Alhamisi, 20 Januari 2022

JAJI MKUU ATETA NA VIONGOZI WAPYA WA JMAT

 Na Faustine Kapama, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 20 Januari, 2022 amekutana na viongozi wapya wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) na kuahidi kuwapa ushirikiano ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu na pia kushughukikia, pamoja na mambo mengine, changamoto mbalimbali zinazowakabili, ikiwemo suala la mishahara na maslahi mengine.

Akizungumza na viongozi hao ofisini kwake Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam walioongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. John Kahyoza, Jaji Mkuu alizitaja baadhi ya changamoto hizo ikiwemo hoja inayohusu mishahara na maslahi kwa Majaji na Mahakimu.

“Mmeahidi kuleta ulinganifu wa mishahara ya Majaji na Mahakimu kutoka Kenya, Uganda, Zanzibar ili tunapopeleka mapendekezo yetu serikalini tuanishe kiwango kinachoweza kukidhi kazi ngumu ambayo mnafanya. Kwa hiyo, mimi naahidi kuwa nitapokea changamoto zenu na nitaziwasilisha mbele ya Tume ya Utumishi wa Mahakama ambayo itazifikisha kwenye mamlaka inayohusika na maslahi na mishahara,” amesema.

Jambo jingine la msingi ambalo liliongelewa na kuwasilishwa kwake, ambapo ameahidi kulifanyia kazi, ni baadhi ya Mahakama za Mwanzo na Wilaya kuwa katika maeneo ya mbali yenye changamoto ya usafiri na ugumu wa kupatikana mitandao, jambo ambalo viongozi wa chama hicho wameomba eneo hilo kuangaliwa, hasa katika kurahisisha utendaji kazi kwa kuzingatia Mahakama kwa sasa inatumia zaidi mifumo ya teknolojia.

Kwa mujibu wa Mhe. Prof. Juma, eneo jingine lilioongelewa linahusu kujiendeleza kwa kuzingatia Mahakimu wengi walijiunga na Mahakama ya Tanzania kwa miaka mingi iliyopita na hawajapata fursa ya kujiendeleza, hivyo wakaomba Mahakama ichukue jukumu la kuwaendeleza kuhakikisha mara baada ya kustaafu wawe katika kiwango kizuri cha elimu.

“Jambo hili tumelipokea na tutalifanyia kazi,” Jaji Mkuu alisema na kubainisha hoja nyingine inayohusu uboreshaji wa huduma za kimahakama zinazoendelea ikiwepo kubadilisha mfumo uliokuwepo ili kuwawezesha Mahakimu wenye Shahada ya Sheria kuanza kusikiliza Mashauri katika Mahakama za Mwanzo, hatua ambayo imesababisha wengi wa Mahakimu waliokuwa wakihudumu katika Mahakama hizo kwa muda mrefu ambao hawana hiyo sheria kubaki katika ngazi zile zile za kimshahara.

“Ingawa uboreshaji huu ni mzuri kwa nchi na kwa Mahakama, lakini umewasahau. Kwa hiyo, mmesisitiza kuangalia eneo hili kuhakikisha hawa Mahakimu ambao wamefanya kazi kwa muda mrefu na kwa uaminifu mkubwa hawabaki katika ngazi ya kusahaulika kimshahara na kimaslahi. Nahidi masuala yote ambayo mmeyaibua yatajadiliwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama na tutawapa mrejesho,” alisema.

Amewapongeza Majaji na Mahakimu kwa kuwapata viongozi wapya ambao wataongoza chama hicho kwa muda wa miaka mitatu ijayo. Jaji Mkuu alibainisha kuwa yeye kama mlezi wa chama hicho ataendelea kushirikiana na JMAT na kuwaunganisha na vyama vingine vya Majaji na Mahakimu wa Afrika Mashariki na katika Jumuiya ya Madola.

Viongozi wa JMAT waliochanguliwa tarehe 18 Desemba, 2021 kuogoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitatu na vyeo vyao kwenye mabano ni Mhe. Kahyoza (Rais), Mhe. Shaibu Mzanda (Makamu wa Rais), Mhe. Lazaro Magai (Katibu), Mhe. Frank Lukosi (Mweka Hazina) na Mhe. Nemes Mumbuli (Katibu Mwenezi).

Awali, Rais wa JMAT, Mhe. Kahyoza alielezea madhumuni ya kukutana na Jaji Mkuu wa Tanzania, ambaye ndiye Mlezi wa chama hicho, ikiwemo kujitambulisha kama viongozi wapya, kupata maelekezo na matarajio kutoka kwake katika kipindi chao cha uongozi na kuomba ushirikiano kwa mambo mbalimbali ili waweze kutekeleza kikamilifu malengo ya kuanzishwa kwa chama hicho.

Aliyataja baadhi ya malengo hayo kama kukuza na kulinda uhuru wa Mahakama. Amesema kuwa anaamini wanachama wakifanya kazi katika mazingira ambayo ni huru wataweza kutekeleza majukumu yao kwa ukamilifu, ikiwemo kulinda haki za binadamu na raia. Mhe. Kahyoza alisema pia kuwa chama chao kinahakikisha wanachama wake wanazingatia maadili, ndiyo maana mwaka 1984 JMAT iliweka kanuni za maadili kwa wananchama wake.

Hata hivyo, alibainisha kuwa jambo hilo kwa sasa limechukuliwa na Mahakama ya Tanzania yenyewe ambapo imetoa kanuni kwa Majaji na Mahakimu, hivyo kufanya kanuni za JMAT za mwaka 1984 kuacha kutumika. Amesema katika eneo hilo ambalo kuna kanuni mpya zilizotayarishwa chama kitachukua jitihada za kuwaelemisha wananchama wao ili wazielewe na kuzitumia katika kutekeleza majukumu mbalimbali.

Mhe. Kahyoza alielezea lengo lingine la kuanzishwa kwa chama hicho ni kukuza, kutetea na kulinda maslahi na haki za wanachama, kwa kuzingatia Majaji na Mahakimu hawapo katika vyama mbalimbali vya wafanyakazi vinavyojishughulisha na kupigania haki na maslahi ya wafanyakazi hapa nchini.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na viongozi wapya wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT)  walipofika ofisini kwake Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam leo tarehe 20 Januari, 2022. Kulia kwa Jaji Mkuu (wa kwanza) ni Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Temeka kinachojishughulisha na mashauri ya kifamilia, Mhe Ilvin Mugeta, ambaye ni Makamu wa Rais mstaafu wa JMAT, ambaye alihudhuria mazungumzo hayo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimsikiza kwa makini Rais mpya wa JMAT, Mhe. John Kahyoza, ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma (hayupo katika picha), alipokuwa akitoa maelezo kwa ufupi kuhusu madhumuni ya viongo hao kumtembelea ofisini kwake.

Rais mpya wa JMAT, Mhe. John Kahyoza, ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo katika picha).


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa JMAT. Kushoto kwa Jaji Mkuu ni Rais mpya wa JMAT, Mhe. John Kahyoza na Mhe. Lazaro Magai. Kulia kwa Jaji Mkuu ni  Makamu wa Rais, Mhe. Shaibu Mzanda, akifuatiwa na Mweka Hazina, Mhe. Frank Lukosi na Katibu Mwenezi, Mhe. Nemes Mumbuli.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni