Jumanne, 25 Januari 2022

ACHENI KUCHUKUA SHERIA MKONONI: JAJI KIONGOZI

 Na Faustine Kapama, Mahakama-Dodoma

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amewataka wananchi kutumia Mahakama zilizopo nchini kama njia sahihi ya kutafuta haki badala ya kujichukulia sheria mkononi kutatua migogoro inayowakabili.

Akizungumza muda mchache kabla ya kuzindua Mahakama ya Wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma leo tarehe 25 Januari, 2022, Mhe. Siyani ameonyesha kusikitishwa na tukio la mauaji ya watu watano wa familia moja lililotokea hivi karibuni katika Kijiji cha Zanka Wilaya ya Bahi mkoani humo.

“Tukio hili na mengine mengi yanayotokea katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu ni ya kusikitisha. Katika wakati ambao Mahakama ya Tanzania inasogeza huduma zake karibu na wananchi, ni aibu kwa wananchi hao kutozitumia Mahakama zetu na kuamua kuchukua sheria mkononi,” amesema.

Jaji Kiongozi ametoa rai kwa watanzania wote kupitia hadhara hiyo kuacha vitendo hivyo na kufuata sheria. “Acheni kuchukua sheria mkononi. Amani tuliyonayo ndiyo tunu yetu,” amesema alipokuwa anaongea na wananchi wa Wilaya ya Chemba waliofurika kushuhudia uzinduzi huo.

Amesema kuwa kila Mtanzania anao wajibu wa kulinda amani iliyopo na kwamba vitendo vya kujichukulia sheria mkononi hupelekea uvunjifu wa amani, hivyo ni vema wananchi kuzitumia Mahakama zilizopo wanapokuwa na migogoro inayohitaji uamuzi.

Aidha, Mhe, Siyani aliwataka watumishi wa Mahakama na wadau wote wa sheria kuchukua hatua kulinda na kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama ambapo Wasajili, Watendaji na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wanapaswa kutatua matatizo ya wananchi.

“Msijifungie, bali vaeni viatu vyao na wasikilizeni. Wananchi wakijenga imani kwa Mahakama zetu hawatachukua sheria mkononi. Siku hizi kero dhidi ya Mahakama huwasilishwa kwa njia nyingi. Mtazikuta kwenye Istagram, twitter au mitandao mingine ya kijamii. Msipuuze, zichukueni na kuzifanyia kazi,” amesema.

Jaji Kiongozi aliendelea kuwaasa viongozi hao na kusema, “Kama umeona kero imeibuliwa lakini haikuwa kwenye eneo lako, kuwa kama mcheza mpira, mpasie mwenzako aliye kwenye eneo linalolalamikiwa. Sote tuwajibike. Mahakama inaweza tu kuheshimika kama itakuwa kimbilio la wanyonge na haiwezi kuwa hivyo kama haisikilizi matatizo yao.”

Akizungumzia uzinduzi wa jengo hilo la Mahakama ya Wilaya Chemba, Jaji Kiongozi amesema kuwa hatua hiyo ni mwendelezo wa uzinduzi wa majengo ya Mahakama katika maeneo mbalimbali nchini katika safari ya uboreshaji wa huduma ambao Mahakama ya Tanzania imeamua kwa dhati kufanya kwa kujenga na kukarabati miundombinu yake.

Kwa mujibu wa Mhe. Siyani, kutokana na kumbukumbu zinazoanzia Desemba, 2019, hadi tarehe 25 Januari, 2022, Mahakama za Hakimu Mkazi Simiyu, Geita na Njombe; Mahakama za Wilaya za Chunya, Bukombe, Chato, Kilwa, Kondoa, Ruangwa Kasulu, Makete na Wanging’ombe, pamoja na majengo ya Mahakama Kuu Shinyanga na Kigoma yamezinduliwa.

Amebainisha kuwa miradi hiyo yote inayotekelezwa ni matokeo ya mikakati na mipango madhubuti ambayo Mahakama ya Tanzania imejiwekea kama taasisi kupitia Mpango Mkakati wa Mahakama wa Miaka Mitano (2015/16 – 2019/20), ambao mwaka huu umehuishwa kupitia Mpango Mkakati wa Mahakama wa Miaka Mitano (2020/21 – 2024/25), na Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Miundombinu ya Mahakama (2016/17 – 2020/21), ambao nao upo katika mchakato wa kuhuishwa, ili kuakisi uboreshaji wa miundombinu unaoendelea.

