Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma
Jumla ya Watumishi 120 wa Mahakama ya Tanzania kutoka Makao Makuu Dar es Salaam wamefanya ziara ya kutembelea na kujionea Mradi wa Ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama unaojengwa katika eneo la Tambuka Reli jijini Dodoma ambapo wameonyesha kufurahishwa na ujenzi wa majengo hayo yanayotarajiwa kukamilika mwisho wa mwaka huu.
Akizungumza na Watumishi hao waliotembelea Mradi huo tarehe 29 Januari, 2022, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi aliwaambia Watumishi hao kujiandaa kisaikolojia kwakuwa wapo mbioni kuhamia Dodoma.
“Ifikapo mwezi wa 12 mwaka huu ninyi wote mtakuwa mmehamia katika jengo hili, kwahiyo ni vizuri mkajiandaa kisaikolojia na kufanya maandalizi mengine ya msingi, kwa mfano najua wengine wana Watoto ambao wanaenda shule, wengine wana wenza wa kuwaweka sawa kisaikolojia, lakini la msingi la Mtendaji Mkuu kuwapa fursa kuja kuona ni ili mpate picha ya sehemu mtakayokuja kufanya kazi,” alisema Bw. Nyimbi.
Aliongeza kuwa Watumishi wote wa Makao Makuu, Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu Masjala kuu wote wanatakiwa kuhamia katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama-Dodoma ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.
Akizungumza kwa niaba ya Watumishi, Afisa Utumishi wa Mahakama, Bw. Nkrumah Katagira ameshukuru Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole kwa kuwapa fursa ya kutembelea jengo hilo la Makao Makuu na kuongeza kuwa wamefurahi sana kupewa nafasi hiyo.
“Kwa niaba ya Watumishi wenzangu, nimshukuru sana Mtendaji wa Mahakama ya Rufani kwa niaba ya Mtendaji Mkuu, Watumishi kwakweli wamefurahi sana kwa hii safari, kwa sababu ni sehemu ya kujiandaa kisaikolojia kujua wapi tutakuja kukaa na hii imepunguza wasiwasi kwetu baada ya kuona sehemu ambayo tutakuja kufanyia kazi,” alisema Bw. Katagira.
Pamoja na kutembelea Mradi wa ujenzi wa Makao Makuu, Watumishi hao pia walitembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Dodoma (IJC) na kutembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria katika Viwanja vya Nyerere ‘square’ Dodoma.
Safari hii imejumuisha Watumishi wa Kada za Wasaidizi wa Kumbukumbu, Wasaidizi wa Ofisi, Wasaidizi wa Maktaba, Makatibu Mahsusi, Walinzi, Madereva wakiongozwa na Maafisa Utumishi.
Makatibu Mahsusi wakiwa katika picha ya pamoja eneo la Mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama walipotembelea leo tar 29.01.2022.
Wasaidizi wa Ofisi wakiwa katika picha ya pamoja eneo la Mradi wa ujenzi wa Majengo ya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania walipotembelea leo tarehe 29 Januari, 2022.
Wasaidizi wa Kumbukumbu wakiwa katika picha ya pamoja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni