Jumanne, 11 Januari 2022

MAHAKAMA KUPUNGUZA MLUNDIKANO WA MASHAURI KUPITIA MAHAKAMA ZINAZOTEMBEA

 Na Waandishi Wetu-Dodoma

Mahakama ya Tanzania inao mpango wa kutumia Mahema kusikiliza mashauri na kuongeza idadi ya Mahakama zinazotembea (Mobile Court) ili kuongeza ufanisi na kasi ya kusikiliza mashauri mahakamani.

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 11 Januari, 2022 na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof.  Elisante Ole Gabriel wakati akizungumza na Viongozi wa Mahakama wakiwemo Watendaji, Wasajili na Maafisa Bajeti kutoka kanda na mikoa yote nchini kwenye mkutano wa kutathimini utekelezaji wa bajeti.

Alisema Mahakama ya Tanzania inatarajia kuongeza magari sita ya Mahakama zinazotembea (Mobile Courts) na kuyasambaza maeneo mengine mbali na mikoa ya Dar es salaam na Mwanza ambapo huduma hiyo inapatikana hivi sasa, lengo ni kusogeza huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi.

Prof. Ole Gabriel alisema sanjari na hilo, Mahakama inatarajia kuanzisha huduma ya kimashauri kupitia ujenzi wa Mahema katika maeneo ambayo yana msongamano na hakuna huduma za kimahakama. Alisema lengo ni kuhakikisha wananchi wengi wanapata huduma ya kusikilizwa kwa mashauri katika mazingira ambayo yako karibu na wanapoishi.

Kwa upande wake, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma amewataka Mahakimu kutumia njia na namna bora ya kuondoa mrundikano wa mashauri ya muda mrefu ili Mahakama isiwe sehemu ya ucheleweshaji wa utoaji wa haki kwa wananchi.

Alisema kumalizika kwa mashauri mapema mahakamani kutasaidia kuongeza imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama. Aidha, Msajili Mkuu aliwataka Viongozi hao kuongeza kasi kwenye matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kupunguza mrundikano wa mashauri mahakamani.

Mhe. Chuma aliwataka viongozi hao kuongeza matumizi ya mikutano Mtandao (video conference) katika kusikiliza mashauri, jambo litakalowawezesha Majaji na Mahakimu kusikiliza idadi kubwa ya mashauri kwa muda mfupi.

Sehemu ya Watendaji, Naibu Wasajili na Maafisa Bajeti kutoka mikoa yote nchini wakiwa kwenye kikao cha kupitia bajeti ya Mahakama leo mjini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa rai kwa Watendaji, Naibu Wasajili na Maafisa Bajeti kutoka Mahakama za mikoa mbalimbali hapa nchini walipokuwa katika kikao cha kupitia bajeti leo mjini Dodoma.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati waliokaa), Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma( kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Mahakama wa Kanda na mikoa baada ya kufunguliwa mkutano wa Naibu Wasajili wa Kanda, Watendaji  na Maafisa Bajeti kutoka Mahakama za mwao. 
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati waliokaa) na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma ( kushoto waliokaa) akiwa kaika picha ya pamoja na Naibu Wasajili kutoka kwenye     Kanda mbalimbai nchini .

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma akitoa rai kwa Watendaji, Wasajili na Maafisa Bajeti kutoka Mahakama za mikoa mbalimbali hapa nchini walipokuwa katika kikao cha kupitia bajeti leo mjini Dodoma.
Maoni 1 :

  1. Kazi nzuri, hongera mtendajimkuu wa mahakama professor Elisante Ole Gabriel

    JibuFuta