“Hata hivyo, ni wazi kwamba, utekelezaji wa mipango na mikakati hii, unatokana na kodi zenu wananchi wa Chemba na Watanzania wote kwa ujumla, fedha ambazo zinasimamiwa vizuri na Serikali yetu. Mahakama ya Tanzania inathamini na kutambua michango wa wananchi wote wa Tanzania wanaolipa kodi ambayo inaiwezesha Serikali kutekeleza miradi ya kimkakati, ikiwemo majengo ya Mahakama. Ni matumaini yangu kwamba majengo haya yanayojengwa kwa fedha za wananchi, yatatumika kutoa haki kwa kila Mtanzania na kwa wakati,”amesema.

Akimkaribisha Jaji Kiongozi kuongea na wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Mahakama hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdeme ameeleza kuwa Mahakama hiyo itaweza kuhudumia zaidi ya wananchi 235, 000 ambao wametawanyika katika Kata 26 Vijiji 114 na Vitongoji 488.

Akizungumza katika hafla hiyo, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martin Chuma aliuomba uongozi wa Wilaya ya Chemba kutenga maeneo kwa ajili ya kujenga makazi ya watumishi wa Mahakama, huku Mtendaji Mkuu wa Mahakakama, Prof. Elisante Ole Gabriel akiuhakikishia umma kuwa makazi hayo yatakayojengwa yatakuwa mazuri na ya kisasa kabisa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Mhe. Simon Chacha aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kufikia uamuzi wa kujenga jengo la kisasa ndani ya wilaya yake ambalo linajumuisha Mahakama Wilaya na Mahakama ya Mwanzo, hivyo kutatua changamoto iliyokuwa inawakabili wakazi wa eneo hilo ambapo walikuwa wakilazimika kutumia muda mrefu na gharama kubwa ya kufuata huduma za utoaji haki katika Wilaya ya Kondoa.

Awali, akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Bi Maria Itala alimweleza Jaji Kiongozi kuwa mradi huo ulijumuisha ujenzi wa majengo mawili, ikiwemo jengo kuu la Mahakama na choo cha nje ambavyo kwa pamoja yamegarimu zaidi ya millioni 797 za Kitanzania.

Alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo ulianza tarehe 12 Mei, 2020 ambapo Mkandarasi alikabidhiwa eneo la ujenzi na kuanza mara moja kazi hiyo. Bi. Ilata alisema pia kuwa mradi huo ulikamilika na ukaguzi wa mwisho ulifanyika na kukabidhiwa rasmi tarehe 12 Octoba, 2021 na mpaka sasa upo katika kipindi cha matazamio.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (aliyeshika mkasi) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa jengo linalojumuisha Mahakama ya Wilaya na Mwanzo Chemba kwenye hafla iliyofanyika leo tarehe 25 Januari, 2022. Uzinduzi wa jengo hilo ulishuhudiwa na viongozi waadamizi wa Mahakama na Serikali.


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akizungumza na wananchi (hawapo katika picha) wakati wa uzindiuzi wa jengo hilo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdeme akimkaribisha Mhe. Siyani kuongea na wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Mhe. Simon Chacha akitoa salamu katika hafla hiyo.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Mahakama na Serikali na baadhi wa wananchi waliofika katika uzinduzi wa jengo hilo.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Mahakama na Serikali na baadhi wa watumishi wa Mahakama ya Chemba na Kondoa waliofika katika uzinduzi wa jengo hilo.



Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Bi Maria Itala akitoa maelezo mafupi ya namna mradi wa ujenzi wa jengo hilo ulivyotekelezwa. 
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martin Chuma akitoa salamu katika hafla ya ufunguzi wa jengo hilo. 

Mtendaji Mkuu wa Mahakakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa salamu fupi katika hafla ya uzinduzi wa jengo linalojumuisha Mahakama ya Wilaya na Mwanzo Chemba.

Sehemu ya wananchi kutoka Wilaya ya Chemba waliofika katika uzinduzi wa jengo hilo.
Kikundi cha Ngoma cha Changamoto kikitumbuiza katika hafla hiyo.


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (katikati) akiwasili katika viwanja vya jengo linalojumuisha Mahakama ya Wilaya na Mwanzo Chemba kwa ajili ya uzinduzi.

                        (Picha na Innocent Kansha - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni