Ijumaa, 14 Januari 2022

RAIS SAMIA MGENI RASMI KILELE CHA SIKU YA SHERIA

 Na Magreth Kinabo- Mahakama

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha Siku ya Sheria nchini itakayofanyika tarehe 01 Februari, 2022 katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 14 Januari, 2022 kwenye ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Temeke Dar es Salaam, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alisema siku hii ya sheria nchini huadhimishwa kila mwaka kuashiria kuanza rasmi kwa shughuli za kimahakama kwa mwaka husika.

‘‘Siku hii itatanguliwa na Maadhimisho ya Wiki ya Sheria, yatakayoanza tarehe 23 Januari hadi tarehe 29 Januari, mwaka huu ambayo yatazinduliwa kwa Matembezi maalum yatakayofanyika tarehe 23 Januari, mwaka huu kuanzia saa 12.00 asubuhi,” alisema Mhe. Prof. Juma.

Alisema kuwa matembezi hayo yataanzia Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Dodoma katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki na yataishia kwenye viwanja vya Nyerere ‘Square’.

Jaji Mkuu aliongeza kuwa mgeni rasmi katika matembezi hayo, anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt.  Hussein Mwinyi.

Alibainisha kuwa kaulimbiu ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria kwa mwaka huu ni ‘Zama za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda: Safari ya Maboresho Kuelekea Mahakama Mahakama Mtandao’.

Mhe. Prof. Juma aliongeza kuwa kaulimbiu hiyo ya mwaka huu inawatayarisha Watanzania, wadau wote wa Mahakama na sekta ya Sheria waelewe kuwa Mahakama ya Tanzania na mfumo mzima wa utoaji haki unaelekea sio tu kwa matumizi ya teknolojia bali pia kuvuna faida kutoka katika uwekezaji mkubwa uliofanyika kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Aliwaomba wananchi kufika katika viwanja vya Nyerere ‘Square’ ili kuweza kupata elimu kuhusu sheria na taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri, ndoa na talaka, utekelezaji wa hukumu, Sheria za Watoto, taratibu za mashauri ya mirathi, msaada wa kisheria na ushughulikiaji wa malalamiko mbalimbali.

Mhe. Prof. Juma alisema elimu hiyo itatolewa na Majaji, Mahakimu, Wasajili, Watendaji wa Mahakama, Watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo wadau wa Mahakama, ambao ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) na wengine.

 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo katika picha) alipofanya mkutano na Wanahabari hao kuzungumzia Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na kilele cha Siku ya Sheria nchini. Mkutano huo umefanyika leo tarehe 14.01.2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Kanda ya Temeke.


Waandishi wa Habari pamoja na baadhi ya Maafisa wa Mahakama wakimsikiliza Mhe. Jaji Mkuu (hayupo katika picha) alipokuwa akizungumza katika Mkutano uliofanyika leo tarehe 14.01.2022.


Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (aliyesimama) akizungumza jambo wakati wa Mkutano huo.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza jambo na Waandishi wa Habari wakati wa Mkutano huo.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni