Na Rosena Suka - Lushoto
Jaji Mkuu Mstaafu wa
Mahakama ya Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman amewashauri Mahakimu wapya kusimamia
kikamilifu Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania na uboreshai wa huduma
unaoendelea ili kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi.
Mhe. Chande alitoa ushauri
huo tarehe 18 Januari, 2022 alipokuwa akifungua mafunzo elekezi kwa Mahakimu
Wakazi 35, wakimwemo wapya walioapishwa hivi karibuni na Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma. Mafunzo hayo yanayoendeshwa na Chuo cha Uongozi
wa Mahakama Lushoto (IJA) ambayo yatafanyika kwa muda wa siku tano.
Jaji Mkuu Mstaafu
aliwaambia Mahakimu hao kuwa Mahakama ya Tanzania inawategemea katika kusimamia
mpango mkakati huo na uboreshaji wa huduma zinazotolewa mahakamani ili kuleta
mabadiliko chanya yanayotarajiwa kwa wananchi.
Mhe Chande aliwaeleza
Mahakimu kuwa taswira nzuri ya Mahakama za Mwanzo wanazoenda kuhudumu ambazo kwa
sasa zimebadilika, hivyo akawaomba waendelee kuzibadilisha na kuzifanya bora
zaidi ili ziweze kutoa huduma nzuri zaidi na kwa wakati kwa wananchi.
“Mahakama za Mwanzo
ndio zinatoa fursa kubwa zaidi juu ya haki kwa Watanzania kuliko ngazi zingine
za Mahakama kwa sababu zimetapakaa Tanzania nzima”, alisema Mhe. Chande.
Aidha, Jaji Mkuu
mstaafu huyo hakusita kuwakumbusha Mahakimu hao kuwa makini kwenye nguzo muhimu
ya uhuru wa kila hakimu na uhuru wa Mahakama kwa ujumla. Aliwasisitiza kuamua
mashauri yaliyo mbele yao kwa kuzingatia sheria, bila woga wala shinikizo.
“Watanzania wanataka
Mahakama huru inayotoa haki kwa wakati, Mahakama adilifu, Mahakama ambayo
inauwezo na Mahakama ambayo haina gharama kubwa, ”aliongeza Mhe. Chande.
Aliwaasa Mahakimu hao
kujua na kufuata taratibu zilizowekwa na Mahakama wakati wa uendeshaji wa
mashauri hadi kutoa uamuzi unaoongozwa na sheria bila kusahau kupata maoni
kutoka ya Wazee wa Baraza na kuainisha sababu walizozingatia kufikia uamuzi huo.
Kwa upande wake Mkuu wa
Chuo cha IJA, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani,
alisema Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ni kitovu cha mafunzo ya
kuwajengea uwezo watumishi wa kada mbalimbali wa Mahakama na wadau wa sheria
nchini.
Mkuu huyo wa Chuo alisema
mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mafunzo ya Taifa ya 2013 na
Mpango Mkakati wa Mahakama (2021/22-2024/25), Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya
Tanzania ya mwaka 2019 ambayo inaelekeza kila mtumishi anayeajiriwa, kupanda
cheo au kuteuliwa apate mafunzo elekezi kabla hajaanza majukumu mapya kwa lengo
la kuboresha huduma za Mahakama.
Mhe. Dkt.Kihwelo aliwaomba
Mahakimu hao kujitahidi kutoa huduma nzuri na kujiepusha na vitendo rushwa
kwani kwa sasa Mahakama zimeboreshwa kwa kuwa na majengo mazuri sana na hivyo huduma
ziendane na uzuri wa majengo hayo.
Akizungumza katika
uzinduzi huo, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt ameupongeza
uongozi wa Mahakama kwa programmu za uboreshaji wa huduma zinazofanyika,
ikiwepo kuwekeza kwenye raslimali watu ambapo Chuo kimekuwa kikifanya kwa vitendo kuwajengea
uwezo watumishi mbalimbali ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi na
weledi.
Jaji Mkuu Mstaafu wa
Mahakama ya Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman akifungua mafunzo elekezi kwa
Mahakimu Wakazi Wapya leo tarehe 19 Januari, 2022 yanayoendeshwa na Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Mkuu wa Chuo cha IJA, Mhe.
Dkt. Paul Kihwelo, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani akitoa neno la
utambulisho kwa washiriki hayo.
Msajili wa Mahakama Kuu
ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt akitoa utambulisho wa vingozi mbalimbali
waliohudhuria nufunguzi wa mafunzo hayo.
Mhe. Chande Othman Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania akiwa katika picha ya pamoja na wawezeshaji Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu Wakazi Wapya yanayoendeshwa na Chuo cha UongoziwaMahakamaLushoto. Waliokaa kushoto ni Mkuu wa Chuo cha IJA, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na kulia Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni