Na Mary Gwera, Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo
tarehe 13 Januari 2022 amewakabidhi nyenzo za kazi jumla ya Mahakimu Wakazi
Wafawidhi wapya 10 baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni.
Akizungumza na Mahakimu hao baada ya kuwaapisha katika
Ukumbi wa Mahakama ya Rufani (T) jijini Dar es Salaam, Mhe. Prof. Juma aliwapongeza
kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo huku akiwaasa kuwa wanyenyekevu katika
utendaji wao wa kazi.
“Unapokuwa kiongozi katika chombo cha utoaji haki
unatakiwa kuwa mnyenyekevu kwa kila mtu unayemhudumia kwakuwa sio wananchi wote
wanaofahamu haki zao, hivyo inabidi kuwaelimisha,” alisema Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kwa kuwataka Mahakimu
hao kuwa na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuendana na kasi ya matumizi
ya TEHAMA ambayo Mahakama inatekeleza katika kufanikisha azma ya kuwa na
Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’.
Mhe. Prof. Juma alisema, “Nafasi yenu kama viongozi mnatakiwa
kuwa na ufanisi ili kuendana na zama za mapinduzi ya nne ya viwanda, muwe
karibu sana na Maafisa TEHAMA mnapokwama ili kuwawezesha kwenda sambamba na kasi
ya utandawazi.”
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma aliwakumbusha
Maafisa hao wa Mahakama kuhusu matumizi ya adhabu mbadala ili kupunguza mlundikano
wa wafungwa gerezani.
Naye, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Mustapher Siyani aliwataka Mahakimu Wafawidhi hao kutatua kero na malalamiko
mbalimbali yanayochafua taswira ya Mahakama, ikiwemo mlundikano wa mashauri ya muda
mrefu, lugha mbaya, kutowajibika kwa baadhi ya Watumishi wa Mahakama, upatikanaji
wa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri pamoja na rushwa.
“Nyenzo za kazi mlizokabidhiwa leo zinawatofautisha na
Mahakimu wengine, hivyo nendeni mkatatue kero na malalamiko ya wananchi, kero
hizi zitawasilishwa kwa njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii ‘facebook’,
‘instagram’, ‘twitter’ na kadhalika na hata kama malalamiko yanayotolewa hayatahusu
kituo chako, saidia katika kutatua kwa kuwa sote tunajenga nyumba moja,”
alisema Mhe. Siyani.
Jaji Kiongozi aliongeza kwa kutoa rai kwa Maafisa hao
wa Mahakama kuwa waadilifu na kuwakumbusha kuwa na ushirikiano na Wadau wa
Mahakama pamoja na Viongozi wa Serikali ili kupiga hatua katika uboreshaji wa
huduma za Mahakama na Taifa kwa ujumla.
Mahakimu Wakazi Wafawidhi waliokabidhiwa nyenzo za
kazi ni wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara, Musoma-Mara, Moshi-Kilimanjaro,
Sumbawanga-Rukwa, Katavi, Morogoro, Kigoma, Singida, Arusha na Tanga.
Baada ya hafla hiyo, Jaji Kiongozi aliwakabidhi Mahakimu Wakazi Wafawidhi hao kila mmoja kadi maalumu kama ishara ya kuwapongeza kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na kukabidhiwa nyenzo zitakazowaongoza katika utendaji wao wa kazi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisisitiza jambo alipokuwa akiongea na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wapya 10 (hawapo kwenye picha) mara baada ya kuwakabidhi nyenzo mbalimbali katika hafla iliyofanyika leo tarehe 13 Januari, 2022 katika ukumbi wa Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakichukua kumbukumbu wakati Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipokuwa akiongea na Mahakimu Wakazi Wafawidhi hao (hawapo katika picha) mara baada ya kukabidhiwa nyenzo za kufanyia kazi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyekaa katikati) akiwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kushoto) na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Edwin Kakolaki katika picha ya pamoja na Mahakimu Wakazi Wafawidhi (waliosimama) mara baada ya kuwakabidhi vitendea kazi mbalimbali.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyekaa katikati) akiwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kushoto) na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Edwin Kakolaki katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Mahakama waliohudhuria hafla ya kuwakabidhi Mahakimu Wakazi Wafawidhi vitendea kazi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akiwakabidhi baadhi ya ya Mahakimu Wakazi Wafawidhi (picha ya juu na chini) kadi maalumu kama ishara ya kuwapongeza kwa kuchaguliwa kushika wadhifa huo.
Nawapongeza Sana Wahe. Mahakimu Wakazi wafawidhi. Mungu awaongoze kwenye majukumu yenu mapya. Na awajaze Hekima na busara.
JibuFuta