Jumanne, 11 Januari 2022

JAJI MKUU ASHAURI MATUMIZI YA TEHAMA KUONGEZA KASI YA UTENDAJI KAZI

 Na Lydia Churi- Mahakama, Dodoma.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewashauri viongozi mbalimbali kufanya kazi zao kwa kuzingatia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuongeza kasi katika kuwatumikia watanzania.

 Akizungumza leo tarehe 10 Januari, 2022 Ikulu jijini Dodoma mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwaapisha viongozi mbalimbali wakiwemo Majaji watatu, Jaji Mkuu ameiomba Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia kuwezesha matumizi ya Teknolojia kwa kujenga miundombinu bora ya Tehama. 

Katika hafla hiyo, Jaji Mkuu pia alimshukuru Rais Samia kwa imani kubwa aliyoionesha kwa Muhimili wa Mahakama kwa kuwateua waheshimiwa Majaji watatu na Mtendaji wa Mahakama mmoja kushika nyadhifa mbalimbali.

Katika uteuzi alioufanya hivi karibuni, Rais Samia alimteua Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Jacobs Mwambegele kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Mwanaisha Kwariko kuwa Mjumbe wa Tume hiyo na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sam Mpaya Rumanyika kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani. Mahakama walioteuliwa kushika nyadhifa hizo kuendelea kufanya kazi zao kwa kuzingatia Sheria na Katiba. "Tekelezeni majukumu yenu kwa kuzingatia viapo vyenu kama Majaji na Mahakimu”, alisisitiza. 

 Mahakama ya Tanzania tayari imeingia katika mfumo wa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika kazi zake za utoaji haki ambapo majengo ya zaidi ya 157 ya Mahakama kwenye maeneo mbalimbali nchini yameunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

 Majengo hayo ni ya ngazi mbalimbali kuanzia Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya pamoja na majengo ya baadhi ya Mahakama za Mwanzo yenye miundombinu rafiki na maumizi ya Tehama.

Mahakama inaendelea na ujenzi wa majengo bora na ya kisasa ya Mahakama ngazi mbalimbali ambapo ujenzi wa majengo hayo unazingatia kwa kiasi kikubwa uwekaji wa miundombinu ya Tehama ili kusogeza huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi na kurahisisha shughuli za utoaji haki.

Rais Samia aliwaapisha Baadhi ya Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mjumbe wa Tume hiyo pamoja na Jaji wa Mahakama ya Rufani.


Sehemu ya Viongozi walioapishwa leo wakiwa kwenye hafla hiyo Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma. Wa tatu kulia Katibu Tawala mpya wa mkoa wa Kilimanjaro Bw. Willy Machumu ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa rushwa na Uhujumu Uchumi. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Jacobs Mwambegele kuwa  Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mwanza Mhe. Sam Mpaya Rumanyika kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni