Jumatano, 26 Januari 2022

NAIBU WAZIRI ATOA RAI VIELELEZO MAHAKAMANI KUTOHARIBIWA

 Na Lydia Churi-Mahakama

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geofrey Pinda ametoa rai kwa Taasisi mbalimbali za serikali zinazojihusisha na upelelezi na ukamataji wa wahalifu kuacha kuuza au kuharibu vifaa vilivyokamatwa ambavyo hutumika kama vielelezo mahakamani.

Akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kutembelea maonesho ya wiki ya Sheria yanayoenelea jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria amesema kitendo cha kuuza au kuharibu mali zilizokamatwa kabla ya shauri kumalizika mahakamani husababisha kuongezeka kwa malalamiko kutoka kwa wananchi.

“Chochote kilichokamatwa kama ushahidi kisiuzwe au kuharibiwa mpaka shauri litakapomalizika mahakamani ili kupunguza malalamiko ya wananchi”, alisisitiza Naibu Waziri Pinda.

Awali akitembelea mabanda mbalimbali ya Mahakama pamoja na wadau kwenye maonesho hayo, Mhe. Pinda aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa maboresho makubwa iliyoyafanya na inayoendelea kuyafanya tangu kuanza kwa Mahakama mpaka sasa.

“Tumejenga kwa kasi sana majengo mapya na ya kisasa ya Mahakama katika maeneo mbalimbali nchini na ifikapo mwaka 2025 wilaya zote zitakuwa na majengo ya kisasa na makao makuu ya kila tarafa kutakuwa na Mahakama ya Mwanzo”, alisema Mhe. Pinda.

Kwa upande wa wadau wa utoaji haki, Naibu Waziri Pinda aliishauri ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kujipanga vizuri na kuhakikisha ushahidi unafikishwa mahakamani mapema ili usaidie mashauri kumalizika kwa wakati.

Kuhusu Magereza, Mhe. Pinda alisema unahitajika mkakati maalum ili kuwe na majengo ya kisasa yanayotosheleza mahitaji ya sasa kwa kuwa majengo mengi ni yale yaliyorithiwa kutoka kwa wakoloni. Aliongeza kuwa Serikali itaboresha majengo ya magereza nchini.

Mahakama ya Tanzania inaendelea na Maonesho ya wiki ya Sheria yaliyoanza  Januari 23-29, 2022 katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma. Aidha, siku ya Sheria nchini itaadhimishwa tarehe 1 Februari, 2022 ambapo mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geofrey Pinda akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa wa Mahakama (hayupo pichani) wakati alipotembelea banda la Maboresho ya Mahakama kwenye Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea kwenye viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geofrey Pinda akisikiliza maelezo alipotembelea banda la wadau wa Mahakama ambao ni Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea kwenye viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geofrey Pinda akiwa kwenye banda la Tume ya Utumishi wa Mahakama wakati alipotembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea kwenye viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geofrey Pinda akisikiliza maelezo alipotembelea banda la Magereza jana jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geofrey Pinda akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geofrey Pinda akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza kutembelea mabanda ya Mahakama pamoja na wadau wa Mahakama kwenye Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea jijini Dodoma.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni