Na Faustine Kapama, Mahakama-Dodoma
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe, Dkt Hussein Mwinyi leo tarehe
23 Januari, 2022 amezidua maadhimisho ya Wiki ya Sheria na kuwakumbusha
watumishi wa Mahakama ya Tanzania na wananchi wote kwa ujumla umuhimu wa
kuzingatia maadili katika utoaji haki na kuheshimu sheria ili kujenga umoja,
amani na mshikamano na kufanikisha shughuli mbalimbali za kiuchumi, kibiashara
na kiuwekezaji.
Akizungumza
katika maadhimisho hayo, Mhe. Mwinyi amebainisha kuwa kwa nafasi yake kama Rais
wa Zanzibar, ambaye ameitumikia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ngazi
mbalimbali za uwaziri, anatambua na kuheshimu muhimu wa sheria kwa pande zote
mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na anafahamu umuhimu wa sheria katika
kujenga umoja, amani, udugu na mshikamano, hivyo mafanikio ya kiuchumi,
kibiashara na kiuwekezaji hutegemea
kuwepo kwa misingi ya utawala bora, sheria na uhuru wa Mahakama.
“Ni
dhahiri kuwa ustawi wa wananchi wetu, pamoja na mambo mengine, kwa kiasi
kikubwa unategemea kuwepo kwa sheria madhubuti inayotambua ukweli kuwa wananchi
wengi kutoka pande zote mbili za Muungano ni maskini. Kwa hiyo, wanategemea
sheria zetu na taratibu za kimahakama zitasaidia kuwainua na kufanikisha
shughuli zao kiuchumi na za kijamii. Kuwepo kwa sheria bora zinazosimamiwa
vyema ndiko kutafanikisha uchumi wao, biashara na shughuli zao za kila siku za
kujitafutia kipato,”amesema.
Rais
Mwinyi alikumbushia pia kuwa katika hotuba zake toka achaguliwe kuwa Rais wa
Zanzibar amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuheshimu sheria kwa vile anatambua kuwa miongoni mwa mambo
yanayodhoofisha misingi ya utawala bora ni kuwepo kwa vitendo vya rushwa,
ubadhirifu, uzembe, kukosa uwajibikaji na kutofuata sheria na kukiukwa kwa
maadili.
“Nachukua
fursa hii kupongeza jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na Mahakama ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha huduma za kutoa haki kwa wananchi na
kuhakikisha mnaongeza kasi ya kusikiliza mashauri mbalimbali yanayowasilishwa
katika ngazi zote za Mahakama,”
amesema.
Mhe.
Dkt Mwinyi pia amepongeza hatua ya kuanzisha Mahakama inayotembea kwani
imesaidia kuweza kuwafikia wananchi wa maeneo mbalimbali na kunufaika na huduma
hiyo. Kadhalika, amepongeza hatua zilizoanza kuchukuliwa za kutafsiri sheria
kwa lugha ya Kiswahili, jambo ambalo kufurahiwa na kuwapa Watazania matumaini kama
hatua mojawapo ya maendeleo ya sekta ya sheria nchini. Hivyo, ameshauri kuongeza
jitihada za kupata wataalam wa lugha ya alama pamoja na kuimarisha miundombinu
inayozingatia uwepo wa Watanzania wenye mahitaji maalum, wakiwemo watu wenye
ulemavu wa aina tofauti.
Rais
Mwinyi pia ameelezea kuridhishwa na hatua ya ushirikiano iliyopo baina na
Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mahakama ya Zanzibar. “Nimeelezwa
kuwa uhusiano huo ni wa muda mrefu toka mwaka 1965. Nafurahi kuona kuwa
ushirikiano huo unaendelezwa kwa kupeana uzoefu na utaalam utakaoongeza ufanisi
katika utekelezaji wa majukumu yenu. Natoa wito kuendeleza ushirikiano huo kwa
lengo la kuwa chachu ya kuleta mabadiliko ya utendaji na kuongeza kasi na
ufanisi katika Mahakama zetu,” alisema.
Mhe.
Dkt Mwinyi amepongeza mafanikio makubwa aliyoyaona wakati akitembelea maonesho
yaliyoandaliwa kwa ajili ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria, ambapo ameelezwa kuwa
huduma zinazotolewa katika juma lote la maonesho ni moja ya utekelezaji wa
nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama na malengo makuu ya nguzo hiyo ni
pamoja na kuimarisha imani ya wananchi na kuongeza uelewa na ufahamu wao wa
taratibu na shughuli za utoaji haki nchini.
Hivyo,
amekubaliana na uamuzi wa kuzidi kutoa taaluma kuhusu huduma za Mahakama kwani
bado haijawafikia wananchi walio wengi. Amebainisha kuwa ni wazi wananchi
watanufaika na huduma hiyo, hivyo ametoa wito kwa wananchi wote kuitumia fursa iliyopo
vizuri kwa kufika kwa wingi kwenye maonesho hayo. Mhe. Dkt Mwinyi amekiri kuwa
maandalizi ya maonesho aliyoyaona kuanzia mpangilio wa mabanda yenyewe, huduma
zinazooneshwa, elimu inayotolewa na weledi wa watoa elimu hiyo ni ishara nzuri
kuwa kazi kubwa ya matayarisho imefanyika.
“Kupitia
maenesho haya pia nimeshuhudia uboreshaji makubwa unaofanywa na unaoendelea
kufanywa katika mnyororo mzima wa utoaji haki. Ni dhahiri kuwa uboreshaji mkubwa
niliyoshuhudia ya matumizi ya TEHAMA ni dalili njema ya matayarisho makubwa ya
kupokea na kuendeleza matumizi ya TEHAMA ndani ya Mahakama zetu. Natoa pongezi
za kipekee kwa uongozi wa Mahakama ya Tanzania na watumishi wote kwa kuendeleza
uboreshaji huu mkubwa,” amesema.
Mhe.
Dkt Mwinyi pia alitumia fursa hiyo adhimu ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria kutoa
wito kwa wanasheria na wataalam wote wa sheria, viongozi wa Mahakama na
Watumishi wote wa sekta ya sheria kuielewa na kuifanyia kazi mipango mikuu ya
uchumi inayotekelezwa na Serikali zote mbili nchini katika jitihada za
kupunguza umaskini na kuwa na uchumi unaolingana na ushindani wa karne ya 21,
hivyo kuwa huru kutoa ushauri wao wa kisheria kwa lengo la kuifanikisha.
“Tunatambua
kuwa zipo sheria ambazo huenda zikawa ni kikwao cha kufikia matarajio yetu ya
kiuchumi na ustawi wa jamii. Sheria hizo zitahitaji kufanyiwa marekebisho ili
zifanikishe mipango yetu ya uchumi wa kisasa. Kwa hiyo, tumieni utaalam wenu
kuzishauri Serikali zetu kuchukua hatua za kurekebisha sheria ambazo
zinakasoro, nasi tutafanya hivyo kwa maslahi mapana ya nchi yetu na Watanzania
wote,” alisema.
(Picha na Innocent Kansha-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni