Jumatatu, 10 Januari 2022

RAIS SAMIA AWAAPISHA MAJAJI WATATU WA MAHAKAMA YA TANZANIA

 Na Artemony Tiganya Vincent - Mahakama, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 10 Januari, 2022 amewaapisha Majaji watatu wa Mahakama ya Tanzania kushika nyadhifa mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Walioapishwa ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Jacobs Mwambegele anayekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Mwanaisha Kwariko kuwa Mjumbe wa Tume hiyo na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Mhe. Sam Mpaya Rumanyika aliyeteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Aidha, Mhe. Samia amemuapisha aliyekuwa Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Bw. Willy Machumu kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Katika hafla hiyo, Rais Samia pia amewaapisha Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu.

Sherehe za kuwaapisha viongozi hao zimefanyika katika Ikulu ya Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Juma, Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Hussein Kattanga.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amewashauri viongozi walioapishwa kutekeleza majukumu ya Rais kwa weledi, uaminifu na uadilifu mkubwa.

Naye Naibu Spika, Mhe. Tulia Ackson aliwashauri viongozi wote walioapishwa kutekeleza majukumu yao kama wasaidizi wa Rais na si vinginevyo.  “Rais ni Mkuu wa nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu, hivyo uongozi wake hauko sawasawa na viongozi wengine wa Mihimili”, alifafanua.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Jacobs Mwambegele kuwa  Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Hafla hiyo imefanyika leo tarehe 10, Januari 2022 Ikulu jijini Dodoma.

Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Mwanaisha Kwariko akiapishwa kuwa Mjumbe  wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Hafla hiyo ilifanyika leo tarehe 10, Januari 2022 Ikulu jijini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Mhe. Sam Mpaya Rumanyika kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania. Hafla hiyo ilifanyika leo tarehe 10, Januari 2022 Ikulu jijini Dodoma.


Baadhi ya Viongozi walioapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 10 Januari, 2022 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, wa tatu kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Willy Machumu ambaye alikuwa ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

(Picha na Lydia Churi-Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni