuatilia tangu mwanzo kwenye uzinduzi uliofanywa na Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe, Dkt Hussein Mwinyi na pia
kwa maadamano ambayo yalifana sana. Naamini maudhui kwenye hotuba nzuri
aliyoitoa mgeni rasmi na Jaji Mkuu mtayabeba, kuyaenzi na kuyafanyia kazi,”
amesema.
Amewapongeza washiriki wote walioandaa maelezo, vifurushi na majarida
mbalimbali kwa ajili ya wananchi ili kuweza kupata rejea ya masuala kadhaa
ambayo wanayafanyia kazi na zaidi ya hapo kupata muda wa kuongea na wadau
kwenye mabanda yao na kuwaelimisha masuala mbalimbali na baadhi yao kutatua
changamoto za wananchi.
“Mmefanya kazi kubwa na kutukuka ya kupigiwa mfano kwenye Makao Makuu ya
nchi, hivyo tunategemea kuona jamii yenye ustaarabu na ustaarabu unapatikana
watu wakifuata sheria, kanuni na taratibu. Kazi hiyo mmeifanya vizuri katika
wiki hii ya maonesho,” Mhe. Shekimweri.
Halikadhalika, Mkuu wa Wilaya huyo amewapongeza wananchi waliojitokeza
kwa wingi kwenye maonesho hayo, hivyo akawaomba kuzigantia yale yote waliyojifunza
kwa sababu kupata maarifa ni kitu kingine na kuyatumia katika usahihi wake ni
kitu kingine. Anaamini wananchi wakifanya hivyo migogoro mingi na malalamiko
mengi yataondoka na kufa kifo cha Mende.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni