Alhamisi, 13 Januari 2022

MAHAKIMU WAKAZI WAFAWIDHI WAPYA WAPATIWA NYENZO ZA KAZI

Na Mary Gwera, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 13 Januari 2022 amewakabidhi nyenzo za kazi jumla ya Mahakimu Wakazi Wafawidhi wapya 10 baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni.

Akizungumza na Mahakimu hao baada ya kuwaapisha katika Ukumbi wa Mahakama ya Rufani (T) jijini Dar es Salaam, Mhe. Prof. Juma aliwapongeza kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo huku akiwaasa kuwa wanyenyekevu katika utendaji wao wa kazi.

“Unapokuwa kiongozi katika chombo cha utoaji haki unatakiwa kuwa mnyenyekevu kwa kila mtu unayemhudumia kwakuwa sio wananchi wote wanaofahamu haki zao, hivyo inabidi kuwaelimisha,” alisema Jaji Mkuu.

Aidha, Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kwa kuwataka Mahakimu hao kuwa na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuendana na kasi ya matumizi ya TEHAMA ambayo Mahakama inatekeleza katika kufanikisha azma ya kuwa na Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’.

Mhe. Prof. Juma alisema, “Nafasi yenu kama viongozi mnatakiwa kuwa na ufanisi ili kuendana na zama za mapinduzi ya nne ya viwanda, muwe karibu sana na Maafisa TEHAMA mnapokwama ili kuwawezesha kwenda sambamba na kasi ya utandawazi.”

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma aliwakumbusha Maafisa hao wa Mahakama kuhusu matumizi ya adhabu mbadala ili kupunguza mlundikano wa wafungwa gerezani.

Naye, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani aliwataka Mahakimu Wafawidhi hao kutatua kero na malalamiko mbalimbali yanayochafua taswira ya Mahakama, ikiwemo mlundikano wa mashauri ya muda mrefu, lugha mbaya, kutowajibika kwa baadhi ya Watumishi wa Mahakama, upatikanaji wa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri pamoja na rushwa.

“Nyenzo za kazi mlizokabidhiwa leo zinawatofautisha na Mahakimu wengine, hivyo nendeni mkatatue kero na malalamiko ya wananchi, kero hizi zitawasilishwa kwa njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii ‘facebook’, ‘instagram’, ‘twitter’ na kadhalika na hata kama malalamiko yanayotolewa hayatahusu kituo chako, saidia katika kutatua kwa kuwa sote tunajenga nyumba moja,” alisema Mhe. Siyani.

Jaji Kiongozi aliongeza kwa kutoa rai kwa Maafisa hao wa Mahakama kuwa waadilifu na kuwakumbusha kuwa na ushirikiano na Wadau wa Mahakama pamoja na Viongozi wa Serikali ili kupiga hatua katika uboreshaji wa huduma za Mahakama na Taifa kwa ujumla.

Mahakimu Wakazi Wafawidhi waliokabidhiwa nyenzo za kazi ni wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara, Musoma-Mara, Moshi-Kilimanjaro, Sumbawanga-Rukwa, Katavi, Morogoro, Kigoma, Singida, Arusha na Tanga.

Baada ya hafla hiyo, Jaji Kiongozi aliwakabidhi Mahakimu Wakazi Wafawidhi hao kila mmoja kadi maalumu kama ishara ya kuwapongeza kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na kukabidhiwa nyenzo zitakazowaongoza katika utendaji wao wa kazi.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisisitiza jambo alipokuwa akiongea na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wapya 10 (hawapo kwenye picha) mara baada ya kuwakabidhi nyenzo mbalimbali katika hafla iliyofanyika leo tarehe 13 Januari, 2022 katika ukumbi wa Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam. 


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwakabishi baadhi ya  Mahakimu Wakazi Wafawidhi (picha ya juu na chini) nyenzo mbalimbali za kufanyia kazi.


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akitoa nasaha fupi kwa Mahakimu Wakazi Wafawidhi hao mara baada ya kukabishiwa nyenzo mbalimbali za kufanyia kazi na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akifafanua jambo wakati akitoa taarifa fupi kuhusu hafla ya kuwakabidhi nyenzo mbalimbali za kufanyia kazi kwa Mahakimu Wakazi Wafawidhi hao (hawapo katika picha).

Baadhi ya viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakichukua kumbukumbu wakati Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipokuwa akiongea na Mahakimu Wakazi Wafawidhi hao (hawapo katika picha) mara baada ya kukabidhiwa nyenzo za kufanyia kazi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyekaa katikati) akiwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kushoto) na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Edwin Kakolaki katika picha ya pamoja na Mahakimu Wakazi Wafawidhi (waliosimama) mara baada ya kuwakabidhi vitendea kazi mbalimbali.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyekaa katikati) akiwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kushoto) na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Edwin Kakolaki katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Mahakama waliohudhuria hafla ya kuwakabidhi Mahakimu Wakazi Wafawidhi vitendea kazi.


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akiwakabidhi baadhi ya ya  Mahakimu Wakazi Wafawidhi (picha ya juu na chini) kadi maalumu kama ishara ya kuwapongeza kwa kuchaguliwa kushika wadhifa huo.

(Picha na Faustine Kapama, Mahakama)

Maoni 1 :

  1. Nawapongeza Sana Wahe. Mahakimu Wakazi wafawidhi. Mungu awaongoze kwenye majukumu yenu mapya. Na awajaze Hekima na busara.

    JibuFuta