Na Lydia Churi- Mahakama
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani amewataka watumishi
wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kuwa na nidhamu ya hali na kuhakikisha wanatekeleza
majukumu yao ipasavyo ili waweze kutimiza malengo ya Taasisi hiyo.
Akifungua
Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama uliofanyika jijini
Dodoma, Jaji Kiongozi ambaye pia ni Mjumbe wa Tume hiyo amesema Taasisi yoyote
ambayo watumishi wake hawana nidhamu ni ngumu kutimiza malengo yake.
“Nidhamu
ni muhimu sana kwa watumishi na hasa wa Tume hii, bila nidhamu malengo ya taasisi
hayawezi kutimizwa, na watumishi wasipokuwa na nidhamu husababisha malalamiko kuongezeka”,
alisisitiza Jaji Kiongozi.
Aliwataka
watumishi wa Tume hiyo kutofanya kazi kwa mazoea na badala yake wawatumikie
wananchi kwa kuwa nafasi za kazi walizonazo ni dhamana waliyopewa.
Aidha,
Jaji Siyani aliwapongeza watumishi wa Tume hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya na
kuwataka kuendelea kutoa miongozo na kanuni kanuni mbalimbali ili Mahakama ya
Tanzania itekeleze majukumu yake ya utoaji haki ipasavyo na kwa kwa mujibu wa
sheria.
“Kila
Mtumishi wa Mahakama aweke malengo ya kazi na kuyatimiza, Tume ya Utumishi wa
Mahakama itaendelea kusimamia kuona watumishi wanatekeleza majukumu yao na isiwavumile
wale wachache wanaosababisha malalamiko kuongezeka”, alisema.
Kuhusu
matumizi ya Tehama, Jaji Kiongozi aliwataka watumishi hao kuongeza kasi katika
matumizi hayo ili kurahisisha utendaji kazi na kuongeza uwazi katika shughuli
za utoaji wa haki. Alisema hivi sasa Mahakama ya Tanzania inaendelea na ujenzi
wa majengo ya bora na ya kisasa ya Mahakama ambayo yanazingatia uwekaji wa
miundombinu ya Tehama.
Naye
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni Katibu wa Tume ya Utumishi
wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka watumishi wa Tume hiyo
kutekeleza majukumu yao kwa nidhamu na kufahamu kuwa tume hiyo ndiyo
inayosimamia utendaji kazi wa Mahakama.
“Mjikite
zaidi kwenye matumizi ya Tehama yatakayowasaidia kupunguza mzigo wa kazi na
kuongeza uwazi zaidi. Mwezi Februari mwishoni tutaingia kwenye matumizi ya
Ofisi Mtandao pamoja na mifumo mingine ya Tehama”, alisema.
Alisema
Mahakama itaboresha maslahi ya watumishi wa Tume hiyo na kufanya jitihada za
kuongeza idadi ya watumishi. Tume ya Utumishi wa Mahakama inapaswa kuwa na
idadi ya watumishi 34, hivyo hivi sasa kuna upungufu wa watumishi 15.
Kuhusu
Uviko 19, Mtendaji Mkuu wa Mahakama amewataka watumishi hao kuchukua tahadhari
dhidi ya ugonjwa huo na kuwashauri kupata chanjo na kutokuwa na hofu za chanjo
hiyo bila ya sababu za msingi.
Tume
ya Utumishi wa Mahakama imeanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na Sheria ya
Uendeshai wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani (katikati) ambaye pia ni Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama akiwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (Katibu wa Tume) wakiimba pamoja na watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wimbo wa Mshikamano wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume hiyo uliofanyika jijini Dodoma. Jaji Kiongozi alifungua Mkutano huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni