Jumanne, 25 Januari 2022

MAHAKAMA MOROGORO KWENDA NA MABADILIKO: JAJI NGWEMBE

 Na. Evelina Odemba - Morogoro

Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, tarehe 24 Januari, 2022 imezindua Wiki ya Sheria ambapo Jaji Mfawidhi, Mhe. Paul Ngwembe amewahakikishia Watanzania kuwa hawatabaki nyuma katika kutekeleza jukumu ya utoaji haki na wapo tayari kwenda na mabadiliko yatokanayo na Mapinduzi ya Nne ya Viwanda.

Akizungumza mara baada ya kushiriki matembezi yaliyoadaliwa kuzindua Wiki ya Sheria ambayo imeazimishwa na Mahakama ya Tanzania katika maeneo ya Kanda mbalimbali kote nchini. Mhe. Ngwembe amesema kuwa Mahakama Mkoani Morogoro haipo nyuma kwenye mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea hivi sasa.

“Tayari tumefunga televisheni tatika gereza la Mahabusu ambapo mashauri mbalimbali yameanza kusikilizwa kupitia mtandao (video conference) huku mahabusu akiwa gerezani na Hakimu akiwa Mahakan. Jambo hili inaokoa muda na gharama za kuwasafirisha Mahabusu kufika Mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa,” amesema.

Aidha Jaji Mfawidhi huyo aliongeza kuwa kwa sasa nakala za hukumu hutolewa siku ya kusomwa kwa hukumu na ili kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa Mahakama imenunua Kompyuta Mpakato kwa Waheshimiwa Mahakimu kote nchini kuwarahisishia kuandika hukumu kwa wakati.

Mhe. Ngwembe alitumia fulsa hiyo kuwakaribisha wananchi wote kufika katika vituo vya kutolea elimu ili waweze kujifunza maswala mbalimbali yanayohusu Mahakama pamoja na wadau wake.

Alivitaja vituo hivyo kuwa ni viwanja vya Mahakama Kuu- Kituo Jumuishi( IJC)- Kihonda -Morogoro, viwanja vya shule ya msingi kiwanja cha Ndege, Soko kuu la Kingalu, stendi kuu ya mabasi Msamvu na soko la Chamwino.

Uzinduzi huo wa Wiki ya Sheria unaenda sambamba na maonesho yaliyoandaliwa na wadau mbalimbali ambao kwa takribani siku tano watakuwa wakitoa elimu ya sheria pamoja na huduma za kisheria kwa wananchi bila malipo yoyote.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, ambaye alitegemewa kuwa Mgeni Rasmi wakati wa uzinduzi huo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Morogoro Bi. Lucy John alitoa pongezi kwa uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kubuni kauli mbiu ambazo zimekuwa zikitambua changamoto mbalimbali wanazopitia wananchi.

Aliongeza kuwa kauli mbiu hizo zimekuwa zikitumiwa na Mahakama katika kuboresha huduma zake. Alisema kuwa ni dhahiri kuwa kujengwa kwa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki katika maeneo mbalimbali nchini utarahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati.

Katika uzinduzi huo Mgeni rasmi pia alipata nafasi ya kutembelea mabanda ya wadau Mbalimbali ambayo yameshiriki kuadhimisha wiki hii kwa kutoa huduma kwa wananchi. Miongoni mwa washiriki ni ofisi ya wanasheria wa serikali, wanasheria wa kujitegemea,  polisi, Rita, TARURA, TANROA na wengine

Maadhimisho ya wiki ya sheria yalianza rasmi mnamo mwaka 1997 ikiwa na malengo ya kuwaleta wananchi wote karibu na Mahakama, kutoa elimu ya sheria kwa wananchi, sambamba na wanasheria hutoa huduma ya kisheria kwa wananchi bila malipo ikiwa ni njia ya kurudisha mchango wao kwa jamii.

Maadhimisho haya kila mwaka huambatana na kauli mbiu ambapo kwa mwaka huu kauli mbiu ni  “zama za Mapinduzi ya nne ya viwanda: safari ya maboresho kuelekea Mahakama Mtandao.”

 

Katibu Tawala wa Wilaya ya Morogoro Bi. Lucy John akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Wiki ya Sheria inayoazimishwa kuanzia tarehe 24 Januari, 2022 katika Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro. Kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Paul Ngwembe akiwatangazia wananchi kuanza maadhimisho ya kwa wiki hiyo.


Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro wakifurahia jambo mara baada ya kushiriki matembezi ya wiki ya sheria.

Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Said Kalunde (kushoto) na Mhe. John Chaba wakiwasili katika Kituo cha kutolewa elimu ya sheria kwa wananchi mara baada ya kushiriki matembezi ya Wiki ya Sheria.


Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mwasiliano (TEHAMA) wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, Bw. Tamimu Hussein akitoa maelezo namna ya kusajili mashauri kwa njia ya mtandao.



Katibu Tawala wa Wilaya ya Morogoro Bi. Lucy John (kulia) akiwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Sheria.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni