Na Faustine Kapama, Mahakama
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amewataka Mahakimu
kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu mkubwa, hivyo kuijenga Mahakama
inayoaminika na isiyo na doa la rushwa.
Mhe.
Siyani ametoa wito huo leo tarehe 17 January, 2022 katika hafla ya kuwaapisha
Mahakimu Wakazi wapya 29 katika ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Temeke
mkoani Dar es Salaam. Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na maafisa mbalimbali, Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alikuwa mgeni rasmi.
Akizungumza
baada ya uapisho huo, Jaji Kiongozi aliwaambia Mahakimu hao kuwa kazi
waliyoiomba inahitaji uadilifu wa hali ya juu, huku akiamini kuwa kila mmoja
wao ni muumini wa dini fulani ambapo dini zote hapa nchini zinahubiri suala
hilo la uadilifu.
Aliwapitisha
kwenye Bibilia, Kumbukumbu la Torati 1:16-17 na Sura ya 4 ya Quran, Aya ya 135
na kusema, “ukiwa Mkristo au Mwislam, vyovyote itakavyokuwa, ili ufanye kazi ya
uhakimu unahitaji kuwa mwadilifu. Usipokuwa mwadilifu basi utakuwa umekosea
kuwa mahali hapa na hautadumu.”
Ili
kuonesha umuhimu wa uadilifu kwa kazi ya uhakimu, Mhe. Siyani alimnukuu
mwanazuoni mmoja kutoka Nigeria ambaye aliwahi kusema, “Afisa wa Mahakama asiye
mwadilifu ana madhara makubwa kwa jamii kuliko mtu anayekimbia hovyo katikati
ya mtaa uliofurika umati wa watu akiwa na upanga mkononi.
“Kwa kuwa
wakati mtu huyo anaweza kuthibitiwa kwa nguvu, Afisa wa Mahakama asiye
mwadilifu kwa makusudi huharibu msingi wa maadili ya jamii aliyomo na kuleta
madhara yasiyoweza kutatuliwa kwa wananchi kwa matumizi mabaya ya madaraka ya
ofisi yake na wakati huo huo akiitwa Mheshimiwa.”
Hivyo,
Jaji Kiongozi aliwaomba Mahakimu kutambua ukubwa na thamani ya kazi ambayo
Taifa limewapa na kuwataka kwenda kuchapa kazi kwa uadilifu na kuijenga Mahakama
inayoaminika na isiyo na doa la rushwa.
Aidha,
Mhe. Siyani aliishukuru Tume ya Utumishi wa Mahakama na Serikali kwa ujumla kwa
kuendelea kuajili watumishi mbalimbali, wakiwemo Mahakimu walioapishwa.
Alibainisha
kuwa bado kuna upungufu mkubwa wa watumishi, hivyo ni imani yake Mahakimu hao
watasaidia kupunguza upungufu uliopo. Jaji Kiongozi aliwapongeza Mahakimu wote waliokula
kiapo na kuwakaribisha katika familia ya Mahakama ya Tanzania.
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akitoa nasaa kwa Mahakimu
Wakazi wapya 29 (hawapo pichani) walioapishwa leo tarehe 17 Januari, 2022.
Baadhi
ya Mahakimu Wakazi wapya 29 walioapishwa wakimsikiliza Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (hayupo kwenye picha) wakati akizungumza
katika hafla ya Uapisho huo.
Meza
Kuu wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mahakimu Wakazi wapya mara baada
ya kula kiapo (picha ya juu na chini). Waliokaa katikati niJaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma, kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani
na kuliani Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki -Temeke, Mhe. Ilvin Mugeta.
Mmoja
kati ya Mahakimu Wakazi 29 (picha ya juu na chini) wakila kiapo mbele ya Jaji Mkuu
wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma wakati wa hafla ya uapisho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni